1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Euro 2016: Mapambano kuanza Ijumaa usiku

Sekione Kitojo10 Juni 2016

Tamasha la wazi la muziki lilifanyika mjini Paris Alhamisi kuadhimisha mkesha wa kuanza tamasha kubwa kabisa la soka barani Ulaya, michuano ya kuwania kombe la mataifa ya Ulaya, Euro 2016.

https://p.dw.com/p/1J478
Frankreich Paris Fans mit Fähnchen
Mashabiki wa Ufaransa mjini ParisPicha: picture-alliance/dpa/A. Morissard

DJ David Guetta aliwaburudisha maelfu ya mashabiki walioko mjini Paris kwa muziki, katika eneo la Champs de Mars, karibu na mnara maarufu wa Eiffel, ambao ulipambwa kwa taa zikitoa mwanga wa rangi tatu za bendera ya Ufaransa, bluu, nyekundu na nyeupe.

Mashindano ya kombe la bara la Ulaya yanafanyika mwaka huu nchini Ufaransa, na yamezingirwa na wasi wasi kuhusiana na usalama baada ya nchi hiyo kushambuliwa hivi karibuni na magaidi.

Michezo inaanza rasmi Ijumaa kwa wenyeji wa mashindano hayo Ufaransa watakapopambana na Romania katika uwanja wa Stade de France mjini Paris. Naibu meya wa jiji la Paris Jean Francois Martins amesema tusikubali kushindwa. "Iwapo tunataka ISIS kushinda , basi tuseme tu kwamba tunayafuta mashindano haya na kusema, ok mmeshinda."

Wasiwasi na migomo

Lakini mbali na masuala ya soka ambayo yamewavuta mashabiki kutoka nchi mbali mbali zinazoshiriki katika tamasha hilo na zisizoshiriki pia, pia kuna matatizo na wasi wasi wa migomo, ya wakusanyaji taka katika jiji la Paris na marubani wa ndege wanatishia kufanya mgomo.

Frankreich Paris Blick vom Eiffelturm auf Fanmeile
Umma wa mashabiki wa muziki walifurika katika mkesha wa ufunguzi wa Euro 2016 mjini ParisPicha: picture-alliance/abaca/R. Julien

Mbali na hali hiyo, rais Francois Hollande amesema atafanya kila lililo katika uwezo wake kuhakikisha maandamano hayaharibu mashindano hayo ya bara la Ulaya , Euro 2016 yanayoanza rasmi Ijumaa.

"Ufaransa ilichaguliwa kuwa wenyeji wa mashindano haya , na itafanya kwa mujibu wa kiwango kinachotakiwa," Hollande alisema, na kuongeza kufanyika bila matatizo kwa tukio hili la tatu kwa ukubwa dniani katika michezo pia utaionesha nchi hiyo ambayo pia inawania kuwa mwenyeji wa michezo ya Olimpiki ya mwaka 2024.

Serikali yake ilianza uangalizi kwa masaa 24 kabla ya mchezo wa kwanza wa tamasha hilo la mwezi mzima ambapo mamilioni ya mashabiki na watu kutoka nje ya nchi hiyo wanamatumaini ya kufuatilia, mbali na mizozo ya migomo ambayo baadhi imeathiri usafiri wa umma na ukusanyaji wa taka, na kuzuwia barabara muhimu za mji huo mkuu.

Frankreich Euro 2016 David Guetta Konzert in Paris
DJ Guetta akiwapelekesha mashabiki kwa muziki mjini ParisPicha: picture-alliance/AP Photo/K. Zihnioglu

Hata hivyo kabla ya mashindano hayo kuanza, baadhi ya mashabiki wameanza kutoa changamoto kwa polisi na walinzi wa usalama. Mashabiki wa Uingereza walipambana na polisi katika mji wa kusini wa Marseille, ambao utafanyika mchezo wa kombe la Ulaya kati ya Uingereza na Urusi kesho Jumamosi.

Wakati huduma za reli zimeanza kuwa bora wakati mgomo wa siku tisa ukipungua nguvu , wanaharakati wa chama cha mrengo wa kushoto cha SUD wanatishia kuvuruga safari za treni zitakazowachukua mashabiki kwenda katika mchezo wa ufunguzi kati ya Ufaransa na Romania Ijumaa.

Timu ya taifa ya Ujerumani "Die Manschaft" itaingia uwanjani siku ya Jumapili kupambana na Ukraine katika uwanja wa Stade Pierre Mauroy mjini Lille.

Mwandishi: Sekione Kitojo/rtre

Mhariri: Iddi Ssessanga