1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ebola ,Kobane na Uchumi wa Ujerumani Magazetini

15 Oktoba 2014

Hofu ya mambukizo ya Ebola,vita vya Kobane na athari zake kwa mkataba wa amani kati ya Uturuki na wakurd wa chama cha PKK na makadirio ya ukuaji wa kiuchumi nchini Ujerumani ni miongoni mwa mada magazetini

https://p.dw.com/p/1DVrf
Hospitali ya St George ya mjini Leipzig alikokuwa akitibiwa mtu aliyeambukizwa virusi vya Ebola na ambae amefariki hivi karibuniPicha: picture-alliance/dpa/Hendrik Schmidt

Tuanze lakini na kitisho cha kuenea maradhi hatari ya Ebola.Gazeti la "Volksstimme" linaandika:"Maradhi hayo hatari yameshafika.Sio tu katika eneo fulani la Afrika,bali hapo tu karibu.Mjini Leipzig,mgonjwa wa Ebola amefariki dunia.Hakuna dawa ya kutibu maradhi haya hatari-kilichobaki ni kuwatenga tu wagonjwa na kujiwekea matumaini pengine watapona.Tauni nyengine inatuathiri.Wataalam wa idara za afya nchini Marekani wanakadiria hadi mwisho wa mwaka 2015 watu laki tano watakuwa wameshaambukizwa Afrika Magharibi-au pengine wengi zaidi ya hao.Katika ulimwengu mdogo ulio wazi,hatari ya kuenea katika mabara mengine haiwezi kuepukwa.Cha kusisimua lakini ni ile hali kwamba hadi wakati huu maelfu ya wajerumani wamejiandikisha kwa khiari kwenda kusaidia kupambana na maradhi hayo kule kule yalikoanzia.Ni sawa na kujitafutia mauti,kwasababu hakuna kinga inayoweza kudhamini kwamba hawatoambukizwa.Kilichobakia ni kuwavulia kofia.Hata hivyo mkakati jumla tu dhidi ya Ebola ndio utakaosaidia kuepusha hofu zisienee kote ulimwenguni.

Uchunguzi wa maoni umefanywa humu nchini kupima maoni ya wananchi yakoje kuhusiana na kitisho cha kuenea maradhi hatari ya Ebola.Gazeti la "Stuttgarter Nachrichten" linaandika:"Utafiti wa maoni ya umma uliofanywa hivi karibuni umebainisha kwamba raia wengi wa Ujerumani wangeona bora kama hospitali za Ujerumani zisingewatibu tena wagonjwa wa Ebola.Baadhi wanataka watu wanaotokea Afrika Magharibi wasiruhusiwe kuingia humu nchini.Kimaadili jambo hilo haliwezekani na wala halisaidii kuzuwia maradhi hayo hatari yasienee.Hakuna sababu ya kuingiwa na wahka humu nchini.Wenye kuchochea hofu wanabidi wazuwiliwe.Na hata kama kuna kadhia nyengine za Ebola zitakazoripotiwa nchini Ujerumani,hikma na busara zinabidi zitangulizwe mbele.

Erdogan acheza na moto

Vita vya Kobane vinatishia kuvuruga makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwaka jana kati ya serikali ya Uturuki na waasi wa zamani wa chma cha wakurd-PKK.Gazeti la "Reutlinger General-Anzeiger" lnaandika:"Msimamo wa serikali ya mjini Ankara unaweza kuchochea tena vita vya wenyewe kwa wenyewe katika eneo la kusini mashariki la Anatolia.Sera za Erdogan kuelekea jamii ya wakurd na jamii za wachache kwa ujumla pamoja pia na utaratibu wa amani pamoja na PKK zinatishia kushindwa.Erdogan anawalazimisha PKK waanzishe upya mpambano kwa mtutu wa bunduki,hata kama wenyewe wasingependelea tena kupigna."

Lengo la bajeti bila ya nakisi liheshimiwe

Mada yetu ya mwisho magazetini hii leo inahusu makadirio ya ukuaji wa kiuchumi nchini Ujerumani.Gazeti linalosomwa na wengi "Bild" linaandika:"Uchumi wa Ujerumani haujaanza bado kupungua,hata hivyo hali ya mambo si ya kuridhisha.Mzozo wa Ukraine,vitisho vya wanamgambo wa itikadi kali wa dola la kiislam IS,na Ebola,yote hayo yanadhoofisha usalama wa dunia.Matokeo yake ni kwamba biashara yetu ya nje inapungua.Sigmar Gabriel aligusia tangu msimu wa kiangazi uliopita kuhusu madhara ya migogoro ya kimtaifa.Na hiyo hasa ndio sababu ya kufuata mkondo ulioko,lengo la kusawazisha bajeti lisikiukwe.Na kwa hilo makamo Kansela Gabriel hajakosea.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman