1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

England, Wales zalenga hatua ya mtoano

Admin.WagnerD20 Juni 2016

England na Wales zinawania kuimarisha nafasi zao kuingia katika awamu ya mtoano katikaq michuano ya kombe la mataifa ya Ulaya Euro 2016 nchini Ufaransa .

https://p.dw.com/p/1JAB9
UEFA EURO 2016 England - Russland
Wachezaji wa timu ya England wakitafakari jamboPicha: picture-alliance/Sven Simon/F. Hoermann

Tuanze na kombe la mataifa ya Ulaya , Euro 2016, ambapo England na Wales zinalenga leo kuimarisha nafasi zao kuingia katika awamu ya mtoano wakati timu zote katika kundi la B zinanafasi kuweza kusonga mbele. England baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya ndugu zao wa Wales , inaongoza kundi hilo kwa kuwa na pointi nne, wakati Wales na Slovakia zina pointi tatu kila moja.

Urusi haijaonesha umahiri wake hadi sasa , lakini na wao pia wana nafasi wakiwa na pointi moja. Iwapo watashinda mchezo wao wa leo dhidi ya Wales watakuwa na pointi nne na kuirejesha nyumbani Wales ikiwa na pointi zake tatu tu.

Frankreich Fußball-EM Frankreich vs Schweiz in Lille
Paul Pogba (kushoto) akipambana na mchezaji wa UswisiPicha: Reuters/G. Fuentes

England inapambana na Slovakia mjini Saint-Etienne ikitambua kwamba sare inatosha kuwaingiza katika duru ijayo, na ikiwa itashinda itajihakikishia kushika nafasi ya kwanza katika kundi hilo la B.

Mchezaji wa kati wa Wales Joe Allen amesema ana matumaini kumbukumbu ya kufungwa katika mchezo wa mchujo wa Euro 2004 dhidi ya Urusi zinaweza kuwatia nguvu na kuweza kunyakua nafasi kuingia katika duru ya timu 16 zitakazobaki katika fainali hizi wakati timu hizo zitakapokutana tena leo usiku mjini Toulouse katika mchezo wao wa mwisho katika kundi B.

Baada ya kumaliza wakiwa wapili baada ya Italia katika kundi lao la mchujo, Wales ilipoteza mchezo huo kwa kufungwa bao 1-0 na Urusi mwaka 2003 na walikosa nafasi katika fainali ambazo zilifanyika nchini Ureno.

Deschamps amsifu Pogba

Wakati huo huo kocha wa Ufaransa Didier Deschamps amemsifu mchezaji wake wa kati Paul Pogba na kwamba ana uwezo mkubwa sana , baada ya mchezaji huyo jana kuweka kando wiki ya matatizo na kung'ara katika mchezo wa jana uliomalizika kwa sare ya bila kufungana na Uswisi.

Frankreich Fußball-EM Rumänien vs Albanien in Lyon Jubel
Wachezaji wa Albania wakishangiria ushindi wao wa kihistoriaPicha: Getty Images/C. Brunskill

Shabiki mmoja wa Ufaransa amesema haja katishwa tamaa na sare ya jana.

"Bado tumefurahi licha ya kupata pointi moja. Angalau tumefanya vizuri, tumeshika nafasi ya kwanza katika kundi letu. Uswisi wamefurahi pia. Kila mtu amefurahi."

Matokeo hayo yana maana kwamba Ufaransa itacheza na timu itakayokata tikiti ya nafasi ya tatu kutoka ama kundi C, au D , ama E katika timu 16 zitakazosalia katika kinyang'anyiro hicho mjini Lyon , hapo Juni 26.

Vyombo vya habari vya Albania

Vyombo vya habari nchini Albania leo vilisherehekea ushindi wa kwanza wa nchi hiyo katika mashindano makubwa , ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Romania hapo jana , na kuwa na matumaini kwamba ushindi huo utatosha kuipeleka timu hiyo katika awamu ijayo ya mtoano.

EM Frankreich Training der deutschen Nationalmannschaft Thomas Müller
Thomas Mueller wa UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa

Gazeti la kila siku la Shekuli limeisifu timu ya taifa kwa kusema "Ushindi wa kwanza wa kihistoria katika kombe la Ulaya," wakati Televisheni ya Klan ilisema " Albania ilisubiri miaka 68 kwa hili."

Lakini licha ya ushindi huo Albania itabidi kusubiri kwa muda wa siku tatu hivi , wakati taifa hilo dogo la eneo la Balkan litakapofahamu iwapo limefanikiwa kuingia katika timu 16 zilizofuzu kuingia katika duru ijayo.

Timu hiyo itabidi kusubiri hadi michezo ya makundi itakapomalizika siku ya Jumatano kabla ya kufahamu iwapo ni moja kati ya timu nne zilizoshika nafasi ya tatu katika makundi yao zinazoingia katika kundi la timu 16 zilizofuzu kuingia katika awamu hiyo ya mtoano.

Die Manschaft

Timu ya taifa ya Ujerumani haijaonesha makali yake hasa hadi sasa, na mshambuliaji hatari wa timu hiyo Thomas Mueller bado hajapata mbinu za kufumania nyavu. Magoli ya mwanzo ya Mueller yaliisaidia timu ya taifa ya Ujerumani . Die Manschaft , kushinda kombe la dunia miaka miwili iliyopita, na pia alichangia mabao matano katika kombe la dunia mwaka 2010 nchini Afrika kusini.

