1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia: Asilimia 50 ya baraza la mawaziri ni wanawake

Oumilkheir Hamidou
17 Oktoba 2018

Asilimia 50 ya mawaziri katika baraza jipya nchini Ethiopia ni wanawake. Hii ni rekodi mpya kuwahi kuwekwa na Ethiopia ikiwa ni sehemu ya mageuzi tangu waziri mkuu, Abiy Ahmad alipokabidhiwa hatamu za uongozi.

https://p.dw.com/p/36gpi
Äthiopien Parlament bestätigt neues Kabinett
Picha: Federal Government Communication Affairs Office of Ethiopia

Baraza jipya la mawaziri la Ethiopia limeweka rekodi kwa kujumuishwa asilimia 50 ya wanawake, ikiwa ni pamoja na waziri wa kwanza wa ulinzi, mwanamke, katika historia ya nchi hiyo ya pembe ya Afrika. 

Bunge la Ethiopia liliidhinisha kwa sauti moja majina ya baraza jipya la mawaziri lililopendekezwa na waziri mkuu mpenda mageuzi Abiy Ahmed.

"Mawaziri wetu wanawake watazisuta hoja kwamba wanawake hawawezi kuongoza" amesema Abiy alipokuwa akiwasilisha pendekezo lake bungeni."Uamuzi huu ni wa kwanza katika historia ya Ethiopia na pengine ya kwanza pia barani Afrika".

Mageuzi Ethiopia chini ya Abiy Ahmed

Ethiopia inashuhudia mageuzi ya kina ya kisiasa mpaka ya kiuchumi tangu waziri mkuu, Abiy Ahmed mwenye umri wa miaka 42 alipokabidhiwa hatamu za uongozi mwezi wa Aprili uliopita baada ya miezi kadhaa ya maandamano dhidi ya serikali na kutoa ahadi ya kuitishwa uchaguzi huru na wa haki.

Nchi hiyo muhimu ya pembe ya Afrika inajiunga na kundi dogo la nchi, nchi kati ya hizo zikiwa za ulaya ambako wanawake wanashikilia asilimia 50 au zaidi ya nyadhifa serikalini- hayo ni kwa mujibu wa shirika linalojumuisha mabunge pamoja pia na shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia akina mama.

Baraza jipya la mawaziri 20 ni la pili kuundwa tangu Abiy alipoingia madarakani mwezi April uliopita. La kwanza lilikosolewa kutokana na kuwepo idadi ndogo ya mawaziri wa kike.
Baraza jipya la mawaziri 20 ni la pili kuundwa tangu Abiy alipoingia madarakani mwezi April uliopita. La kwanza lilikosolewa kutokana na kuwepo idadi ndogo ya mawaziri wa kike.Picha: picture-alliance/AP Photo/Saudi Press Agency

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau wameanzisha mnamo miaka ya hivi karibuni mpango wa kuheshimu wizani sawa wa jinsia serikalini.

Wizara ya Ulinzi kuongozwa na mwanamke

Aisha Mohammed Musa ataongoza wizara ya ulinzi ya Ethiopia. Mwanamke mwengine, spika wa zamani wa bunge Muferiat Kamil ataongoza wizara ya masuala ya amani katika wakati ambapo nchi hiyo, ya pili yenye wakaazi wengi zaidi barani Afrika inakabiliwa baadhi ya wakati na mivutano  mikubwa ya kikabila kila wakati ambapo wakaazi wake wanazidi kujivunia uhuru wa kisiasa.

Wizara ya amani itasimamia shughuli za idara yenye nguvu ya usalama na upelelezi wa taifa, taasisi ya mtandao wa habari na usalama, halmashauri kuu ya  polisi , idara ya usalama wa fedha na kituo cha habari.

Baraza jipya la mawaziri 20 ni la pili kuundwa tangu Abiy alipoingia madarakani mwezi April uliopita. La kwanza lilikosolewa kutokana na kuwepo idadi ndogo ya mawaziri wa kike.

Ethiopia imekuwa ikitajwa kuwa nchi ambayo mwanamme ndie mwenye usemi wa mwisho katika jamii na inasumbuliwa na uhaba wa ukosefu wa wizani sawa wa jinsia."Wanawake na wasichana wananyimwa haki wakilinganishwa na wenzao wa  kiume katika sekta kadhaa, ikiwa ni pamoja na elimu, afya na haki za kimsingi za binaadam" shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia masuala ya akina mama limesema.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman