1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Eritrea yapeleka kisiri makombora, na silaha za hali ya juu Somalia.

Jane Nyingi27 Julai 2007

Silaha za hali ya juu zimeendelea kuwafikia wapiganaji wa kiislamu nchini Somalia kutoka Eritrea kwa mfano makombora yanayorushwa kutoka nchi kavu. Nyingi ya silaha hizo zimeingizwa nchini humo kisiri na kujipata mikononi mwa wapiganaji hao wa mahakama za kiislamu.

https://p.dw.com/p/CHjz
Polisi wakishika doria wakati wa mkutano wa pamoja wa amani mjini mogadishu ulioandaliwa na serikali ya mpito:
Polisi wakishika doria wakati wa mkutano wa pamoja wa amani mjini mogadishu ulioandaliwa na serikali ya mpito:Picha: AP

Kwa mujibu wa ripoti ya hivi majuzi kwa baraza la usalama la umoja wa mataifa iliyochapishwa na umoja huo, kwa sasa kuna mrundiko wa silaha nchini somalia hiki kikiwa kiwango cha juu cha silaha tangu mapema miaka ya 1990 wakati serikali ya dictator Mohammed Said Barre ilipinduliwa na kulifanya taifa hilo lilo kaskasini mashariki mwa africa bila ya serikali.

Eritrea ambayo inaelekezewa lawama zote imekataa kata kata kuhusika katika kupeleka silaha hizo hasa makombora yanayorushwa kutoka nchi kavu. Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya umoja wa mataifa kuna picha kutoka kwa kanda za video za wapiganaji hao wakibeba makombora aiana ya SA-18 yaliyotumiwa kuitungua ndege ya belarus ambayo ililazimika kutua kwa dharura mjini mogadishu,mji mkuu wa Somalia.

Kundi la umoja wa mataifa lilopewa jukumu la kuchunguza silaha hizo mwezi aprili pia lilionyesha kamati ya usalama ya umoja huo iliyoongozwa na balozi wa africa kusini Dumisani Kumalo,kanda ya video inayoonyesha kombora hilo lililotumiwa katika kujaribu kuitungua ndege hiyo. Kombora hilo ni mojawapo ya yale yaliyoiiizwa nchini humo kutoka eritrea.

Eritrea ni hasimu mkuu wa Ethiopia, na wanadiplomasia wanasema mataifa hayo mawili yamekuwa yakiwapiganisha raia wa somalia tangu mwaka jana. Asmara imekuwa ikiwaunga mkono wapiganaji wa kiislamu huku ethiopia ikiwa upande wa serikali. Ethiopia hata ilivipeleka vikosi vyake nchini humo kuisadia serikali na kuwaondoa wapiganaji wa kiislamu mjini mogadishu.

Marekani inayoamini kuwa wapiganaji hao wa kiislamu wana uhusiano na kundi la kigaidi la al-qaeda,vikosi vyake vilifanya mashambulizi mawili ya angani mwezi januari.Mashambulizi hayo yalifanywa pwani mwa kijiji cha Bargal kunakoaminika ni maficho ya wafuasi wa kundi hilo la kigaidi la al.qaeda.

Taarifa nyingine ni kuwa wapiganaji wa kiislamu na wanasiasa wa upinzani nchini somalia waliokwenda mafichoni nchini Eritrea wamepuuzilia mbali mkutano wa pamoja wa amani mjini mogadishu ambao pia ulikuwa umewaalika wanamgambo walioashambulia jumba kulikokuwa kunafanyika mkutano huo.

Mapema waandalizi wa mkutano huo uliokuwa umehairishwa mara mbili walisema hawatafanya mashauri yeyote kuhusu kugawanywa kwa nyadhifa za kisiasa na kuwa wapiganaji wa kiislamu walikuwa tu wanahudhuria mkutano huo kama wawakilishi wa koo zao.

Mkutano huo ulikuwa umeandaliwa na serikali ya mpito ya rais Abdullahi Yusuf.

Serikali hiyo ya mpito inataka kufufua huduma zote zilikwama miaka 16 iliyopita kufuatia kupinduliwa kwa serikali ya said barre na kulifanya taifa hilo kuwa bila serikali hali iliyosababisha vyeti vya kusafiria nchini humo kuwa miongoni mwa hati za kusafiria zinazotumika vibaya kote duniani, na kupatikana kwa urahisi kimagendo hasa katika eneo la africa mashariki.

Serikali hiyo imeifungua ofisi ya uhamiaji katika harakati za kutafuta ungwaji mkono na wananchi.