1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU kukaza masharti ya kuuza chanjo za COVID-19

John Juma Mhariri: Daniel Gakuba
24 Machi 2021

Halmashauri kuu ya Ulaya inatarajiwa kukaza masharti na kanuni za kuuza chanjo ya COVID-19 nje kuanzia leo ili kuzuia kile inachotizama kama ukosefu wa usawa katika uuzaji wa chanjo.

https://p.dw.com/p/3r2Zf
Anti-Rassismus-Gipfel der EU | Ursula von der Leyen
Picha: European Union

Kulingana na rasimu ambayo shirika la habari la AFP limeipata, Umoja wa Ulaya umeghadhabishwa na hatua ya Uingereza kudai kwamba tayari imeshanunua dozi za chanjo ya AstraZeneca ambazo zimetengenezwa katika kiwanda cha kampuni hiyo kilichoko Uholanzi, ilhali kiwanda cha kampuni hiyo kilichoko Uingereza kimeshindwa kutimiza ahadi yake ya kuwasilisha dozi kamili ambazo Umoja wa Ulaya uliagiza.

Huku mazungumzo yakiendelea nyuma ya pazia kati ya Umoja wa Ulaya na serikali ya Uingereza, kuepusha kitisho cha kupiga marufuku kabisa uuzaji wa chanjo zilizotengenezwa ndani ya Umoja wa Ulaya nje ya umoja huo, tayari halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya imeamua kukaza sheria za uuzaji nje wa chanjo.

Soma pia:

Uhaba wa chanjo wasababisha mvutano

Sheria hiyo inayolenga kufuatilia chanjo zinazotolewa ndani ya Umoja wa Ulaya kuuzwa nje na ikibidi kuzuia uuzaji huo, imeshawahi kutumiwa mara moja wakati dozi za AstraZeneca zilizokusudiwa kutolewa Italia na kuuziwa Australia zilizuiwa.

Umoja wa Ulaya wailaumu kampuni ya AstraZeneca kutowasilisha kiwango cha chanjo kilichokubaliwa.
Umoja wa Ulaya wailaumu kampuni ya AstraZeneca kutowasilisha kiwango cha chanjo kilichokubaliwa. Picha: Dado Ruvic/REUTERS

Hata hivyo rasimu hiyo ya sheria iliyosahihishwa, pia inalalamikia nchi zinazozuia chanjo kusafirishwa kuingia Umoja wa Ulaya, kutokana na sheria au kutokana na mikataba waliyonayo na kampuni za kutengeneza chanjo.

Kampuni ya AstraZeneca imesema mkataba wake na serikali ya Uingereza unaipa Uingereza kipaumbele kupokea chanjo zake zaidi. 

Ursula von Der Leyen atoa onyo kwa AstraZeneca

Akiungwa mkono na viongozi wengine wa Umoja wa Ulaya akiwemo kansela wa Ujerumani Angela Merkel, rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von Der Leyen, ametaka kuwe na kile alichokitaja kuwa utimizaji wa makubaliano katika uuzaji wa chanjo huku akionya kwamba huenda kampuni ya AstraZeneca ikapigwa marufuku kuuza chanjo nje ya Umoja wa Ulaya.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Michael Kappeler/AP Photo/picture alliance

Rasimu hiyo imeonya pia kwamba baadhi ya nchi ambazo kwa sasa hazina sheria za kudhibiti uuzaji wa bidhaa nje ya mipaka yao zina kiwango cha juu cha utoaji chanjo hata kushinda Umoja wa Ulaya, ama hazijaathiriwa zaidi na janga la virusi vya corona.

Kufuatia hali hiyo rasimu imesema usafirishaji wa chanjo kuelekea nchi hizo huweza kuathiri upatikanaji wa chanjo ndani ya Umoja wa Ulaya.

Boris Johnson aingiwa wasiwasi na fikra za EU

Mnamo Jumanne, waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson alielezea wasiwasi wake kuhusu hatua hiyo ya Umoja wa Ulaya, lakini alielezea matumaini kwamba mazungungumzo yao yataleta suluhisho.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris JohnsonPicha: Tolga Akmen/REUTERS

Hayo yanajiri mnamo wakati mkuu wa vyumba vya kuwahudumia wagonjwa mahututi katika hospitali ya Paris nchini Ufaransa Jean-Francois [Janfranswaa] Timsit akisema mwezi ujao utakuwa kile alichokitaja kuwa ‘maafa makubwa' kufuatia kulemewa kwa mfumo wa afya kwa sababu ya wimbi la tatu la maambukizi ya COVID-19.