1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia: Zenawi bado imara

Admin.WagnerD20 Julai 2012

Kufuatia kuenea kwa uvumi kwamba Waziri wa Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi, amekuwa mgonjwa kwa muda mrefu sasa, serikali ya nchi hiyo imetoa taarifa ikisema kwamba Zenawi amechukua mapumziko tu ya kikazi na atarejea.

https://p.dw.com/p/15bvu
Waziri Mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi
Meles Zeinawi Äthiopien PremierministerPicha: AP

Kiongozi huyo amechukua mapumziko hayo kutokana na kuchoka sana, na atarejea ofisini baada ya siku chache, na kuongeza kuwa hali ya kiongozi huyo mwenye nguvu katika Pembe ya Afrika si mbaya kama inavyoripotiwa.

Uvumi ulienea kuwa kiongozi huyo yu taabani, na ulienea kwa kasi baada kushindwa kuhudhuria mkutano wa viongozi wakuu wa Afrika uliofanyika kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Addis Ababa, wiki iliyopita.

Kukosekana kwa taarifa kuhusu hali ya afya ya kiongozi huyo na hata mahali alipo kumezusha pia maswali miongoni mwa jamii juu ya nani atamrithi na kuongoza taifa hilo la pembe ya Afrika lililogubikwa na mizozo.

Waziri wa Mawasiliano nchini humo, Berekt Simon, amesema kuwa kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 57, kwa sasa anafuata ushauri wa daktari uliomtaka apumzike kutokana na uchovu uliosababishwa na kufanya kazi kwa miaka mingi bila kupumzika.

Uvumi juu ya pahala alipo Zenawi

Waziri huyo alikataa kutoa taarifa zaidi juu ya aina ya matibabu anayopatiwa kiongozi huyo na kwa muda gani hasa amekuwa kwenye tiba hiyo. Duru za diplomasia nchini humo zinasema kuwa kiongozi huyo anatibiwa mjini Brussels, lakini ugonjwa wake bado ni siri. Vyanzo vingine vianaripoti kuwa matibabu hayo anayapata hapa Ujerumani, huku baadhi ya taarifa zikithubutu kusema huenda ameshakufa.

Wiki kadhaa zilizopita mitandao ya upande wa upinzani nchini humo imekuwa ikichapisha taarifa kuwa Zenawi yuko kwenye matibabu kutokana na afya yake kuwa mbaya sana. Uthibitisho wa kwanza juu ya kuugua kwa kingozi huyo ulitolewa jumamosi iliyopita na Rais wa Senegal. Rais huyo aliyasema hayo kwa viongozi waliohudhuria mkutano wa Umoja wa Afrika. Hii ni mara ya kwanza kwa Zenawi kushindwa kuhudhuria mkutano huo tangu achukue madaraka mwaka 1991.

Mkutano wa viongozi wakuu wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa
Mkutano wa viongozi wakuu wa Umoja wa Afrika mjini Addis AbabaPicha: dapd

Siku ya Jumatatu bunge la Ethiopia lilipitisha bajeti ya mwaka ya serikali iliyoanza kutumika tarehe 8 mwezi huu bila ya kuwepo kiongozi huyo. Waziri Bereck amesisitiza kuwa Zenawi hajawahi kuugua mahututi hata mara moja, na kwamba bado anashikilia madaraka ya taifa hilo. Aliwaeleza waandishi wa habari kuwa atarejea ofisini siku chache zijazo, lakini hakusema ni lini hasa.

Mipango yaendelea kutekelezwa licha ya kutokuwepo Zenawi

Kwa sasa chama tawala nchini humo kinatekeleza mpango wake ambao umeshuhudia mawaziri wazito kwenye baraza la mawaziri wakistaafu na wengine kupelekwa nchi za nje kama mabalozi na wawakilishi mbalimbali. Berekt amesema mpango huo unatarajiwa kukamilika wakati Zenawi atakapoondoka madarakani mwaka 2015.

Meles Zenawi, aliyekuwa kiongozi wa vita vya msituni, amekuwa madarakani tangu mwaka 1991 baada ya kuondolewa kwa utawala wa kijeshi wa Mengistu Haile Mariam mwaka huohuo.

Amekuwa akisifiwa na baadhi ya mataifa ya magharibi kwa ukuaji wa uchumi nchini mwake pamoja na uungaji mkono wa jeshi lake katika mapambano dhidi ya makundi ya wanamgambo wenye misimamo mikali yenye mafungamano na mtandao wa al-Qaeda kwenye nchi jirani ya Somalia.

Wanamgambo wa Al-Shabab nchini Somalia
Wanamgambo wa Al-Shabab nchini SomaliaPicha: AP

Lakini pia analaumiwa kuwa anakwenda kinyume na matakwa ya wananchi kwa kuweka sheria kali na pia kuukandamiza upinzani na vyombo vya habari kwa kutumia kigezo cha usalama wa taifa.

Mwandishi: Stumai George/Reuters/APE

Mhariri: Miraji Othman