1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ECOWAS yaisimamisha Guinea baada ya jeshi kutwaa mamlaka

9 Septemba 2021

Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika magharibi ECOWAS imesimamisha uanachama wa Guinea katika mkutano wa kilele wa viongozi wa jumuiya hiyo baada ya wanajeshi wa nchi hiyo kuiangusha serikali ya rais Alpha Conde.

https://p.dw.com/p/4065P
Symbolbild | ECOWAS | Westafrikanischer Regionalblock verabschiedet neuen Plan zur Einführung einer einheitlichen Währung im Jahr 2027
Picha: Pius Utomi Ekpei/AFP/Getty Images

Katika taarifa kwa waandishi wa habari, waziri wa mambo ya nje wa Burkina Faso Alpha Barry,aliyeshiriki kwenye mkutano huo wa viongozi wa nchi 15 za ECOWAS uliofanyika jana jioni kwa njia ya video, mjini Ouagadougou amesema Guinea kwa sasa imesimamishwa kwenye mabaraza yote ya kupitisha maamuzi ya jumuiya hiyo ya ECOWAS.

Luteni Kanali Mamady Doumbouya aiiyetwaa madaraka nchini Guinea
Luteni Kanali Mamady Doumbouya aiiyetwaa madaraka nchini GuineaPicha: AFP

Waziri wa mambo ya nje wa Burkina Faso amefahamisha kwamba jumuiya hiyo sasa itauomba Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kuidhinisha uamuzi wake huo. Wakati huo huo waziri wa mambo ya nje wa Burkina Faso amesema ujumbe wa upatanishi wa jumuiya hiyo utakwenda hii leo Alhamisi katika mji mkuu wa Guinea, Conakry kufanya mazungumzo na mamlaka mpya.

Soma Zaidi: Viongozi wa mapinduzi Guinea wawaachia wafungwa wa kisiasa

Vikosi maalum vinavyoongozwa na Luteni Kanali Mamady Doumbouya vilitwaa madaraka katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi mnamo siku ya Jumapili na kumkamata Rais Alpha Conde mwenye umri wa miaka 83 na watu wengine. Jumuiya ya ECOWAS inataka kuachiwa huru mara moja kwa rais Alpha Conde na kuanhzishwa mchakato wa kurejea kwenye katiba. Kuna taarifa kwamba baadhi ya watu waliokamatwa tayari wameachiwa. Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya na Marekani zimelaani vikali mapinduzi ya kijeshi ya nchini Guinea.

Rais wa Guinea Alpha Conde aliyeng'olewa madarakani
Rais wa Guinea Alpha Conde aliyeng'olewa madarakaniPicha: Facebook/Alpha Condé

Hali ya kutoridhika kwa umma nchini Guinea imejitokeza kwa miezi kadhaa kutokana na uchumi wa nchi hiyo kudhoofika na janga la COVID- 19 likiwa ni moja wapo ya sababu ya kudhoofika kwa uchumi wa Guinea lakini pia umma umekuwa ukilalamika juu ya uongozi wa Conde, rais wa kwanza aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia mnamo mwaka 2010 na kisha kuchaguliwa tena mnamo mwaka 2015. Lakini hali ilibadiliaka mwaka jana, pale Conde alipopitisha katiba mpya ambayo ilimruhusu kuwania muhula wa tatu katika uchaguzi wa mwezi Oktoba mwaka uliopita. Conde alishinda uchaguzi lakini vyama vya upinzani vilisema kura hiyo ilikumbwa na udanganyifu. Hatua hiyo ilisababisha maandamano makubwa ambapo baadhi ya waandamanaji waliuawa.

Vyanzo:AFP/DPA