1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU kukomesha utoaji gesi ukaa mwaka 2050

Admin.WagnerD13 Desemba 2019

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kanda hiyo kukomesha utoaji wa gesi ya ukaa ifikapo mwaka 2050, katika makubaliano ambayo hata hivyo yalitiwa kiwingu na uamuzi wa Poland wa kukataa kutekeleza lengo hilo.

https://p.dw.com/p/3Ujm5
Brüssel EU Gipfel | Pressekonferenz Ursula von der Leyen
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen (kushoto) na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Charles MichelPicha: Getty Images/AFP/K. Tribouillard

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Charles Michel amesema makubaliano yalaliyofikiwa jana wakati wa mkutano wa wakuu wa nchi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels, ni uthibitisho madhubuti unaoiweka Ulaya katika mstari wa mbele kwenye juhudi za ulimwengu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Michel amesema makubaliano yaliyofikiwa ni muhimu kwa Ulaya kuonesha nia yake linapokuja suala la kupambana na uchafuzi wa mazingira.

Kwa upande wake rais mpya wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen ameyasifu makubaliano yaliyofikiwa baada ya majadiliano makali yaliyojumuisha wasiwasi kuhusu uwezekano wa kufikiwa malengo yaliyopendekezwa.

"Tumenuwia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuyageuza kuwa fursa kwa Umoja wa Ulaya, tukifahamu kuwa sasa Umoja wa Ulaya ndiyo kinara kwenye suala hilo na tunataka kuendelea kuwa kinara, tunataka kuwa mfano wa kuigwa" amesema Von der Layen mjini Brussels.

Poland yatia doa makubaliano ya EU

Brüssel EU Gipfel | Familienfoto
Viongozi wa Umoja wa Ulaya katika picha ya pamoja wakati wa mkutano mjini BrusselsPicha: Getty Images/AFP/A. Jocard

Hata hivyo makubaliano hayo yalitiwa doa na uamuzi wa Poland nchi mwananchama wa Umoja wa Ulaya inayotegemea kwa sehemu kubwa nishati ya makaa ya mawe, kusema haiko tayari kusitisha haraka matumizi ya nishati chafuzi ifikapo mwaka 2050.

Kulingana na wanadiplomasia mjini Brussels, Poland inahitaji pengine hadi mwaka 2070 ili kuhamia kikamilifu katika kutumia nishati rafiki kwa mazingira, huku mataifa mengine kama jamhuri ya Czech yalipigia upatu kuendelea kutumiwa nishati ya nyuklia.

Ili kujizuia na aibu ya kuanguka kwa makubaliano yaliyofikiwa kutokana na upinzani wa Poland, viongozi wa Umoja wa Ulaya wameidhinisha kipengele mahsusi kitakachowezesha hoja za poland kujadiliwa kwa upana wakati wa mkutano mwingine wa kilele mwezi Juni mwaka 2020.

Makubaliano ya mjini Brussels ni matokeo ya mpango wa kufikia Ulaya isiyochafua mazingira ambao ulizinduliwa Jumatano iliyopita.

Mpango unajumuisha kukusanya Euro bilioni 100 kuzisaidia nchi wanachama kuhamia katika matumzii ya nishati jadidifu.

Upinzani ni mkali Ulaya Mashariki 

Brüssel EU Gipfel Sitzungssaal
Picha: picture-alliance/AP Photo/Y. Herman

Hata hivyo lakini wakosoaji wake wa Ulaya Mashariki wanasema hilo halitoshi.

Waziri mkuu wa Jamhuri ya Czech amesema nchi yake pekee itahitaji kati ya Euro bilioni 30 hadi 40 ili kufikia uwezo wa kuzalisha nishati isiyochafua mazingira.

Kadhalika Rais wa Lithuania, Gitanas Nauseda amekadiria kwa nchi yake itahitaji kutumia  karibu theluthi mbili ya pato jumla la ndani kufikia lengo la kuachana na nishati chafuzi.

Katika hatua nyingine viongozi wa Umoja wa Ulaya wametangaza kurefusha kwa muda wa miezi sita zaidi vikwazo dhidi ya Urusi kuhusiana na dhima yake katika mzozo wa mashariki ya Ukraine.

Vikwazo dhidi ya Urusi viliwekwa mwaka 2014 baada ya nchi hiyo kuichukua kwa nguvu rasi ya Crimea na kuwaunga mkono wale wanaotaka kujitenga masharikiy a Ukraine.