1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan aanza ziara yake nchini Iran

7 Aprili 2015

Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan anafanya ziara nchini Iran ambapo atashiriki katika mikutano ya ngazi ya juu, licha ya mivutano ya karibuni kuhusiana na operesheni ya mashambulizi inayoongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen

https://p.dw.com/p/1F3Td
Tayyip Erdogan und Hassan
Picha: Reuters

Ziara hiyo inayoanza leo imekuwa ikipangwa kwa muda sasa, wakati baadhi ya wabunge wa Iran wakiitaka ifutiliwe mbali baada ya Erdogan kutangaza hadharani kuiunga mkono operesheni hiyo ya Saudi Arabia dhidi ya waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran na kuikosoa Iran kwa kujaribu "kuitawala kanda hiyo". Bruce Amani na ripoti kamili

Erdogan akiandamana na ujumbe wa mawaziri wa Uturuki, atafanya mikutano na Rais Hassan Rouhani na Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei. Wakati wa ziara hiyo, masuala yanayozihusu nchi hizo mbili yatajadiliwa kwa kina na pia kutakuwa na mashauriano kuhusu masuala ya kikanda na kimataifa.

Mataifa hayo mawili yana uhusiano imara wa kiuchumi, huku Iran ambayo inakumbwa na vikwazo vya nchi za magharibi, ikiwa muuzaji wa pili mkuu wa gesi nchini Uturuki ambapo inaipa mita za ujazo bilioni 10 kila mwaka.

Erdogan Khamenei Iran Türkei
Erdogan akiwa na Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei nchini Uturuki mwaka wa 2014Picha: Mehr

Hata hivyo uhusiano wa kidiplomasia umeathirika katika miaka ya karibuni, na hasa mgawanyiko mkali kuhusiana na namna ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi jirani ya Syria. Mapema wiki iliyopita, rais Erdogan alisisitiza kuwa ataizuru Iran "Kwa sasa tunabakia na mpango wa ziara yetu ya Iran, lakini tunaiangalia hali nchini Yemen. Matukio ya nchini Yemen ni muhimu. Huenda kukawa na hatua ambazo zitatuwezesha kufanya kila aina ya uamuzi. Lakini kwa sasa hakuna mabadiliko katika ziara yetu".

Erdogan alisema “Iran inatumia juhudi zake zote kuitawala kanda ya mashariki ya kati, na hilo haliwezi kuvumiliwa. Aliongeza kuwa hali hiyo inazikasirisha nchi nyingine za kikanda kama vile Saudi Arabia, na mataifa ya Ghuba.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Mohammed Javad Zarif alijibu akimshambulia Erdogan kwa maneno aliishutumu Uturuki kwa kusababisha mashaka katika mashariki ya Kati kuhusiana na sera zake zenye malengo ya kupindukia.

Hata hivyo licha ya tofauti zao, nchi zote mbili zimeiacha wazi milango yao ya mazungumzo. Mzozo kuhusiana na mashambulizi ya anga yanayoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya waasi wa Houthi nchini Yemen, unaonekana kuwa mkubwa zaidi baina ya pande hizo mbili tangu mzozo wa mwaka wa 2011-2012 kuhusiana na ujenzi wa sehemu ya mradi wa kinga ya makombora ya NATO katika ardhi ya Uturuki, japokuwa Uturuki ilisisitiza kwa wakati huo kuwa haikuilenga jirani yake.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/reuters

Mhariri:Hamidou Oummilkheir