Ethiopia: Mkuu wa Jeshi apigwa risasi
23 Juni 2019Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amefahamisha kuwa mkuu wa majeshi Seare Mekonen alipigwa risasi baada ya kuzuka machafuko Jumamosi jioni katika taifa hilo la Pembe ya Afrika. Hata hivyo hali ya mkuu huyo wa jeshi haijulikani.
Kwa mujibu wa mwandishi wa shirika la habari la AFP, Rais Abiy alizungumza kupitia kwenye televisheni ya taifa akiwa amevaa mavazi rasmi ya kijeshi baada ya kutokea jaribio la mapinduzi katika jimbo la Amhara lakini maelezo zaidi hayakutolewa kuhusiana na lengo la mashambulio hayo katika jimbo la pili lenye watu wengi zaidi nchini Ethiopia linaloongozwa na Rais wa kikanda Ambachew Mekonen.
Ubalozi wa Marekani ulitoa tahadhari baada ya kusisikia milio ya bunduki katika mji mkuu wa Addis Ababa, na pia vurugu karibu na mji mkuu wa jimbo la Amhara, Bahir Dar.
Serikali ya Ethiopia imesema jaribio hilo la kuipindua serikali ya kikanda kaskazini mwa nchi hiyo lilishindikana. Ofisi ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed imelaani jaribio hilo la mapinduzi katika ujumbe wa Twitter uliochapishwa Jumamosi jioni.
Wakazi katika mji mkuu wa mkoa huo, Bahir Dar, wameripoti kusikia milio ya bunduki. Nchini Ethiopia mara nyingi mivutano ya kikabila imekuwa ndio chanzo cha mapigano katika nchi hiyo ambayo kwa muda mrefu imetawaliwa kwa mkono wa chuma.
Tangu Abiy alipochukua mamlaka mwezi wa Aprili 2018, ameleta mageuzi, ikiwa ni pamoja na kuwaachia wafungwa wa kisiasa, mageuzi ya kiuchumi, ameruhusu makundi ya watu mbali mbali kurudi nchini, na ameaahidi kupambana na vitendo vinavyokiuka haki za binadamu na amejaribu kuboresha uhuru wa vyombo vya habari.
Lakini Wasziri Mkuu Abiy Ahmed anakabiliana na kuongezeka kwa mivutano kati ya makundi ya kikabila katika nchi hiyo ambayo kwa kawaida ni juu ya ardhi na rasilimali, mivutano hiyo inasababisha vurugu mbaya katika nchi yenye watu zaidi ya milioni 100.
Vyanzo:/AFP/DPAE