Ethiopia na Kenya zatawala New York Marathon
7 Novemba 2016Ghebreslassie mwenye umri wa miaka 20 alishinda mbio hizo kwa upande wa wanaume kwa kutumia muda wa saa mbili, dakika saba na sekunde 51, dakika moja zaidi mbele ya Mkenya Lucas Rotich.
Ushindi wa Ghebreslassie uliuwekea kikomo ushindi mara nne mfululizo wa wanaume wa Kenya katika mbio hizo. Nafasi ya tatu ilichukuliwa na Mmarekani Abdi Abdirahman mwenye umri wa miaka 39.
Kwa upande wa wanawake, Keitany aliibuka mwanamke wa kwanza katika miongo mitatu kushinda mbio za New York Marathon mara tatu mfululizo. Mkenya huyo mwenye umri wa miaka 34 alishinda na pengo la zaidi ya dakika tatu kwa kutumia muda wa saa mbili dakika 24 na sekunde 26. Mwenzake Sally Kipyego alimaliza wa pili na Mmarekani Molly Huddle akatwaa nafasi ya tatu.
Keitanny alijiunga na Muingereza Paula Radcliffe kuawa wanawake waliowahi kushinda mbio hizo mara tatu mfululizo. Radcliffe alishinda mataji ya 2004,2007 na 2008. Aliyeshinda mataji mengi zaidi ni Grete Waitz wa Norway aliyetwaa matano kuanzia mwaka wa 1982 hadi 86.
Haile Gebrselassie
Mwanariadha nguli aliyestaafu Haile Gebrselassie amechaguliwa kuwa rais wa Shirikisho la Riadha la Ethiopia. Nyota huyo wa michezo mwenye umri wa miaka 43, anayetambulika kuwa mmoja wa wanariadha bora zaidi wa masafa marefu wa muda wote, atahudumu kwa muhula wa miaka minne. Vyombo vya habari nchini humo viliripoti kuwa alishinda kura 9 kati ya 15 zilizopigwa ili kupata wadhifa huo.
Gebrselassie alikuwa mkosoaji mkubwa wa shirikisho la riadha la Ethiopia, akiwashutumu viongozi wake kwa "uzembe” katika maandilizi ya michezo ya Olimpiki ya Rio.
Ethiopia ilishinda medali nane tu katika michezo ya Rio, ikiwemo dhahabu moja pekee ya Almaz Ayana katika mbio za mita 10,000 kwa wanawake, na ikamaliza katika nafasi ya 44 kimataifa, nyuma kabisa ya Kenya, jirani yake na hasimu wa kihistoria.
Gebrselassie alitoa wito wa uongozi wa shirikisho hilo kujiuzulu akisema yuko tayari kutoa uzoefu wake na kusaidia Ethiopia kujiandaa kwa mashindano yajayo ya ubingwa wa dunia ya IAAF jijini London mwaka wa 2017 na michezo ya Olimpiki ya Tokyo 2020.
Mwandishi:_Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu