1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU yaitaka Saudia kutoa ufafanuzi zaidi mauaji ya Khashoggi

18 Novemba 2018

Umoja wa Ulaya umeiambia Saudi Arabia kutoa ufafanuzi kamili juu ya nauaji ya Mwandishi habari Jamal Khashoggi. Rais wa Marekani Donald Trump, mshirika wa karibu wa Saudia bado anasitasita kuibebesha lamawa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/38SpK
Jamal Khashoggi
Picha: Getty Images/C. McGrath

Mkuu wa sera ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini ameiambia hadharani Saudi Arabia Jumamosi jioni kwamba inahitaji bado kufafanua kikamilifu juu ya "uhalifu wa kinyama", licha ya mwanasheria mkuu wa Saudi Arabia kuelekeza kidole cha lawama kwa watuhumiwa watano.

Akiwa safarini kuelekea jimbo la California lililokumbwa na moto uliosababisha mafa makubwa Jumamosi, Rais Donald Trump alisema kupitia wizara ya mambo ya nje ya Marelani kwamba ripoti zilizosema serikali yake imefikia hitimisho la mwisho hazikuwa sahihi.

Trump mwenyewe aliwambia waandishi habari mjini Malibu kwamba ataarifiwa "yumkini Jumatatu au Jumanne," na kuongeza kuwa Saudi Arabia ni "mshirika wa kuvutia." "Mimi ndiye rais - Lazima nizingatie mambo mengi sana," Trump alisema.

Mauaji yaliamuriwa kutoka juu?

Siku ya Ijumaa gazeti la Washington Post lilisema shirika la uchunguzi wa uhalifu la Marekani CIA, lilihitimisha kwamba mrithi wa kiti cha ufalme Mohammed bin Salman aliamuru mauaji hayo yafanyike - madai ambayo awali yalikanushwa na naibu mwendesha mashitaka mkuu Shalaan al-Shalaan.

Saudi-Arabien - Saudischer Kronprinz Mohammed bin Salman
Mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia Mwanamflame Mohammed bin Salman anashtumiwa kwa kuamuru mauaji ya Jamal Khashoggi.Picha: picture alliance/abaca/Balkis Press

Mawakala 15 wa Saudi walikwenda mjini Istanbul katika ndege ya serikali, gazeti la Post lilidai. Shalaan alisema siku ya Alhamisi, kwamba  mwanamfalme Salman, anaechukuliwa kama mtawala halisi wa Saudi arabia, hakujua chochote kuhusu operesheni ya mauaji ya Khashoggi.

Shirika la habari la Associated Press - likiripoti juu ya ziara ya California ya Trump, - liliripoti pia kwamba mashirika ya upelelezi ya Marekani "yalihitimisha kuwa  mrithi wa kiti cha ufalme aliamrisha mauaji hayo." Shirika la AP lilimnukuu afisa ambaye haruhusiwi kuzungumzia suala hilo hadharani."

Seneta wa chama cha Republican na mwenyekiti wa kamati ya mambo ya mambo ya nje ya baraza la Seneti Bob Corker, kupitia ujumbe wa Twitter siku ya Jumamosi, alisema: "Kila kitu kinaonesha kuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, MBS kama anavyoitwa kwa kifupi, ndiye aliamrisha mauaji ya Khashoggi.

Khashoggi, mchangiaji wa gazeti la Washington Post mwenye makao yake nchini Marekani na mkosoaji wa serikali ya Saudi Arabia, aliuawa wakati alipoutembelea ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul, Uturuki Oktoba 2. Mwili wake ulikatwa vipande na kisha kuondolewa.

Adhabu ya kifo haiwezi kutetewa, yasema EU

Mogherini, ambaye tangazo lake liliungwa mkono na mawaziri 28 wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya, akiwemo wa Ujerumani Heiko Maas, pia alilaani wito wa Shalaan wa Alhamisi kwamba washukiwa watano wa mauaji hayo wahukumiwe adhabu ya kifo.

"Ni msimamo wa muda mrefu wa Umoja wa Ulaya kupinga adhabu ya kifo katika kesi zote na katika mazingira yote," Mogherini alitangaza, na kuongeza kuwa "mchakato stahiki wa kimahakama" ulikuwa muhimu, pia ajili ya familia ya Khashoggi.

Türkei, Istanbul: Die Menschen besuchen ein symbolisches Begräbnisgebet für den saudischen Journalisten Jamal Khashoggi im Innenhof der Fatih-Moschee
Watu wakishiriki swala ya ghaibi kwa ajili ya Jamal Khashoggi, ambaye mwili wake haujapatikana, Novemba 16, 2018, mjini Istanbul.Picha: Reuters/M. Sezer

Kutafuta 'ukweli wote muhimu'

Wakati Trump akielekea California, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Heather Nauert alisema Washington "ingeendelea kutafuta ukweli wote muhimu." "Ripoti za karibuni zinazoonesha kuwa serikali ya Marekani imefanya hitimisho la mwisho siyo za kweli," alisema Nauert, na kuongeza kuwa maswali kadhaa bado yanahitaji majibu.

Licha ya hatua ya karibuni ya wizara ya fedha ya Marekani kuwawekea vikwazo watuhumiwa 17 maafisa wa serikali ya Saudi Arabia, Trump amekataa miito ya kuzuwia mauzo ya silaha kwa falme hiyo huku akielezea ushughulikiaji wake wa kisa cha mauaji ya Khashoggi kama "mmoja ya ufichaji mbaya zaidi katika historia."

Tusi kwa uhuru wa habari, asema Pence

Akihudhuria mkutano wa kanda ya pasifiki nchini Papua New Guinea siku ya Jumamosi, makamu wa rais wa Marekani Mike Pence alisema Jumatano kuwa Washington "itafuatilia ukweli" huku ikijaribu kulinda "ushirikiano wake imara na kihistoria" na Saudi Arabia.

Pence pia alielezea kile alichokiita mauaji hayo kuwa "tusi kwa tasnia huru ya habari." Maelezo rasmi ya maafisa wa Saudi Arabia kuhusu mauaji hayo ya Oktoba 2 yamekuwa yakibadilika mara kwa mara: awali walikanusha kufahamu chochote kuhusu uwepo wa Khashoggi na baadae wakasema aliuawa baada ya malumbano na maafisa wa Saudi kusababisha mapigano.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/DW

Mhariri: Lillian Mtono