Eneo la Maghreb lavamiwa na Al Qaeda
3 Februari 2010Tawi la kigaidi la Waislamu wenye imani kali linawateka nyara watu kutoka mataifa ya nje, linafanya biashara ya silaha pamoja na madawa ya kulevywa na kuna kitisho cha kusambaa vita ya jihad hadi katika nchi yenye matatizo ya kivita ya Nigeria. Ripoti
Katika eneo la jangwa ambalo halina kitu chochote na mpaka usiokuwa na mwisho kati ya Algeria , Mauritania, Mali na Niger kuna eneo tu kama linavyojulikana kuwa halina mwenyewe. Magaidi na waporaji katika eneo hilo wanahifadhi kila kitu, silaha, madawa ya kulevywa, husafirisha wahamiaji haramu, wale ambao wanataka kuingia katika bara la Ulaya. Na katika eneo hili ambalo haliingiliki, magaidi wamefanikiwa kulifanya eneo lao la kujificha. Magaidi wameweza mara kwa mara kugonga vichwa vya habari kutokana na matukio ya utekaji nyara. Majira ya joto ya mwaka 2009 waliweza kumuua mateka wao raia wa Uingereza. Hii ikiwa ni alama ya kundi la al-Qaeda kutoka eneo la Afrika ya kaskazini, ama maghreb kama anavyoeleza mtaalamu wa masuala ya ugaidi Mathieu Guidere''Mateka kutoka nchi za nje kwa magaidi ni kama wafungwa wa kivita, ambao hutumika pia kama karata turufu ya kufanya majadiliano, ili kupata fedha ama kuweza kuwatesa wafungwa wao. Ni pale tu taifa la Ulaya magharibi kama katika tukio hili la kusikitisha, Uingereza , ilikataa kufanya majadiliano, ndipo Al-Qaeda huwauwa mateka wao.''
Mwakilishi wa Osama
Kundi la kigaidi la Al-Qaeda liliundwa mwishoni mwa mwaka 2006 kutoka katika kile kinachojulikana kama GSPC, ambao ni mtandao usiojulikana wa kigaidi nchini Algeria. Kiongozi wake wakati huo al-Zawahiri binafsi alijitangaza kuwa mwakilishi wa Osama bin Laden. tangu wakati huo kundi hilo la eneo la Maghreb likapata jina la al-Qaeda katika eneo la maghreb na linaendesha mambo yake lenyewe. Kundi hilo linahisi kuwa linalazimika kufuata nadharia ya al-Qaeda nchini Afghanistan, licha ya kijifanyia mambo yake yenyewe. Mathieu Guidere anasisitiza kuwa al-Qaeda katika eneo la maghareb haliangalii tena mustakabali wake kuelekea mataifa ya magharibi nchini Algeria, bali linataka kupanua shughuli zake katika sehemu kubwa zaidi kuelekea upande wa kusini, na kupeleka kile kinachojulikana kama vita takatifu katika eneo lote la jangwa la Sahara, pamoja na Afrika kusini mwa jangwa la Sahara.''Mashambulio ya kigaidi pamoja na mateka wengi wanaokamatwa inamaana ya maafa makubwa kwa utalii katika eneo hilo. Hofu ya mambo hayo inasababisha watu wanaotaka kusafiri kwenda katika eneo hilo kutoka duniani kote kutofanya hivyo na kuharibu uchumi wa mataifa yanayohusika kwa kiasi kikubwa. Al-Qaeda inaiona biashara ya utalii kama aina mpya ya ukoloni na ubeberu, na kwamba magaidi hao hawataki kabisa kuwaona watu ambao si Waislamu katika maeneo yao .''
Makundi haram
Athari ya kutengwa na mataifa ya magharibi pia inaonekana wazi katika maeneo ya kaskazini ya Nigeria ambako kuna masikini wengi. Makundi ya kidini kama Boko Haram yanajifananisha na Taliban na yanapigana ili kuunda taifa la Kiislamu, na kutokana na hali hiyo baina ya Waislamu wa upande wa kaskazini na Wakristo wa upande wa kusini kila mara kuna kuwa na hali ya machafuko na watu kwa mamia huuwawa. AQMI, tawi la mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda upande wa Afrika kaskazini , linatumia hali hii ya wasi wasi. Tayari magaidi wamekwisha sema , nadharia yao ya Uislamu wenye msimamo mkali inayopata nguvu nchini Nigeria ni lazima iendelezwe. Kwa kupeleka silaha na risasi pamoja na mapambano. Mtaalamu wa masuala ya ugaidi , Mathieu Guidere anasema kuwa hilo lilikuwa ni suala la muda tu, licha ya kuwa , bado Nigeria si kituo cha al-Qaeda . Lakini hali ni tete. Katika hali hiyo ya wasi wasi kuna suala la serikali isiyo na kiongozi ambapo rais anaendelea kupata matibabu nje ya nchi hadi leo . Bila shaka Waislamu wenye imani kali wanaendelea kupata wafuasi.
Katika hali hiyo hicho si kitisho kwa eneo la jangwa la Sahara pekee. Kundi la al-Qaeda katika eneo la maghreb hawakujiweka tu kufanya ugaidi katika eneo la jangwa, lakini pia linalenga maeneo ya mataifa magharibi. Kijana wa Ki-Nigeria Umar Faruk Abdulmutallab, ambaye alijaribu kuilipua ndege mjini Detroit ni mmoja kati ya watu waliopata mafunzo kutoka kwa al-Qaeda. Kama tunaweza kuyaamini mashirika ya kijasusi, al-Qaeda tayari katika eneo la Maghreb lina vikundi dazeni vya kigaidi katika mataifa ya Ulaya. Kwa sasa wanasubiri tu.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ZR
Mhariri: Thelma Mwadzaya.