Erdogan ashinda kura ya maoni, wapinzani walalamika
17 Aprili 2017Mabadiliko hayo makubwa ya katiba yaliyoidhinishwa kupitia kura hiyo ya maoni yanaunda mfumo wa madaraka ya rais ambao utampa rais Erdogan madaraka zaidi kuliko kiongozi yeyote tangu muasisi wa Uturuki Mustafa Kemal Ataturk na mrithi wake Ismet Inonu.
Kambi ya "ndio" imeshinda kwa asilimia 51.4 ya kura dhidi ya asilimia 48.6 kwa upande wa "hapana", tume ya uchaguzi imesema katika tarakimu zilizonukuliwa na shirika la habari la Anadolu, katika zoezi la kuhesabu kura kwa misingi ya asilimia 99.5 ya masanduku ya kura. Watu waliojitokeza kupiga kura ni asilimia 85.
Matokeo ya kura hiyo pia yanaathari pana kwa Uturuki ambayo imejiunga na jumuiya ya kujihami ya NATO mwaka 1952 na katika kipindi cha mwisho cha nusu karne nchi hiyo imelenga katika kujiunga na Umoja wa Ulaya.
Sherehe mitaani
Kundi kubwa la watu waliokuwa wakipunga bendera walisherehekea ushindi huo mitaani, Erdogan akiisifu Uturuki kwa kuchukua "uamuzi wa kihistoria".
"Pamoja na umma, tumeweza kufikia mabadiliko muhimu katika historia yetu," ameongeza.
Lakini waungaji mkono wa upinzani katika wilaya zinazompinga Erdogan za mjini Istanbul wameonesha kutoridhishwa kwa kupiga mabakuli na sufuria kwa vijiko na umma na kufanya kelele za kupinga. Mamia ya watu pia waliingia mitaani katika maeneo ya Besiktas na Kadikoy.
Mkuu wa mamlaka kuu ya uchaguzi Sadi Guven amethibitisha kwamba kambi ya "ndio" imeibuka mshindi, lakini upinzani umeapa kupinga matokeo hayo.
Kura hiyo ya maoni ilifanyika chini ya amri ya hali ya hatari ambayo imeshuhudia watu 47,000 wakikamatwa katika ukandamizaji baada ya jaribio lililoshindwa la mapinduzi dhidi ya Erdogan Julai mwaka jana.
Mwishoni mwa kampeni iliyokuwa na hamasa nyingi , kambi ya "hapana" iliweza kuongeza idadi ya kura wakati kura zaidi zikihesabiwa , baada ya kuwa nyuma kwa muda mrefu katika matokeo ya awali, lakini kambi hiyo ilishindwa kuipita kambi ya kura za "ndio".
Wakati huo huo theluthi mbili ya Waturuki wanaoishi nchini Ujerumani wamepiga kura zao wakimuunga mkono rais Recep Tayyip Erdogan katika kura ya maoni inayotaka kumpa madaraka zaidi rais. Asilimia 63.1 ya wapigakura Waturuki nchini Ujerumani wameunga mkono hatua hiyo, limesema shirika la habari la Uturuki Anadolu mapema leo Jumatatu.
Maoni ya viongozi mbali mbali
Taarifa ya pamoja ya rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean-Calude Juncker na waziri mwenye dhamana ya masuala ya kigeni katika Umoja huo Federica Mogherini imesema , mabadiliko ya katiba na hususan utekelezaji wake utatathminiwa kwa misingi ya jukumu la Uturuki kama nchi inayotaka kujiunga na Umoja huo na mwanachama wa baraza la Ulaya.
Mkuu wa jukwaa la haki za binadamu barani Ulaya Thorbjorn Jagland amesema kwamba Uturuki inapaswa kupima hatua yake nyingine kwa makini baada ya kura hiyo ya maoni ambapo kambi ya "ndio" ilishinda kwa kiwango kidogo.
Mwandishi: Sekione Kitojo /dpae / afpe
Mhariri: Yusra Buwayhid