1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya kuanzisha upya vikwazo Urusi

25 Januari 2021

Umoja wa Ulaya hii leo unazingatia kuanzisha upya vikwazo dhidi ya Urusi kufuatia kamata kamata ya watu zaidi ya elfu 3 siku ya Jumamosi wakishinikiza kuachiliwa huru kwa mkosoaji wa serikali Alexei Navalny.

https://p.dw.com/p/3oMtI
Russland | Landesweite Protestaktion Nawalny Verhaftung
Picha: Maxim Shemetov/REUTERS

Akizungumza mjini Brussels kabla ya kuongoza kikao cha Umoja Ulaya, Mkuu wa Sera za Kigeni Joseph Borrel amesema wimbi la kukamatwa na kuzuiliwa kwa wakososaji wa serikali akiwemo Navalny ni jambo ambalo linawatia wasiwasi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas ameikosoa hatua ya kamata kamata hio na kuongeza kuwa katiba ya Urusi inaruhusu kila mtu kuwa na haki ya kutoa maoni yake na pia kufanya maandamano. Maas amesema kuwa kanuni za sheria lazima zifuatwe na kwa ushirikiano na mawaziri wengine wamependekeza kuachiliwa kwa waandamanaji mara moja.

Hatua ya kupewa sumu lazima iangaziwe

Hapo jana Jumapili, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian alielezea wasiwasi juu ya kile alichokiita "udhalimu wa kimabavu wa Urusi ". Le Drian ameongeza kuwa hatua ya kupewa sumu kwa Navalny lazima iangaziwe.

 Joseph Borrell
Mkuu wa Sera za Kigeni Umoja Ulaya, Joseph BorrellPicha: Imago Images/Seeliger

Waziri wa Mambo ya nje wa Lithuania, Gabrielius Landsbergis kupitia njia ya video amesema Umoja wa Ulaya unahitaji kutuma ujumbe wa wazi na kufanya uamuzi wa kuthibitisha kuwa haikubaliki na kuunga mkono mwito wa kuwekewa vikwazo zaidi kwa Urusi.

Umoja Ulaya tayari umewekea vikwazo vya kiuchumi kwa nishati ya Urusi, sekta za kifedha na silaha juu ya nyongeza yake ya 2014 kutokana na nchi hiyo kuinyakua Rasi ya Crimea kutoka Ukraine na pia imeweka vikwazo kwa maafisa wa Urusi wa karibu na Rais Vladimir Putin kutokana na kupewa sumu Navalny mnamo mwezi Agosti.

Ukanda wa Baltiki unaunga mkono Umoja Ulaya

Russland Moskau | Proteste wegen Nawalny-Verhaftung
Polisi wakimkata mmoja wa waandamanaji wanaopinga kukamatwa kwa Alexei NavalnyPicha: Pavel Golovkin/AP Photo/picture alliance

"Tumekuwa tukifuatilia kwa wasiwasi mkubwa yaliyotokea nchini Urusi, kukamatwa kwa waandamanaji wa amani na pia kukamatwa kwa Bwana Navalny. Wale waliokamatwa wanapaswa kuachiliwa mara moja, ni muhimu sana kwamba mawaziri wa mambo ya nje leo wajadili, pia kupewa sumu Navalny na nini kifanyike pamoja na kuunga mkono uchunguzi sahihi wa kisheria wa kesi hii." Waziri wa Mambo ya nje wa Finland, Pekka Haavisto amesema.

Nchi za ukanda wa Baltiki za Latvia na Estonia zinaunga mkono Umoja Ulaya kuweka vikwazo zaidi kwa baadhi ya watu wa Urusi, huku waziri wa mambo ya nje wa Italia akisema Roma iko tayari kuunga mkono marufuku zaidi ya kusafiri na kufungia mali. Romania imeunga mkono hadharani vikwazo kwa Urusi.

 

Vyanzo/Reuters, AP,