Ethiopia yampata rais wa kwanza mwanamke
25 Oktoba 2018Sahle-Work Zewde ambaye ni mwanadiplomasia wa muda mrefu, anachukuwa nafasi ya Mulatu Teshome ambaye amejiuzulu wadhifa wa urais ambao nchini Ethiopia ni wa heshima tu. Baada ya kuchaguliwa kwake, Sahle-Work amesema kuingia madarakani kwa waziri mkuu Abiy Ahmed ni hatua ya mfano mwema, ambayo anaamini itasaidia kuleta amani nchini Ethiopia ambako mnamo miezi ya hivi karibuni kumeshuhudiwa mizozo mingi yenye msingi wa kikabila.
Fitsum Arega ambaye ni kiongozi wa ofisi ya waziri mkuu Abiy Ahmed, amesema kupitia ukurasa wake wa twitter, kwamba kuchaguliwa kwa rais mwanamke katika nchi ya Ethiopia ambayo ni jamii ya mfumo dume, sio tu kutoa mfano wa kuigwa kwa mustakabali wa nchi, bali pia kunafanya ushirikishwaji wa wanawake katika maamuzi muhimu kuwa kitu cha kawaida.
Mfululizo wa maamuzi chanya kwa wanawake
Wiki iliyopita, waziri mkuu wa Ethiopia alilifanyia marekebisho baraza la mawaziri, na kuteuwa wanawake 10, akiwemo waziri wa ulinzi wa kwanza mwanamke wa nchi hiyo.
Kwa uteuzi huo, Ethiopia imekuwa nchi ya tatu barani Afrika kuwa na baraza lenye idadi sawa ya wanawake na wanaume, baada ya Rwanda na Ushelisheli.
Akizungumza bungeni leo baada ya kuchaguliwa, Sahle-Work amesema pale nchi inapokosa amani, akina mama hukata tamaa, na hivyo kutoa wito wa kila mtu kupigania amani kwa ajili ya akina mama wote.
Mtangulizi wa Sahle-Work katika wadhfa wa rais Mulatu Teshome Wirtu ambaye amehudumu kwa miaka 5, amejiuzulu ukisalia mwaka mmoja kabla ya kumaliza muhula wake, akisema anataka kuchangia katika mabadiliko yanayoendelea.
Baadhi ya wachambuzi wanasema kujiuzulu kwake kunaweza kuwa na malengo ya kuweka urari wa kikabila, kwa sababu anatoka jamii ya Oromo kama alivyo waziri mkuu Abiy Ahmed.
Mwanadiplomasia mahiri
Rais mpya, Bi Sahle-Work ni wa nne katika wadhifa huo tangu mseto wa vyama wa EPRDF ulipoingia madarakani mwaka 1988,kufuatia ushindi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Ni mwanaplomasia wa muda mrefu, akiwa ameiwakilisha nchi yake katika nchi za Ufaransa, Djibouti, Senegal na katika Jumuiya ya Ushirikiano ya nchi za Upembe wa Afrika, IGAD.
Kwa wakati huu Sahle-Work Zewde ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, na mjumbe maalumu wa Katibu mkuu wa umoja huo katika makao makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, na ana umri wa miaka 68.
Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe,rtre
Mhariri: Iddi Ssessanga