Lakini hali ya kungoja inaendelea ili kusherehekea bao lake la kwanza katika michezo saba katika michuano miwili ya kombe la Ulaya.

Frankreich Fußball-EM Deutschland vs. Polen in Saint-Denis
Robert Lewandowski (katikati) akipambana na wachezaji wa UjerumaniPicha: Reuters/K. Pfaffenbach

"Natumai naweza kufunga bao, lakini kama nilivyokwisha sema kabla ya mashindano, sio suala kuu," Mueller amesema jana Jumapili , kabla ya mchezo wa mwisho wa Ujerumani wa awamu ya makundi dhidi ya Ireland ya kaskazini katika uwanja wa Parc des Princes mjini Paris kesho Jumanne.

Kwa upande mwingine mchezaji mwenzake katika klabu ya Bayern Munich Robert Lewandowski wa Poland ataiongoza timu hiyo kupambana na timu ambayo tayari imekwisha nyoosha mikono juu kusalim amri katika mashindano haya Ukraine kesho katika mchezo wa mwisho wa kundi C na sare katika mchezo huo itatosha kuwavusha Wapoland kuingia katika awamu ya mtoano.

UEFA EURO 2016 Deutschland - Ukraine - Ausschreitungen in Lille
Wahuni katika michezo katika Euro 2016Picha: picture-alliance/Maxppp/E. Bride/La voix du nord

Hata kipigo hakitaleta madhara makubwa kwa Poland iwapo Ujerumani itashinda dhidi ya Ireland ya kaskazini.

Siku ya Jumatano itakuwa mwisho wa awamu ya makundi, ambapo kundi D litajitupa uwanjani kuamua nani anaingia katika timu 16 bora.

Mchezaji wa kati wa Uswisi Granit Xhaka ametoa tahadhari kubwa katika awamu ya mtoano katika michuano hii ya Euro 2016 kwa kuonesha uwezekano wa kupambana na Ujerumani baada ya Uswisi kufikia awamu ya mtoano kwa mara ya kwanza kufuatia sare ya jana ya bila kufungana na Ufaransa.

Ufaransa ilishika usukani wa kundi hilo kwa kuwa na pointi 7 wakati Uswisi imefikia awamu hiyo ya mtoano baada ya kuibuka wa pili wakiwa na pointi tano.

Hii ina maana kwamba Uswisi itacheza ama na Ujerumani, Poland ama Ireland ya kaskazini ikitegemea kundi hilo la C litamaliza michezo yake vipi kesho Jumanne.

Wakati Ujerumani na Poland zinafungana kwa pointi na magoli , kuna uwezekano kuliko watabiri walivyotarajia kwamba mabingwa wa dunia Ujerumani huenda wakamaliza wakiwa katika nafasi ya pili katika kundi hilo.

"Hata Ujerumani inaweza kushindwa," Xhaka , amewaambia waandishi habari. "Iwapo itakuwa Ujerumani katika mchezo wa timu 16 ama mchezo wa fainali hii haina maana kwangu. Lakini kwangu mimi itakuwa vizuri tukikutana nao katika fainali." amedokeza Xhaka.

Ghasia za mashabiki

Kesho pia kutakuwa na mtanange mwingine kati ya Croatia na Uhispania katika mchezo wa mwisho katika kundi la D usiku ambapo mtazamo utakuwa zaidi kuhusu mashabiki wahuni wafanya fujo kuliko uwanjani.

Frankreich Fußball-EM Frankreich vs Schweiz in Lille zerrissene Trikots
Jezi ya Granit Xhaka ikiwa imechanikaPicha: Reuters/G. Fuentes

Mashabiki wahuni wa Croatia wamesababisha ghasia katika michezo yote miwili ya timu yao hadi sasa na shirikisho la soka la bara la Ulaya UEFA linatarajiwa kutoa tamko kuhusiana na uchunguzi wa tabia ya mashabiki wa Croatia baadaye leo.

UEFA ilianzisha uchunguzi wa kinidhamu baada ya mashabiki wa Croatia kurusha viripuzi na kuingia uwanjani wakati wa mchezo wao wa ufunguzi katika kundi D baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Uturuki.

Nayo Uturuki inabakiwa na mchezo mmoja tu kuweza kukata tikiti yake kuingia katika awamu ya mtoano ya Euro 2016 lakini mlinzi Gokhan Gonul anaamini bado wana nafasi, iwapo wataishinda Jamhuri ya Czech katika mchezo wao wa mwisho wa kundi D kesho Junamme.

"Kuna kitu ambacho kila mara timu ya taifa ya Uturuki hufanya , ambacho ni kuufukuza mchezo hadi dakika za mwisho," amesema mlinzi huyo Gonul mwenye umri wa miaka 31.

Hata hivyo Jamhuri ya Czech ina jiamini mno baada ya kutoka nyuma , kwa kufungwa mabao mawili lakini walimaliza mchezo huo kwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Croatia.

Uturuki , kwa kulinganisha , walikosa meno wakati waliposhindwa kwa bao 1-0 dhidi ya Croatia katika mchezo wao wa kwanza kabla ya kupewa funzo la soka la mabingwa watetezi Uhispania kwa kuchapwa mabao 3-0.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / ape / afpe / dpae
Mhariri: Yusuf , Saumu