Ethiopia kufanyia mageuzi mfumo wa uchaguzi
11 Oktoba 2016Waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn amesema serikali yake inataka kufanya mageuzi ya mfumo wa uchaguzi, ambao kwa muda mrefu umeutenga upinzani na kuchangia kutokea kwa maandamano mabaya ambayo yamedumu kwa miezi kadhaa. Haya yanajiri wakati Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akimaliza ziara yake nchini humo ambapo amesema waandamanaji waruhusiwe kuandamana.
Waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn amewaambia wanahabari kuwa “kufuatia mfumo uliopo sasa wa uchaguzi nchini humo, asilimia 51 ya kura inatosha kutwaa ushindi wa viti vyote". Na sasa serikali yake inataka kufanya marekebisho ili kuhakikisha mfumo huo unabadilishwa ili watu wote wakiwemo wapinzani wawakilishwe bungeni.
Chini ya mfumo uliopo sasa, muungano wa Hailemariam ambao ndio unatawala, ulishinda viti vyote 546 vya ubunge katika uchaguzi mkuu, uliofanywa mwaka jana. Hii hapa kauli ya Hailemariam kuhusu suala, la demokrasia na usalama nchini mwake."Ethiopia imejitolea kukuza demokrasia.Ethiopia imejitolea kuwa na demokrasia ya vyama vingi kulingana na katiba yetu. na Ethiopia imejitolea kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa. Lakini Ethiopia pia inapinga ghasia ya misimamo mikali au makundi yanayojihami kwa fujo".
Hailemariam aliyasema hayo baada ya kukutana na mgeni wake Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, akimaliza ziara yake ya siku tatu barani Afrika, ambapo amesema demokrasia iliyoimarika inahitaji kuwepo na upinzani pamoja na uhuru wa vyombo vya habari. Ameitaka Ethiopia kuwapa uhuru waandamanaji bila ya ukandamizaji wa aina yoyote. Kando na kuhimiza serikali kufanya mazungumzo na upinzani, Merkel pia ameahidi kuwa, nchi yake itatoa mafunzo kwa maafisa wa polisi wa Ethiopia kuhusu namna ya kukabiliana na waandamanaji.
Akiwa Ethiopia, Kansela Merkel amemwambia mwenyeji wake Waziri Mkuu Desalegn kuwa waandamanaji waruhusiwe kuandamana na kuwa hatua yoyote ya vyombo vya usalama iwe kulingana na sheria. Kadhalika amesema wanaharakati wa upinzani na watetezi wa haki za kibinadamu wanapaswa kuwa na uhuru wa kutekeleza majukumu yao. Lakini Waziri Mkuu Hailemariam amepinga madai kuwa maafisa wa polisi walitumia mbinu za fujo dhidi ya waandamanaji, na kuahidi kuwa serikali yake itachunguza visa hivyo.
Wiki iliyopita, zaidi ya watu 50 waliuawa kwenye mkanyagano baada ya polisi kujaribu kuwatawanya waandamanaji. Hali iliyosababisha kuongezeka kwa maandamano zaidi, na kulazimisha serikali kutangaza hali ya hatari nchini humo mwote.
Ethiopia imekumbwa na maandamano ya miezi kadhaa ambapo waandamanaji wanashinikiza kupatikana kwa uhuru wa kisiasa na haki ya kumiliki ardhi, huku wakilaumu serikali kwa kuendeleza utawala wa kimabavu.
Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, watu 400 wamekufa nchini Ethiopia kutokana na maandamano hayo dhidi ya serikali. Hayo yamesemwa na makundi ya kutetea haki za kibinadamu pamoja na wanaharakati wa upinzani.
Jumatatu wiki hii, rais wa Ethiopia alitangaza bungeni kuwa sheria za uchaguzi zitafanyiwa marekebisho ili kuruhusu vyama vingi vya kisiasa na kuwapa nafasi wapinzani. Hata hivyo, matumizi ya mtandao yangali yamezimwa nchini humo, baada ya maandamano kuzidi kwa muda wa wiki moja ambapo pia waandamanaji walifanya uharibifu katika biashara na afisi za ubalozi wa nchi zinazofikiriwa kushirikiana na serikali.
Marekani na mataifa mengine yameitaka serikali ya Ethiopia kujizuia katika kukabiliana na waandamanaji huku maafisa wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wakitaka uchunguzi huru ufanywe kuhusu matukio hayo katika eneo la Oromia.
Merkel amekamilisha ziara yake ya siku tatu katika nchi za Mali, Niger na Ethiopia yenye lengo la kuhimiza uimarishaji wa usalama ili kupunguza wimbi la wakimbizi. Ethiopia ni mojawapo ya nchi inayowahifadhi wakimbizi wengi duniani. Mamia ya maelfu ya wakimbizi hao wakitoka Somalia, Sudan Kusini na kwingineko. Sawa na Ujerumani ambayo.
Merkel pia inakumbwa na mzigo wa wakimbizi kwa sasa, ambapo takriban wakimbizi mioni moja waliingia Ujerumani tangu mwaka jana pekee.pia amefungua rasmi jingo jipya la Muungano wa Afrika ambalo pia litakuwa la baraza la amani na usalama. Jengo hilo lililopo Addis Ababa limejengwa kwa ufadhili wa yuro milioni 27 kutoka Ujerumani.
Mwandishi: John Juma/APE/RTRE
Mhariri: Mohammed Khelef