1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU na Mali wakubaliana kudhibiti uhamiaji

12 Desemba 2016

Umoja wa Ulaya na Serikali ya Mali wametiliana saini makubaliano yatakayowezesha kurejeshwa nyumbani kwa wahamiaji ambao wamefika katika mwambao wa Ulaya na wale ambao maombi yao ya kuomba hifadhi yamekataliwa.

https://p.dw.com/p/2U9Jz
UNICEF Mazedonien Flüchtlinge
Picha: UNICEF/UN012725/Georgiev

Makubaliano hayo yametiwa saini na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uholanzi kwa niaba ya Umoja wa Ulaya ni ya mara ya kwanza, ikiwa ni njia ya kuzisaidia nchi za kiafrika kwa kuwarudisha katika nchi zao wale ambao maombi yao ya hifadhi hayakukubaliwa.

Katika taarifa yake waziri huyo amesema mkataba huo unalenga kupambana na vyanzo vya uhamiaji haramu na pia kuwasaidia raia wa Mali kurejea nchini mwao. Makubaliano hayo yanafikiwa ikiwa ni baada ya mkutano wa kilele uliofanyika Malta, Valleta Novemba mwaka jana, ambako viongozi wa Umoja wa Ulaya walikubaliana na wenzao wa Afrika kutenga kiasi cha mpaka euro bilion 1.8 kusaidia kukabiliana na vyanzo vya uhamiaji.

Ikiwa ni sehemu ya makubaliano hayo nchi za kiafrika zilipewa jukumu la kuhakikisha kuwa wanadhibiti mipaka yao na kuwarudisha makwao wale ambao watafanikiwa kuingia Ulaya na kuonekana kuwa hawana haki ya kubaki.

Mittelmeer Schiffsunglück Flüchtlingsboot vor der libyschen Küste gesunken
Wahamiaji kutoka mataifa mbalimbali wakiwa nchini ItaliaPicha: Getty Images/T.M. Puglia

Mkataba huo wa Umoja wa Ulaya na Mali unajenga misingi ya mipango ya kuwasaidia vijana kupata ajira na pia kuimarisha mifumo ya vikosi vya usalama katika nchi. Mali pamoja na nchi za jirani wanatarajiwa kuanzisha vita dhidi ya wasafirishaji wa binadamu wakati huo huo wakiimarisha ulinzi katika mipaka yao. Jumla ya miradi 9 yenye bajeti ya euro milion 145.1 ilipitishwa.

 Nigeria, Gambia na Mali zaongoza

Watumishi wa umma kutoka nchini Mali wataruhusiwa kusafiri katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya ili kusaidia kuwatambua wahamiaji lengo likiwa ni kuongeza kasi yakurudishwa makwao.

Takwimu zinaonyesha kuwa Idadi ya wahamiaji kutoka nchi za Afrika ikiwemo Mali, Nigeria na Gambia imeongezeka, watu  ambao huhatarisha maisha yao kwa kusafiri katika bahari wakiwa na lengo la kufika Ulaya.

Makubaliano hayo yamewasilishwa leo mjini Brussels yanaelezwa na waziri wa mambo ya nje wa Uholanzi Bert Koenders ambaye nchi yake itachukua urais baada ya mwaka mpya kuwa ni ya muhimu.

"Vijana kutoka Mali wana vitu vingi vya kufanya kwa ajili ya nchi yao, tunatakiwa kusaidia katika kuwazuia raia wa Mali kusafiri kwenda Afrika ya Kaskazini au Ulaya kwa hofu ya kupoteza maisha  au kuangukia katika mikono ya watu ambao wanafanya biashara haramu ya usafirishaji binadamu." alisema Waziri huyo.

Mwandishi: Celina Mwakabwale/AFP

Mhariri:Yusuf Saumu