Erdogan:Vikwazo dhidi ya Qatar havikubaliki
13 Juni 2017Mgogoro huo umeiweka Uturuki katika nafasi tete kutokana na Qatar kuwa mshirika wake mkuu katika eneo hilo la Ghuba huku pia ikidumisha uhusiano wake unaoimarika na Saudi Arabia, taifa lenye ushawishi mkubwa katika eneo hilo. Matamshi ya Erdogan yametolewa siku nane baada ya Saudi Arabia, Umoja wa falme za kiarabu,Bahrain na Misri kuvunja uhusiano wao na Qatar kwa madai ya kuunga mkono makundi ya wapiganaji wa kiislamu,madai aliyoyakanusha vikali. Akiwahutubia wanachama wa chama chake cha AK bungeni,Erdogan amesema leo atashiriki mkutano kwa njia ya simu na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron na Emir wa Qatar Tamim Bin Hamad al Thani kuujadili mgogoro huo.Hatua zilizochukuliwa na mataifa ya Ghuba dhidi ya taifa hilo ndogo lenye utajiri wa mafuta na gesi na lilo na idadi ya watu millioni 2.7 zimekatiza hata uagizaji chakula na vifaa vyengine kutoka nje."Uamuzi huo ni kama hukumu ya kifo dhidi ya Qatar.Taifa hilo limeathirika upande wa chakula,dawa na chochote unachoweza kufikiria.Hata kufunga anga zake kwa ndege za Qatar” amesema Erdogan. Qatar, ambayo asilimia 80 ya chakula chake kilikuwa ni kutoka mataifa jirani kabla ya kuvunjika uhusiano wa kidplomasia sasa imelazima kuzigeukia Iran na Uturuki kupata chakula na maji.
Erdogan aitetea Qatar kuhusu ugaidi
Rais Erdogan amekanusha vikali madai kuhusishwa Qatar na magaidi,na kusema taifa hilo limesadia kukabiliana na wapiganaji wanaojiita dola la kiislamu-IS. "Qatar sio nchi inayounga mkono ugaidi. Badala yake Qatar pamoja na Uturuki zimeonyesha msimamo mkali dhidi ya dola la Kiislamu IS ambalo limesababisha uharibifu mkubwa na maumivu katika eneo letu."Rais Erdogan pia anatazamiwa kufanya mazungumzo kwa njia ya simu na rais wa Marekani Donald Trump kuhusiana na mzozo huo wa eneo la ghuba japo siku ya mazungumzo hayo haijatangazwa. Erdogan ameahidi kuendelea kuisaidia Qatar na kusema mzozo huo unapaswa kushughulikiwa kabla ya kumalizika mwezi mtukufu wa Ramadhani.Ingawa mgogoro huo kwa kiasi fulani umetulia ,lakini malumbano yanaendelea katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Mwandishi:Jane Nyingi AFP/AP
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman