Ethiopia: Kiongozi wa upinzani awachiliwa huru
17 Januari 2018Mwenyekiti wa chama cha upinzani nchini Ethiopia cha Oromo Federalist Congress (OFC), Merera Gudina ameachiliwa huru Jumatano asubuhi baada ya kuwekwa kizuizini kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Kuachiliwa huru kwa Merera ndicho kitu kikubwa walichokuwa wakidai waandamanaji wa kundi kubwa la kikabila nchini humo la Oromos. Mnamo mwaka 2015, watu wa kabila la Oromo waliandamana dhidi ya pendekezo la kutaka kuupanua mji mkuu wa Addis Ababa. Wakihofia upanuzi huo utawapokonya ardhi yao .
Mamia waliuawa katika vurugu hizo, zilizosababisha kutangazwa hali ya dharura iliyodumu miezi kumi na kumalizika mwezi Agosti. Merera ni kiongozi wa kwanza wa kisiasa kuachiliwa huru tokea Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn, alipotangaza mapema mwezi huu kwamba wanasiasa wenye hatia watasamehewa.