Ethiopia: Chama cha PP cha Abiy Ahmed chashinda uchaguzi
11 Julai 2021Chama cha Prosperity (PP) cha Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kimeshinda viti vingi katika uchaguzi wa bunge la Ethiopia. Waziri Mkuu Abiy Ahmed na chama chake kipya cha PP walitangazwa kushinda kwa kishindo na tume ya uchaguzi katika hafla iliyofanyika kwenye mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.
Soma zaidi:Waasi wa Tigray wakubali kusitisha mapigano kwa masharti
Abiy amepongeza uchaguzi huo ambapo raia wa Ethiopia walipiga kura mnamo tarehe 21 Juni. Amesema huo ni uchaguzi wa kwanza huru na wa haki kufanyika baada ya miongo kadhaa ya utawala wa ukandamizaji.
Tume ya uchaguzi ya Ethiopia imetangaza kuwa chama cha Abbiy cha Prosperity (PP) kimeshinda viti 410 kati ya viti 436 vya bunge katika maeneo ambapo uchaguzi ulifanyika.
Upigaji kura haukufanyika katika maeneo bunge yote 547 ya nchi hiyo kutokana na mgomo wa upande wa upinzani, vita katika mkoa wa kaskazini wa Tigray, vurugu za kikabila na changamoto za kufikishwa vifaa vya kupigia kura kwenye maeneo matatu kati ya majimbo kumi nchini Ethiopia.
Uchaguzi utafanyika mnamo Septemba 6 katika maeneo ya Harar na Somali lakini jimbo la Tigray bado halijapangiwa tarehe ya kufanyika uchaguzi.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Birtukan Mideksa amekiri kuwepo changamoto hizo lakini amesema mchakato wa kupiga kura umewahakikishia watu juu ya kuwepo na serikali walioichagu kupitia kura zao.
Wakati huo huo Tume ya uchaguzi imesema uchaguzi utarudiwa kwenye maeneo 10.
Matokeo ya uchaguzi huo yameonyesha kwamba vyama vya upinzani nchini Ethiopia na wagombea huru walipata idadi ndogo ya kura.
Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa Twitter, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ameandika kuwa uchaguzi huo ni wa kihistoria, na kwamba chama chake kimepata faraja kubwa kwamba kimechaguliwa na watu kuiongoza nchi.
Uchaguzi huo wa Juni 21 ni wa kwanza kwa Abiy kupigiwa kura tangu alipoteuliwa kuwa waziri mkuu mnamo 2018 kufuatia maandamano ya miaka kadhaa yaliyopinga serikali.
Angalia:
Upinzani uliogawika unahisi kudhulumiwa
Vyama vya upinzani vilivyogawika nchini Ethiopia vimepata viti 11 tu. Birhanu Nega, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Ethiopian Citizens for Social Justice (ECFSJ), amesema chama chake kimewasilisha malalamiko zaidi ya 200 kwa kwa tume ya uchaguzi juu ya kura hiyo.
Ethiopia, ambayo ni nchi ya pili kwa ukubwa barani Afrika, ina zaidi ya raia milioni 37 waliojiandikisha kupiga kura. Tume ya uchaguzi nchini humo imesema zaidi ya asilimia 90 ya watu walijitokeza kupiga kura.
Kuvunja muungano
Waziri Mkuu Abiy Ahmed aliuvunja muungano wa vyama tawala EPRDF uliokuwa na vyama vinne na badala yake akunda chama kipya cha PP mnamo mwaka 2019. Hatua hiyo ilisababisha kutengana na chama cha Tigray People's Liberation Front (TPLF), ambacho kilitawala kwa karibu miongo mitatu.
Soma zaidi:UN na tume ya haki za binadamu Ethiopia zataka raia walindwe
Hali haikuwa shwari tangu wakati huo na ndipo vikaibuka vita mnamo Novemba mwaka uliopita. Watu maelfu wamekufa na wengine wapatao milioni 2 wamegeuka kuwa wakimbizi. Umoja wa Mataifa umetoa tahadhari ya kutokea baa la njaa katika jimbo la Tigray. Waziri mkuu Abiy amekosolewa mno kutokana na jinsi alivyosimamia mzozo wa Tigray.
Vyanzo:/DPA/AFP/https://p.dw.com/p/3wJja