EURO bilioni 130 kwa Ugiriki
9 Machi 2012Wizara ya fedha ya Ugiriki imesema asilimia 83.5 ya wakopeshaji binafsi nchini humo, wamekubali kubadilishana hati za mkopo kwa hasara. Hii ni zaidi ya kiwango cha asilimia 75 serikali ya Ugiriki ilichokuwa imepanga kama sharti la kuendelea na mazungumzo ya kupatiwa mkopo wa pili.
Hasara asilimia 74
Sasa, wenye hati za mikopo watakubali kupata hasara ya karibu asilimia 74 ya thamani ya hati zao katika makubaliano yanayotizamiwa kupunguza zaidi ya euro bilioni 100 katika deni la Ugiriki. Serikali ya Ugiriki ilikuwa imesema ingewalaazimisha wenye hati za mikopo nchini humo kukubaliana na matakwa hayo, kwa kutumia vifungu vya uwajibikaji wa pamoja kwenye hati zenye thamani ya euro bilioni 177 zinazodhibitiwa chini ya sheria ya nchi hiyo.
Umoja wa Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) waliitaka Ugiriki ifanikishe makubaliano ya kubadilishana hati za mikopo kama sharti la muhimu la kupatiwa udhamini wa mwingine wa euro bilioni 130 zilizokubaliwa mwezi uliyopita.
Wakopeshaji kupata hati mpya
Kutokana na makubaliano hayo wadeni wote wa Ugiriki sasa watapata hati mpya za mikopo zenye thamani ya asilimia 31.5 ya mikopo iliyobadilishwa, pamoja na noti za miezi 24 kutoka mfuko wa kuokoa uchumi wa Umoaja wa Ulaya (ESF).
Dhamana hizi mpya zinakuja na riba ya asilimia 2.0 hadi mwaka 2015, asilimia 3.0 hadi mwaka 2020 na asilimia 4.3 kila mwaka baada ya muda huo, mpaka kipindi cha mwisho ambacho ni mwaka 2042.
Kwa makubaliano hayo, Ugiriki itapata mikopo yenye thamani ya euro bilioni 130 hadi mwaka 2014, ambapo bilioni 30 kati ya hizo zitakuwa kama dhamana kwa benki binafsi nchini humo kuendelea kushiriki katika mchakato wa kupunguza deni, kwa kusaidia kufidia hasara watakazozipata.
Mkopo huu unafuatia ule wa euro bilioni 110 uliyotolewa mwezi Mei mwaka 2010. Kiwango cha riba kwa mikopo ambayo imeshatolewa kw Ugiriki kitapunguzwa na hivyo kuisaidia nchi hiyo kuokoa kiasi cha euro bilioni 1.4.
Benki ya Ulaya yaonesha njia
Benki ya Umoja wa Ulaya, tayari imeshabadilishana na Athens, hati ya mkopo za mkopo iliyonunua kwa punguzo kubwa katika wakati mgogoro huu wa madeni ulipofikia hatua mbaya zaidi.
Faida ya thamani ya juu iliyopatikana kutoka kwenye mabadalishano hayo inaelekezwa kwenye nchi za kanda ya Euro ili itumike kama msaada kwa ugiriki. Kiasi hiki kinaaminika kuwa mamilioni ya euro.
Ugiriki kubana zaidi matumizi
Bunge la ugiriki nalo limekubali kuchukua hatua zaidi za kubana matumizi zinazotizamiwa kuokoa euro bilioni 3.3 mwaka 2012, hasa kutokana na kupunguza viwango vya chini vya mishahara na pia viwango vya akiba za uzeeni.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\AFPE
Mhariri: Mohamed Abdul Rahman