Europa Ligi, mabingwa watetezi Atletico Madrid yaona mwezi
22 Oktoba 2010Kandanda.
Katika michuano ya ligi ya Europa jana Alhamis , viongozi wa ligi ya Ujerumani Bundesliga, Borussia Dortmund ilikubali goli la dakika ya mwisho la kusawazisha dhidi ya Paris St Germain na kutoka sare ya bao 1-1. Klabu ya Stuttgart ambayo iko mkiani mwa Bundesliga hadi sasa msimu huu ilipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya FC Getafe ya Hispania. Nayo Bayer Leverkusen ilitoka sare ya bila kufungana na Aris Saloniki kutoka Ugiriki. matokeo hayo yanaiweka Bayer Leverkusen katika nafasi ya juu ya kundi B wakati Aris imeendeleza rekodi yake ya kutofungwa nyumbani.
Mabingwa watetezi Atletico Madrid ilishinda kwa mara ya kwanza msimu huu katika kinyang'anyiro hicho kwa kuirarua Rosenborg kwa mabao 3-0 , nae Emmanuel Adebayor alipachika mabao matatu wakati Manchester City ilipofanikiwa kuiangusha Lech Poznan ya Poland kwa mabao 3-1.
Timu ya daraja la pili nchini Uswisi Lausanne, ikiwa nyuma kwa mabao 3-1 dhidi ya Sparta Prague katika dakika ya 23, iliweza kujikwamua na kutoka sare ya mabao 3-3 katika matokeo ya kushangaza usiku huo ambao timu zote nne za Italia zilishindwa kuwika.
Parlemo ilifanya vibaya zaidi ya timu nyingine za Italia wakati ilipochapwa mabao 3-0 nyumbani na CSKA Moscow, wakati Napoli walikabwa koo na Liverpool ya Uingereza na kutoka sare bila kufungana.
Zenit St. Petersburg, VfB Stuttgart, Porto na Sporting zote zilishinda na kuweka rekodi safi ya kushinda michezo yao yote hadi sasa pamoja na CSKA Moscow.
Katika mchezo mwingine wa kundi A Juventus Turin ilitoka sare ya bao 1-1 na Salzburg.
Mwandishi : Sekione Kitojo / RTRE
I