1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Euro 2016 kuanza chini ya ulinzi mkali

9 Juni 2016

Ufaransa inakabiliwa na changamoto yake kuu ya kwanza ya usalama wakati wa dimba la Kombe la Mataifa ya Ulaya, Euro 2016. Tamasha la wazi la ufunguzi linaandaliwa Paris katika eneo lenye uwezo wa kuwa na watu 90,000

https://p.dw.com/p/1J3rH
Frankreich Paris Eiffelturm UEFA Euro 2016
Picha: picture alliance/NurPhoto/M. Taamallah

Baada ya maandalizi ya muda mrefu ambayo yamekabiliwa na changamoto chungu nzima, hatimaye dimba la EURO 2016 linaanza kutifua vumbi Ijumaa nchini Ufaransa. Lakini katika habari ambayo huenda isiwafurahishe mashabiki ni kuwa wamiliki wa mabaa na mikahawa hawatoruhusiwa kuziweka nje skrini za televisheni wakati wa kipindi kizima cha michuano hii.

Hatua hiyo tata inalenga kuimarisha usalama wakati wa dimba hilo la mwezi mzima, wakati maafisa wa Ufaransa wanataraji kuwa watu wachache watakusanyika nje ya maeneo rasmi ya kukutana mashabiki ikiwa skrini za televisheni za nje zitapigwa marufuku.

Euro 2016 Fan Zone Champs de Mars Paris Frankreich Sicherheit Security
Maeneo ya kukusanyika mashabiki yana ulinzi mkaliPicha: picture-alliance/dpa/T.Vandermersch

Maeneo ya mashabiki kawaida huwekwa katika kumbi za wazi au bustani karibu na miji mikuu ya mji, na kuwawezesha mashabiki kutizama mechi kwenye skrini kubwa za televisheni. Hatua za zoada za usalama, ikiwemo mifumo ya video za siri, zimeongezwa ili kuweka usalama katika maeneo ya mashabiki.

Leo usiku, Dj maarufu wa Kifaransa David Guetta atautumbuiza umati chini ya mnara wa Eiffel mjini Paris, siku moja kabla ya wenyeji Ufaransa kushuka dimbani dhidi ya Romania katika mpambano wa ufunguzi wa kinyang'anyiro hicho uwanjani Stade de France.

Serikali ya Ufaransa imezindua app ya smartphone isiyo na malipo katika lugha ya Kifaransa na Kiingereza ambayo itawaonya wageni dhidi ya “mgogoro wowote mkuu”, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kutokea mashambulizi.

Frankreich Fußball EM Euro 2016 - Abflug deutsche Nationalmannschaf in Frankfurt a.M.
Timu ya Ujerumani imewasili UfaransaPicha: picture-alliance/Photoshot

Hata hivyo, wasiwasi mkubwa kwa sasa ni migomo ya wafanyakazi inayoendelea pamoja na mtafaruku wa kisiasa kuhusiana na mageuzi tata ya sekta ya kazi hali ambayo intarajiwa kuendelea licha ombi la serikali kwa vyama vya wafanyakazi kusitisha migomo hiyo.

Wafuasi wa vyama vya wafanyakazi wamevizingira vituo vya kuteketeza taka katikati ya Paris, na kusababisha mrundiko mkubwa wa taka ambazo hazijakusanywa katika maeneo kumi ya mji huo mkuu. Meya wa Paris Anne Hidalgo ameahidi kuirekebisha taswira hiyo

Wafanyakazi wa reli wamesema wataendelea kuvuruga huduma za usafiri wa matreni, na kuurefusha mgomo wao kwa siku ya tisa mfululizo mjini Paris na maeneo mengine nchini humo. Lakini licha ya hayo, mashabiki wote wa kandanda wanataraji kushuhudia dimba la kufana la Euro 2016.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/AP
Mhariri: Yusuf Saumu