1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EURO 2008 yazidi kupamba moto

Kalyango Siraj12 Juni 2008

Uswisi nje na Ujerumani uwanjani tena leo alhamisi

https://p.dw.com/p/EINh
Kocha wa Ujerumani Joachim Löw wakati wa mechi kati ya Ujerumani na Poland.Picha: AP

Kiny'anganyiro cha kutafuta ubingwa wa soka katika kombe la Ulaya la mwaka huu,kinaendelea huku mhanga wa kwanza akiwa amepatikana kutokana na matokeo ya jumatano. Kwa wakati huohuo leo alhamisi Ujerumani inaingia tena uwanjani.

Timu ya soka ya taifa ya Ujerumani inarejea tena uwanjani alhamisi jioni nchini Austria katika juhudi za kutafuta kibarua cha kusonga mbele katika mashindano yanayoendelea ya bara la Ulaya ya mwaka huu.

Ujerumani itacheza dhidi ya Croatia.

Mechi ambayo itachezwa jioni milango ya saa moja za Afrika mashariki itakuwa ya umuhimu kwa Ujerumani kwani kushindwa kwa Ujerumani kutavuruga nafasi yake ya kusonga mbele.

Pia Ujerumani itakuwa inaomba dua kuwa Poland, ilioilaza mabao mawili kwa bila katika mechi ya ufunguzi, iwashinde wenyeji Austria ili kuona kama inapanda kilele cha kundi hilo la B na hivyo kufunguliwa milango ya kuingia katika robo fainali.

Timu ya Ujerumani ambayo imezoea kupata ushindi itateremka uwanjani ikimtegemea mshambuliaji wake Lukas Podolski kufanya vitu vyake kama alivyofanya katika mechi ya fungua dimba dhidi ya Poland.

Hata hivyo ni lazima timu ya Ujerumani iwe na uangalifu katika mechi yake dhidi ya Croatia kwani timu hiyo ina wachezaji kadhaa ambao wanajua aina ya soka inayochezwa Ujerumani kwani inawachezaji kadhaa wanaochezea katika baadhi ya timu za ligi kuu za Bungesliga.Kocha wa timu ya Ujerumani,Joachim Löw,anasema kuwa Croatia si timu ya kuchezea.

'Tunachojua kwa sasa ni kuwa Croatia si ya kuchezea. Inawachezaji ambao wanauwezo wa kucheza kwa mbinu zote. Ni timu nzuri ilio na wachezaji wazuri,’amesema Löw.

Umuhimu wa mchezo wa leo kwa Ujerumani sio tu unazunguziwa na kocha lakini pia na washika dau wengine hasa wapenzi wa soka hapa Ujerumani.Moja wao ni mwandishi wa habari wa jarida la michezo ,mashuhuri hapa Ujerumani la SportBild, aitwae Jochen Coenen, 'Wachezaji sita wa Craotia wanacheza katika ligi kuu ya soka ya Ujerumani, na wanapata ujira wao nchini Ujerumani kwa hivyo mchezo wa leo ni muhimu sana kwa Ujerumani',amesema Coenen.

Mechi ya pili kwa leo alhamisi itakuwa kati ya moja wa wenyeji Austria dhidi ya Poland.Na itachezwa saa nne kasoro robo za usiku, saa za Afrika Mashariki.

Mechi hiyo itakuwa ya kufa na kupona kwa timu zote mbili kwani zitakuwa zinajaribu kuona angalau kila moja inapata ushindi ili iweze kusongambele .

Utaratibu ni kuwa timu ikishindwa mechi mbili za mwanzo inakuwa vigumu kusonga mbele katika duru ya robo fainali.Poland ililambishwa mbili kwa nunge na Ujerumani, huku Austria kulala moja bila dhidi ya Croatia.

Kwa mda huohuo mwenyeji mwingine Uswisi ameondolewa katika kiny'anganyiro hicho baada ya kupikuliwa na Uturuki jana jumatano kwa kuishinda mabao mawili kwa 1 katika kundi A.

Hii inaifanya Uswisi kuwa nchi ya pili miongoni mwa mataifa wenyeji wa mashindano hayo kuondolewa katika awamu hiyo.

Katika mashindano kama hayo, ya mwaka wa 2000, Ubelgiji kama mwanadalizi mwenza, ilishindwa kupita awamu ya kwanza.

Mechi ya jana jumatano kati ya Uturuki na Uswisi, ilichezwa katika uwanja uliojaa maji kutokana na mvua iliokuwa ikinyesha huku mchezo ukiendelea mbele.

Pia mechi hiyo ndiyo ya kwanza kati ya timu hizo mbili tangu miaka mitatu iliopita wakati timu hizo mbili zilipokutana mjini Istanbul na baadae kutokea fujo,ambapo rais wa shirikisho la soka duniani FIFA, Sepp Blatter,alitishia kuipiga marufuku Uturuki kutoshiriki katika kombe la dunia la mwaka wa 2010.

Kwa upande mwingine Ureno,ambayo inafundishwa na Luiz Felipe Scolari,imefuzu kwa duru ya robo fainali, baada ya kuibamiza Jamhuri ya Czech mabao 3 kwa 1.

Kwa mda huohuo, kocha huyo wa Ureno, Scolari, ameteuliwa kuwa kocha mkuu wa klabu ya soka ya Uingereza ya Chelsea. Miongoni mwa mafanikio yake ni kuiongoza Brazil hadi ushindi wa kombe la dunia mwaka wa 2002 na pia kuiongoza Ureno hadi fainali za kombe la Ulaya la mwaka 2004.