EU kupendekeza mageuzi ya mfumo wa uhamiaji, wakimbizi
23 Septemba 2020Mfumo wa uhamiaji wa Umoja wa Ulaya umekumbwa na shinikizo zaidi katika miaka ya karibuni, huku changamoto zikijitokeza kwenye mipaka ya nje ya kanda hiyo.
Chini ya sheria za sasa za Umoja wa Ulaya, nchi ambako watu wanafikia kwa mara ya kwanza ndiyo inapaswa kushughulikia maombi yao ya hifadhi, hii ikimaanisha kwamba mataifa wanachama yalio na mipaka ya nje ya Umoja wa Ulaya yanabeba mzigo usio sawa na mengine.
Wakati baadhi ya mataifa yanapigania mfumo ambao utagawa moja kwa moja watafuta hifadhi, mengine kama Hungary, Jamhuri ya Czech na Austria - yanaupinga vikali mfumo huo.
Soma pia:Ugiriki: Ulaya ionyeshe mshikamano wa vitendo
Wanaharakati wa haki wana wasiwasi kwamba hatua mpya zinaweza kusababisha kukazwa zaidi kwa sheria za hifadhi. Wakati ambapo mapendekezo hayo yakitarajiwa kusababisha msuguano kati ya mataifa ya Umoja wa Ulaya, haijabainika wazi iwapo yataidhinishwa na wakuu wa mataifa na Bunge la Ulaya.
Mfumo wa kugawanya wakimbizi umeshindwa
Kansela wa Austria, Sebastian Kurz alionya siku ya Jumanne dhidi ya jaribio lolote la kuyalazimisha mataifa ya Umoja wa Ulaya kuchukuwa watafuta hifadhi, na kuelezea katika mahojiano na shirika la habari la Ufaransa AFP, namna juhudi za huko nyuma za halmashauri kuu kuanzisha mfumo wa viwango vya lazima kwa ajili ya wakimbizi kwa wanachama wote zilivyokataliwa na mataifa mengi ya Ulaya Mashariki na Kati.
"Tunaamini kwamba mjadala kuhusu ugawanyaji wa watafuta hifadhi ndani ya Umoja wa Ulaya umeshindikana na kwamba hili linasababisha tu mabishano kuliko ushirikiano. Lakini kilicho muhimu ni kulinda mipaka yetu ya nje, kupambana dhidi ya wasafirishaji haramu wa watu na kusaidia papo kwa hapo," alisema Kurz.
Soma pia: Wimbi jipya la wakimbizi kwenye mpaka wa Uturuki na Ugiriki
Kuelekea kuwasilisha mapendezo hayo, shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR na shirika la Kimataifa la Uhamiaji yameusihi Umoja wa Ulaya siku ya Jumanne, kuheshimu haki ya kutafuta hifadhi, yakidai mkakati wa sasa wa kanda hiyo haufanyi kazi, hauwezi kutetewa na mara nyingi unabeba madhara makubwa ya kibindamu.
Kwa mujibu wa masijala ya nyaraka ya halmashauri kuu, chombo hicho cha utendaji cha Umoja wa Ulaya kitapendekeza kanuni mpya tano na zilizorekebishwa, baadhi yake zikishughulikia uchunguzi wa watafuta hifadhi na hali za mizozo. Uchunguzi unaweza kuhusisha ukaguzi kwa wanaowasili ambao hawajisikii vizuri, au kwa watu ambao wameainisha kama kitisho cha usalama.
Hofu ya mashirika ya haki za binadamu
Unaweza pia kumaanisha wahamiaji kufanyiwa tathmini ya awali ili kuondoa wale ambao hawana msingi wa kuomba hifadhi, kama ilivyopendekeza Ujerumani. Mashirika ya haki za binadamu yana wasiwasi kwamba hili linaweza kuzuwia kutathminiwa kwa usahihi, maombi ya baadhi ya makundi ya waomba hifadhi,na kwamba hata watu wanaweza kuzuwiwa nje ya mipaka ya Umoja wa Ulaya.
Soma pia: Kambi ya wahamiaji Ugiriki yateketea kwa moto
Kufuatia moto uliosababisha janga mapema mwezi huu kwenye kambi ya wahamiaji ya Moria kwenye kisiwa cha Ugiriki cha Lesbos, ambayo ilikuwa inawahifadhi watu wapatao 12,000, halmashauri kuu pia inatrajiwa kupendekeza mfumo wa mshikamano kwa ajili ya nyakati za mizozo.
Sheria hiyo, kwa mujibu wa mashirika ya haki za binadamu na ripoti za vyombo vya habari, itazingatia mkakati wa hatua tatu, ambazo ni ngazi ya kawaida ambako mshikamano ni wa hiari, pili, kuanza kwa mzozo na tatu, ngazi ya mzozo mkali.
Chanzo:Mashirika