EU yaipatia Italia fedha kumarisha ulinzi baharini
20 Machi 2017Tangazo hilo la Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya limetolewa leo katika mkutano wa kilele kuhusu wahamiaji unaofanyika mjini Roma, Italia kati ya mawaziri wa mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya na Afrika Kaskazini. Kwa mujibu wa umoja huo, Euro milioni 75 kati ya hizo, zitakuwa maalum kwa ajili ya fedha za dharura.
Serikali ya Italia tayari imeshapokea zaidi ya Euro milioni 592 ambazo ni fedha za Umoja wa Ulaya kwa ajili ya kusaidia katika kuwapatia hifadhi wakimbizi na kuwasaidia kuweza kutengamana vyema katika jamii nchini humo. Mkutano huo pia una lengo la kusaidia kutekeleza mkataba mpya na Libya ili iweze kufanya doria nzuri katika pwani yake na kuwazuia wafanyabiashara kutumia meli za mizigo kusafirisha watu kimagendo.
Ama kwa upande mwingine, Umoja wa Ulaya umepongeza kuhusu makubaliano ya wahamiaji kati yake na Uturuki, ikiwa ni mwaka mmoja baada ya makubaliano hayo kuanza kutumika rasmi. Msemaji wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Margaritas Schinas, amesema leo kuwa makubaliano hayo yamesaidia kuuvunja mtandao wa watu wanaofanya biashara ya kuuza watu kimagendo ambao wamekuwa wakiyaweka hatarini maisha ya watu.
Hata hivyo, shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International, limesema kuwa makubaliano hayo ni ya kufedhehesha ambayo yamechangia kuteseka kwa maelfu ya wakimbizi na wahamiaji. Nalo Shirika la Kimataifa la Uokozi, IRC, limesema makubaliano hayo yanakiuka haki za wakimbizi, na kuwasababishia kupata mateso.
Schinas hata hivyo, amepuuzia ukosoaji huo, akisema licha ya kuwepo na malalamiko mengi, hakuna hata mtu mmoja aliyekuja na njia mbadala zinazofaa ambazo zingeweza kuyaokoa maisha ya watu wengi.
Asilimia 90 ya wahamiaji waliingia Italia 2016
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Italia, Marco Minniti, amesema asilimia 90 ya wahamiaji walifanikiwa kuingia Italia wakitokea Libya kwa mwaka 2016, lakini hakuna hata mmoja ambaye alikuwa na uraia wa Libya.
''Lengo kuu ni kukabiliana kwa pamoja na changamoto ya mmiminiko wa wahamiaji, madhumuni ya mkutano huu ni kudhibiti mmiminiko huu, ikiwa na pamoja kuchukua hatua katika fukwe za Bahari ya Mediterania. Pia inamaanisha kuwepo kwa sera za ushirikiano na maendeleo, sera za ustawi na sera za udhibiti wa mipaka,'' alisema Minniti.
Waziri Mkuu wa Italia, Paolo Gentiloni, pamoja na mwenzake wa Libya, Fayez al-Serraj, ambaye anaongoza serikali ya mjini Tripoli inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, pamoja na Kamishna wa Uhamiaji wa Umoja wa Ulaya, Dimitris Avramopoulos wanatarajiwa kuhutubia katika mkutano huo wa kilele utakaowakutanisha mawaziri kutoka Algeria, Libya, Tunisia, Austria, Ufaransa, Ujerumani, Malta, Slovenia na Uswisi.
Mkutano huo unafanyika wakati ambapo walinzi wa pwani wa Italia wamewaokoa zaidi ya wahamiaji 3,000 katika pwani ya Libya kutoka kwenye boti zisizo salama kwa matumizi ya baharini. Wahamiaji hao wameokolewa mwishoni mwa juma lililopita katika operesheni 24 tofauti zilizofanyika kwenye pwani ya Libya.
Shirika la Kimataifa la Wahamiaji, IOM, limeripoti kuwa wahamiaji na wakimbizi 15, 852 wameingia Italia kupitia Bahari ya Mediterania hadi Machi 15 mwaka huu, huku watu 481 wakiripotiwa kufa wakati wakijaribu kuingia Italia.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, AP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman