1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU aondoa mpango wa vikwazo kwa Urusi

21 Oktoba 2016

Umoja wa Ulaya umeuweka kando mpango uliolenga kuiongezea vikwazo Urusi kutokana na ushiriki wake katika mashambulizi yanayofanywa na utawala wa Syria na washirika wake mjini Aleppo, baada ya Italia kuupinga vikali.

https://p.dw.com/p/2RWBD
Belgien | Donald Tusk auf dem EU-Gipfel in Brüssel
Picha: picture-alliance/AP Photo/G. Vanden Wijngaert

Awali rasimu yake ilikuwa imesambazwa jana Brussels kwa viongozi wanaoshiriki mkutano wa kilele wa Umoja huo, ikiwataka viongozi hao kuangazia njia nyingine za kuishughulikia Urusi na Syria, ikiwa ni pamoja na hatua kali zitakazowalenga watu binafsi wanaounga mkono utawala wa Rais Bashar al-Assad.

Awali, pamoja na kupingwa vikali kwa mpango wa mashambulizi ya kijeshi nchini Syria yanayofanywa na Urusi, kwa lengo mahsusi la kuusaidia utawala wa Rais Assad, viongozi wa mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya wameshindwa kukubaliana na juu ya hatua ya pamoja ya kuionya Usuri kuhusiana na hatua kali zinazoweza kuchukuliwa dhidi yake. 

"Mkakati wa Urusi unalenga kuudhoofisha Umoja wa Ulaya", alisema Rais wa Baraza la Umoja huo, Donald Tusk, ambaye alikuwa akiongoza mkutano huo wa siku mbili mjini Brussels. Amesema, viongozi wa Umoja wa Ulaya kwa pamoja wamekuwa wakilaani mashambulizi dhidi ya raia yanayofanywa na serikali ya Syria na washirika wake wanaoongozwa na Urusi, na walitaka kusitishwa mara moja kwa mapigano, na kama wataendeleza ukatili huo wawe tayari kwa hatua zozote zitakazochukuliwa.

Rais Francois Hollande wa Ufaransa amesema lengo kuu hasa katika kipindi cha kusitisha mapigano mjini Aleppo ni kutafuta namna ya kuanzisha mazungumzo ili kumaliza ukatili ambao umeshuhudiwa kwa muda mrefu. Hata hivyo, naye ameongeza kuwa: "iwapo kutatokea ukatili mkubwa zaidi, hakutakuwa na mbadala zaidi ya kutumia njia zote", ingawa hakusema chochote kuhusu vikwazo.

Alipoulizwa kuhusiana na iwapo anaona umuhimu wowote wa kuongezwa kwa vikwazo, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani alisema "iwapo mashambulizi ya angani yataendelea dhidi ya Aleppo, ndipo sasa Ulaya itakuwa na sababu ya kuangalia namna nyingine ya kufanya.

EU Gipfel in Brüssel - Bundeskanzlerin Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amesema EU itafanya kila liwezekanalo kuendelea usimamishaji wa mapigano mjini Aleppo.Picha: Getty Images/AFP/T. Charlier

Kwenye mjadala baada ya chakula cha jioni, Waziri Mkuu wa Italia, Matteo Renzi, alisema haina maana yoyote kuamini ni kwa namna gani mzozo wa Syria unaweza kumalizwa kwa kuiwekea vikwazo zaidi Urusi. 

Kwa muda mrefu, viongozi hao wa Umoja wa Ulaya wamekuwa wakijipanga kurejelea uhusiano wao na Urusi ambao ulivurugika kutokana na hatua ya Urusi kuichukuwa Rasi ya Crimea iliyokuwa ikimiliwa na Ukraine na kisha kujihusisha na mzozo mashariki mwa nchi hiyo. Hata hivyo, mikakati ya kutaka kurejesha upya uhusiano huo imeingia gizani kwa mara nyingine kufuatia mpango wa Urusi wa kuunga mkono mashambulizi ya kutisha ya mabomu katika mji unaoshikiliwa na waasi wa Aleppo nchini Syria.

Kabla ya kuanza kwa mkutano huo, Waziri Mkuu wa Estonia, Taavi Roivas, alisema Urusi inatamani kuugeuza mji wa Aleppo kuwa kama Grozny mpya, akirejelea mashambulizi yaliyofanywa na Urusi dhidi ya mji mkuu wa Chechenya mwaka 1990 na ambayo yaliuharibu kabisa mji huo.

Mjadala kuhusu Urusi ulianza kwenye mkutano uliofanyika jioni ya Jumatano hii, mjini Berlin Ujerumani, ambapo Kansela Merkel na Rais Hollande walishindwa kuafikiana msingi wa pamoja na Rais Vladmir Putin wa Urusi.

Mjini Brussels, Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Donald Tusk, pia ameituhumu Urusi kwa kuvunja sheria za anga la Ulaya, kwa kufanya mashambulizi ya mtandaoni na kuingilia uchunguzi unaoongozwa na kampuni ya uchunguzi toka Uholanzi, inayowashutumu waasi wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine kwa kuitungua ndege chapa MH17 ya Malaysia na kusababisha vifo vya watu 298 miaka mitatu iliyopita.

Mkutano huo unatarajiwa kumalizika leo, kwa kuangazia eneo la biashara, wakati ambapo kuna wasiwasi kuhusu hatua ya Ubelgiji ya kutounga mkono Umoja wa Ulaya kusaini makubaliano ya kibiashara na Canada, CETA.

Mwandishi: Lilian Mtono/APE/DPAE
Mhariri: Mohammed Khelef