DW inakuletea mchezo wa Karandinga
DW inakuletea mchezo wa Karandinga
Haya, twende Sasa!
Kila kitu kiko tayari: Fundi mitambo, Christof Wurster (Kushoto), Grace Kabogo, (aliyeketi) mtayarishaji na mwandaaji wa vipindi vya Noa Bongo-Jenga Maisha Yako na Simon John (kulia) mtayarishaji msaidizi, waliofanikisha kurekodiwa mchezo mpya wa ''Karandinga'', hadithi nne kuhusu upelelezi katika uhalifu wa Ugaidi, uwidaji haramu, unyakuzi wa ardhi na dawa bandia.
Chanzo cha shambulizi ni nini?
Katika mchezo wa ''Chimbuko la Itikadi Kali'', Inspekta Brenda (Sarah Kassim, kulia) akiwa na Kamishna wa Polisi Cletus (Deo Songa, kushoto) wakijadiliana namna ya kukabiliana na ugaidi na kufanya uchunguzi unaofichua taratibu zinazowafanya vijana kujiunga na makundi ya kigaidi.
Sababu za kujiunga na ugaidi
Macray Rusasa (Katikati) anayecheza kama Bobo anayetaka kujiunga na kundi la kigaidi. Katika sehemu ya Tano ya mchezo huu wa ''Chimbuko la Itikadi Kali'', yuko kwenye kibanda cha kutoa huduma za mtandao kwa ajili ya kuwasiliana na mkufunzi wake. Ili kuweza kupata sauti nzuri inayoonyesha mazingira ya kwenye kibanda cha kutoa huduma za mtandao, tulitumia ubao uliowekwa kati yake na kipaza sauti.
Mjadala bungeni
Watu hawa wanawakilisha sehemu ya serikali ya nchi ya kufikirika ya Kululaland. Hawa ni wabunge ambao katika mchezo huu wa ''Chimbuko la Itikadi Kali'', japokuwa wengine wanaonekana wakitabasamu, wako katika mjadala mkali kuhusu namna ya kupambana na magaidi.
Kuwalinda wanyamapori
Dokta Susan Galana (Mwajuma Abdul, kushoto), ni mtetezi wa wanyamapori na mwanaharakati wa mazingira kwenye mji wa Bovu. Katika sehemu hii ya mchezo wa ''Wawindaji Haramu'', anaonekana akiwa na Bwana Chang (Chacha Nyamaka, kulia), ambaye ni raia wa kigeni na mfanyabiashara haramu wa pembe za ndovu.
Kuwasaka wawindaji haramu
Katika mchezo wa ''Wawindaji Haramu'', tunamuona afisa upelelezi Allan (Aloyce Michael, kushoto) akifurahi baada ya kuwakamata wawindaji wawili haramu Emmanuel (Richard Mshanga, katikati) na John (Mzome Mahmoud, kushoto), ambao walikuwa ni wafanyakazi wa Bwana G. Walikuwa wakijipongeza baada ya kumaliza kurekodi sehemu yao, katika mbuga ya wanyamapori ya Bovu.
Mahojiano kuhusu kifo cha Peter
Kutoka kushoto ni afisa upelelezi Kalumba, (Aloyce Michael), Mfamasia Marijane (Deborah Dickson), mtayarishaji na mwandaaji Grace Kabogo, afisa upelelezi Salamisha (Sarah Kassim) na fundi mitambo Christof Wurster. Maafisa hao wawili wa upelelezi walikuwa wakimuhoji Marijane kuhusu kifo cha Peter, kilichotokana na kiwango kikubwa mno cha dawa, kwenye mchezo wa ''Dawa za Kutibu, Dawa za Kuua''.
Mchango wa vyombo vya habari
Katika mchezo wa ''Dawa za Kutibu, Dawa za Kuua'', tumeona jinsi waandishi wa habari walivyotoa mchango mkubwa kuielimisha jamii kuhusu matumizi ya dawa bandia. Mtangazaji wa kituo cha utangazaji cha kufikirika cha Ketagu (Editha Mayemba, kushoto) akiwa na mwandishi wa habari wa kituo hicho (Zainab Mlawa, kulia), wakijiandaa kutekeleza majukumu yao.
Kwenye wakati mgumu
Katika mchezo wa ''Ardhi ya Chongwe'', mwili wa Chifu Awombo, unakutwa katika kingo ya mto kwenye shamba la maua. Je aliuawa na mnyama wa mwituni kama serikali inavyotaka watu wa Chongwe waamini, ama aliuawa na watu? Pichani, Inspekta Mwamto (Chacha Nyamaka), anakabiliwa na wakati mgumu kuamua kama ashikilie msimamo rasmi wa serikali au azma yake ya kutafuta hasa kilichotokea.
Harakati za kuepusha machafuko
Grace Kabogo (kushoto), mtayarishaji na mwandaaji wa michezo ya Noa Bongo-Jenga Maisha Yako, akimwelekeza Jembe (Lucy Mwinuka, kulia) sehemu anayotakiwa kuigiza katika mchezo wa ''Ardhi ya Chongwe''. Sehemu hiyo inamtaka kuwa na wasiwasi na uharaka, hasa wakati akitoa taarifa kwa polisi na mpelelezi wa kujitegema Mweri, kuhusu nia ya Zumari kutaka kumvamia mkurugenzi wa shamba la maua waridi.