Eritrea yaituhumu Ethiopia
18 Agosti 2011Wanadiplomasia katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamesema Ethiopia imekuwa ikitafuta uungwaji mkono wa baraza hilo juu ya ombi lililotolewa na jumuia ya Ushirikiano wa Maendeleo ya IGAD- kwa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika wa kuiwekea vikwazo sekta yake ya madini ya Eritrea inayostawi, kutokana na madai kuwa nchi hiyo inawasaidia waasi wanaopigana dhidi ya serikali ya Somalia.
Eritrea imekuwa ikikanusha tuhuma kwamba inawapa fedha na silaha wapiganaji wa al Shabaab, shutuma ambazo zililifanya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwaka 2009, kuiwekea vikwazo vya silaha nchi hiyo ya pembe ya Afrika pamoja na kuzuia mali na marufuku ya kusafiri kwa viongozi wake wa ngazi za juu, pamoja na makampuni.
Mwezi Uliopita Jumuia ya IGAD, ambayo inajumuisha mataifa saba ya mashariki mwa Afrika ilitaka Eritrea iwekewe vikwazo zaidi katika sekta yake ya madini na kstiks malipo yanayoletwa na raia wa nchi hiyo waishiyo nje.
Nchi hiyo ya Eritrea imeonekana iko katika ustawi mzuri katika sekta yake ya madini, hali ambayo inaweza kufufua uchumi wake wenye matatizo. Aidha malipo inayoyapata nchi hiyo. kutoka kwa raia wake wengi waishiyo nje ya nchi hususan mashariki ya kati, na katika nchi za magharibi, ndio chanzo chake kikubwa cha ubadilishaji wa fedha za kigeni.
Taarifa iliyotolewa na ujumbe wa Eritrea katika Umoja wa Mataifa imeeleza kusikitishwa na jinsi Ethiopia inavyofanya kampeni za kuihujumu nchi hiyo iweze kuwekewa vikwazo zaidi, chini ya kisingizio kwamba inavuruga amani katika eneo la pembe ya Afrika.
Eritrea imetoa tuhuma hizo dhidi ya Ethiopia wakati rais wa nchi hiyo Isaias Afewerki leo anakamilisha ziara yake ya siku tatu nchini Uganda, kuzungumzia hali ya usalama katika eneo hilo. Uganda imepeleka wanajeshi wake katika kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika mjini Mogadishu, Somalia kupambana na wapiganaji wa al Shabaab.
Taarifa hiyo imeongeza kusema kwamba kampeni hizo za Ethiopia zimekusudia kuendeleza nia yake ya kuondoa utawala uliopo kupata njia ya kuingia katika bahari ya Sham.
Imesisitizia pia kwamba tuhuma kuwa Eritrea inachochea ghasia katika kanda hiyo ni kupotosha sera ya nje ya nchi hiyo.
Ethiopia ilipoteza mamlaka yake kwa bahari hiyo, baada ya kutengana na Eritrea mwaka 1993. Nchi hizo mbili pia zimekuwa zikipigania mpaka, kuanzia mwaka 1998 hadi 2000. Na mabishano yao mpaka sasa bado hayajapatiwa ufumbuzi licha ya kupewa ufafanuzi mwaka 2002 juu ya mpaka wao, na tume ya kimataifa inayohusika na mipaka.
Ethiopia pia imekuwa ikitaka kuimarisha vikwazo vya kimataifa dhidi ya Eritrea tangu jopo la Umoja wa Mataifa liliposema mwezi uliopita kwamba nchi hiyo inahusika na kula njama za kupanga mashambulio ya mabomu katika mkutano wa Umoja wa Afrika uliofanyika Addis Ababa mwezi Januari.
Ethiopia imetupilia mbali madai hayo ya Eritrea, kwa kusema kuwa ni jaribio la kutaka kupotosha ukweli kwamba nchi hiyo imeshindwa kufuata maazimio ya Umoja wa Mataifa.
Mwandishi Halima Nyanza(afp, reuters)
Mhariri: Aboubakary Liongo