EU ipanue wigo wake kuelekea Moldova na Ukraine kujiunga
23 Juni 2022Kabla ya kuanza kwa mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels Kansela Scholz amesema upo ulazima wa kuweka mazingira muhimu kwa Ukraine kusonga mbele na wakati huohuo Ulaya iwe na ufahamu wa utayari wa kupanua wigo wake. Amesema muungano huo mkubwa ufanye kazi zake kwa ufanisi, maamuzi mengi yanapaswa kufanywa na wengi, na kuachana na ubinafsi.
"Kwa hiyo hoja muhimu zaidi ni kwamba sisi sote tunafanya kazi pamoja na kwamba mataifa ya Balkani ya Magharibi yatapata fursa nzuri ya kuwa wanachama halisi wa Umoja wa Ulaya. Wamefanya kazi kwa bidii. Kwa hivyo wajibu wetu wa pamoja ni kufanya hatua hiyo iwe na matokeo. Ahsante," alisema Scholz.
Mataifa ya Brics yashirikiane na Urusi
Katika hatua ya mwanzo ni kwamba mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya unatarajiwa kutoa uamuzi wa kihistoria ambao utatoa nafasi kwa Ukraine na Moldova kusonga mbele katika hatua ya kuwania kuingia katika Umoja wa Ulaya.
Katika hatua nyingine Rais wa Urusi Vladimir Putin Alhamis aliwatolea wito viongozi wa mataifa ya Brazil, India, China na Afrika Kusini wa kushirikiana nae katika kukabiliana na kile alichokiita "vitendo vya ubinafsi" vya mataifa ya Magharibi, wakati huu ambao serikali yake inakabiliana na vikwazo vya mataifa hayo ya Magharibi kufuatia kuingia kwake kijeshi nchini Ukraine.
Katika ujumbe wake kwa njia ya vide uliorushwa kupitia televisheni kwa mataifa yenye kuunda umoja huo unaofahamika kwa ufupi BRICS, Putin amesema ni kwa msingi wa ushirikiano wa uaminifu na wa kunufaisha pande zote wanaweza kupata ufumbuzi wa mzozo huu wa sasa unaondelea katika uchumi wa dunia, unaotokana na hatua mbaya na za ubinafsi za baadhi ya mataifa.
Jeshi la Urusi laongeza mashambulizi mashariki
Katika hotuba yake hiyo Putin aliongeza kwa kusema kuwa mataifa ya BRICS yanaweza kutegemea uungwaji mkono wa mataifa mengi ya Asia, Afrika na Amerika Kusini yanayojitahidi kufuata sera huru. Marekani na Umoja wa Ulaya zimeiwekea urusi idadi ya vikwazo ambavyo havijawahi kushuhudiwa baada ya Putin kutuma wanajeshi wake katika eneo linalounga mkono Magharibi mwa Ukraine Februari 24.
Ndani nchini Ukraine, jeshi la Urusi limeongeza mashambulizi yake katika upande wa mashariki wa taifa hilo, likividhibiti vijiji viwili huku likiwa mbioni pia kuidhibiti barabara kuu, likionekana kuwa na lengo la kuzuia usambazaji wa bidhaa na kuwazingira wanajeshi wa Ukraine walio katika uwanja wa mapambano.
Wizara ya Ulinzi ya Uingereza imesema vikosi vya Ukraine vimejiondoaa kaatikaa baadhi ya maaeneo ya karibu na mji wa Lyschansk kujiepusha na mzingiro na majeshi ya Urusi.