1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan afananisha hatua ya Uholanzi na Manazi

11 Machi 2017

Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki ameilinganisha hatua ya Uholanzi kupiga marufuku ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Uturuki nchini humo na manazi kutokana na mzozo wa kampeni ya kura ya maoni ya Uturuki.

https://p.dw.com/p/2Z38k
Türkei Erdogan wirft Deutschland «Nazi-Praktiken» vor
Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki.Picha: Reuters/M. Sezer

Uturuki inawataka raia wake walioko nje kuunga mkono kura ya ndio kuhusu mabadiliko ya katiba ya nchi hiyo. Matamshi makali ya kiongozi huyo yamekuja baada ya Uholanzi kusema kwamba itazuwiya kibali cha kuruhusu kutuwa kwa ndege iliomchukuwa waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu kuhudhuria maandamano ya kampeni kuunga mkono kura ya ndio juu ya mabadiliko ya katiba ambayo yatamuongezea madaraka Rais Erdogan.

Uamuzi wa Uholanzi wa kumpiga marufuku Cavusoglu kufanya ziara na kuwa na mkutano wa hadhara katika mji wa bandari wa Rotterdam umekuja baada ya Ujerumani na mataifa mengine ya Ulaya pia kushuhudia hatua za kupiga marufuku matukio ya kampeni hizo za wanasiasa wa Uturuki.

Lakini tofauti na Ujerumani ambapo kampeni kadhaa ziliokuwa zimepangwa kufanyika zilizuiliwa na serikali za mitaa nchini Uholanzi serikali iliingilia kati kupiga marufuku ziara hiyo ya Cavusoglu.

Mabaki ya wanazi na mafashisti

Deutschland Mevlüt Cavusoglu in Bonn
Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlüt Cavusoglu .Picha: picture-alliance/SvenSimon

Erdogan ameuambia kutano wa hadhara mjini Istanmbul hapo Jumamosi kwamba " wao ni mabaki ya Wanazi ni mafashisti" ikiwa ni siku chache baada ya kwa ghadhabu kulinganisha hatua za kuzuwiya maandamano hayo nchini Ujerumani na "vitendo vya manazi ."

Erdogan amesema "Mpigeni marufuku waziri wetu wa mambo ya nje kuingia nchini humo kwa kadri mnavyoweza lakini kuanzia sasa tuangalie vipi ndege zenu zitaweza kutuwa nchini Uturuki."

Cavusoglu alisema Jumamosi asubuhi kwamba kwa atakwenda Ritterdam kwa vyo vyote vile na kuishutumu Uholanzi kwa kuwashikilia raia wa Uturiki walioko Uholanzi kama mateka.Amekiambia kituo cha tevisheni cha CNN lugha ya Kituruki kwamba wamewapeleka wananchi wao nchini humo ili wakachangie uchumi wao.Waziri huyo ametishia kuiwekea nchi hiyo vikwazo vikali vya kiuchumi na kisiasa iwapo atazuiliwa kuingia nchini humo.

Erdogan dikteta

Waholanzi wanatarajiwa kupiga kura katika uchaguzi wa taifa hapo Jumatano ambao  hisia dhidi ya wahamiaji imekuwa ikitimiza dhima kubwa huku mgombea wa sera kali za Kizalendo Geert Wilders akimwita Erdogan kuwa ni dikteta.

Deutschland Köln Pro-Erdogan-Demonstration
Wafuasi wa Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki.Picha: Reuters/T. Schmuelgen

Uholanzi ni maakazi ya watu 400,000 wenye asili ya Kituruki na serikali ya      Uturuki  ina shauku ya kukusanya kura za wananchi wake walioko nje kabla ya kufanyika kwa kura hiyo ya maoni ya Aprili 16.

Mikutano ya hadhara minne ya Waturuki iliokuwa imepangwa kufanyika Austria na mmoja nchi Uswisi pia ilifutwa kwa kutaja sababu za kiusalama jambo ambalo limezidi kuuchochea mzozo huo.

Erdogan anazitaka kura za Waturuki wanoishi nje hususan Ujerumani na Uholanzi kumsaidia kunyakuwa ushindi katika kura ya maoni mwezi ujao ambayo itarekebisha mustakbali wa nchi hiyo ambayo nafasi yake ya kupakana na Mashariki ya Kati inaifanya kuwa mshirika muhimu kimkakati kwa Jumuiya ya Kujihami ya NATO.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP

Mhariri : Zainab Aziz