1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ebola,Itikadi kali na Wakimbizi Magazetini

4 Julai 2014

Kitisho cha kuenea maradhi ya Ebola, jinsi mataifa ya Afrika yanavyopania kupambana na wafuasi wa itikadi kali na shida wanazokabiliana nazo wakimbizi wa Sudan kusini ni miongoni mwa mada za Afrika magazetini wiki hii

https://p.dw.com/p/1CVki
Madaktari na wauguzi wakipima damu za wagonjwa walioambukizwa Ebola nchini Sierra LeonePicha: Reuters

Tuanzie na kitisho cha kutapakaa homa hatari ya Ebola katika eneo la Magharibi la bara la Afrika.Taktriban magazeti yote ya Ujerumani yamezungumzia kitisho hicho kinachotokana na maradhi ya kuambukiza ya Ebola yanayotajikana kuwa changamoto kubwa kabisa ya afya kuwahi kuukabili Umoja wa mataifa na mashirika yake.Gazeti la Süddeutsche Zeitung linazungumzia jinsi virusi vya Ebola vinavyoingia mwilini mwa binaadam na maradhi kuchomoza-maradhi ambayo Süddeutsche Zeitung lililowanukuu wataalam wa afya linasema yanaambukiza vibaya sana."Machozi ya kifo" ndiyo kichwa cha maneno cha ripoti ya gazeti hilo la mjini Munich linalozungumzia ziara iliyofanywa na matabibu wa nchi za magharibi katika nchi zilizoambukizwa homa ya Ebola Afrika Magharibi.Woga na wasi wasi wa wauguzi wanaovalia mavazi ya kinga toka kichwani mpaka miguuni,wauguzi wanaokwepa kuwagusa wagonjwa ni picha inayopunguza badala ya kuongeza hali ya kuaminiana kati ya mgonjwa na muuguzi.Ndio maana Süddeutsche Zeitung linamnukuu Stephan Becker wa taasisi ya maradhi ya virusi katika chuo kikuu cha Marburg,unakofanywa pia uchunguzi wa viruisi vya Ebola, akitetea umuhimu wa kupatiwa mavazi ya aina nyengine wauguzi,kupatiwa mafunzo na kutambua wapi hasa hatari ya kuamabukiza inakutikana,ili kurahisisha maingiliano na kurejesha hali ya kuaminiana kati ya madaktari,wauguzi na wagonjwa-pengine hilo litasaidia kupunguza balaa la kutapakaa homa ya Ebola.LInamaliza Süddeutsche Zeitung.

Fikra ya Mwasisi Mwenza wa Umoja wa Afrika Yazingatiwa

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linazungumzia jinsi mataifa ya Afrika yanavyojitahidi kwa pamoja kuwaandama wafuasi wa itikadi kali ya dini ya kiislam.Wazo hilo si la leo lakini utekelezaji wake unahitajika haraka zaidi hivi sasa kuliko wakati wowote ule mwengine;linaandika gazeti hilo linalozungumzia kuhusu mpango wa nchi za Umoja wa Afrika kuunda kikosi cha kuingilia kati haraka ili kukabiliana na wafuasi wa itikadi kali wa dini ya kiislam.Azma hiyo inaungwa mkono na nchi zote wanachama,mabishano yanachomoza katika suala kikosi hicho kiundwe lini,na vikosi vitoke nchi gani.Afrika kusini na Misri zinahimiza kikosi hicho kliundwe haraka.Mataifa mengine,ikiwemo Nigeria ambayo sehemu yake ya kaskazini kwa miaka sasa inakumbwa na mashambulio ya kigaidi ya Boko Haram yanasita sita.Na mengineyo mfano wa Kongo yanahisi mapambano dhidi ya wafuasi wa itikadi kali ya dini ya kiislam hayawahusu.Frankfurter Allgemeine linakumbusha fikra ya kuundwa kikosi cha pamoja cha nchi za Afrika ilitolewa mwaka 1958 na rais wa kwanza wa Ghana Kwame Nkrumah.Fikra hiyo ilishindikana kutokana na utawala wa ubaguzi wa rangi na mtengano Apartheid nchini Afrika Kusini.Baada ya mashambulio ya kigaidi ya septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani fikra hiyo ilizushwa upya na Umoja wa Afrika kuahidi kikosi kiundwe hadi ifikapo mwaka 2015.Wakati ule hakujakuwa na pupa kwasababu wafuasi wa itikadi kali bado hawakuwa wakiangaliwa kama kitisho.Kiitisho kimeibuka kwa kuchipuka makundi ya kigaidi ya Al Shabab nchini Somalia,Boko Haram nchini Nigeria,na Aqmi katika eneo la jangwa la Sahara.Na hiyo ndio maana Umoja wa Afrika unahimiza kikosi hicho kilichobadilishjwa jina toka kikosi cha kuingilia kati haraka ASF na kuwa kikosi cha Afrika cha kutoa jibu la haraka kwa mizozo-ACIRC kiharakishwe.Vipi kuchangia wanajeshi sawa na lile la kugharimia shughuli za kikosi hicho ni suala la khiari.Hata hivyo kitasimamiwa na Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa.Hadi sasa mataifa 13 kati ya 54 wanachama wa umoja wa Afrika yameshaelezea utayarifu wao kujiunga na kikosi hicho,linaandika Frankfurter Allgemeine.

Porträt Kwame Nkrumah
Rais wa Kwanza wa Ghana Dr.Kwame NkrumahPicha: Getty Images

Wakimbizi wa Sudan Kusini wataabika

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusiana na hali ya wakimbizi wa Sudan Kusini.Die Tageszeitzung linazungumzia shida wanazokabiliana nazo wakimbizi 45 elfu wanaoishi katika hali ya shida katika kambi ya wakimbizi ya Bentiu.Matope yameenea kila pembe katika msimu huu wa masika,maji safi ya kunywa hakuna na zoezi la kuokota kuni za kupikia na kupasha moto limekuwa la hatari.Matokeo yake linaandika die Tageszeitung ni utapia mlo na maradhi.Shirika la madaktari wasiojali mipaka sio tuu linawahudumia wagonjwa bali pia linawashughulikia waliokufa kwa hofu wasije wakazikwa kambini.

Südsudan Flüchtlingslager in Bor
Wakimbizi wa Sudan Kusini katika kambi ya BorPicha: Reuters

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Basis/Presser/All

Mhariri: Mohammed Khelef