1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Duru ya pili ya Uchaguzi wa rais Guinea

3 Julai 2009

Mohammed Bacai Sanha na Koumba Yala kupambana katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais mpya atakayechukua mahala pa rais aliyeuwawa Joao Bernado Viera.

https://p.dw.com/p/IgQX
Rais aliyeuwawa Joao Bernardo "Nino" VieiraPicha: AP

Uchaguzi wa rais nchini Guinea Bissau umeingia katika duru ya pili itakayofanyika tarehe 2 mwezi wa Agosti ambapo mpambano utakuwa kati ya wagombea wawili Malam Bacai Sanha na Koumba Yala.Wagombea wote wawili ni viongozi wa zamani wa taifa hilo.Duru ya pili itafanyika baada ya duru ya kwanza iliyofanyika Juni 28 kushindwa kumpata mshindi wa moja kwa moja atakayechukua mahala pa rais aliyeuwawa Joao Bernado Viera.

Takriban miezi minne baada ya kuuwawa kwa rais Joao Bernardo Viera wananchi wa Guinea Bissau waliingia katika hatua ya kupiga kura katika uchaguzi wa rais mpya mnamo jumapili ya tarehe 28 mwezi wa Juni.Na siku tano baadae tume ya Uchaguzi ikatangaza matokeo ya mwanzo ambapo hakuna hata mgombea mmoja aliyeweza kupata wingi unaohitajika kuweza kuchukua uongozi wa nchi hiyo.

Der Markt von Gabu in Guinea Bissau.
''Wananchi wa Guinea-Bissau wataraji rais mpya ajae atautokomeza umaskini''Picha: Jochen Faget

Tume hiyo ya Uchaguzi jana alahamisi ikatangaza kwamba sasa kutabidi kufanyike duru ya pili ya Uchaguzi huo ambapo wagombea wawili wakuu ndio watakaopambana katika uchaguzi huo.Mkuu wa tume ya kitaifa ya uchaguzi Desejado Lima da Costa aliutangaza uamuzi huo mbele ya waaandishi wa habari akisema

''Naomba msikilize kwa makini matokeo ya uchaguzi wa rais.Malam Bacai Sanha na Mohammed Koumba Yala watachuana katika duru ya pili''

Katika matokeo ya duru ya mwanzo Malam Bacai Sanha wa chama tawala ambacho pia kimetawala kwa muda mrefu jukwaa la kisiasa nchini humo cha PAIGC ndiye aliyepata ushindi.Alikuwa na asilimia 39.59 idadi ambayo haikuweza kumfanya kutangazwa rais wa taifa hilo.

Nafasi ya pili ilichukuliwa na mpinzani wake wa karibu Mohammed Koumba Yala rais wa zamani wa nchi hiyo na kutoka chama cha PRS ambaye alikuwa na asilimia 29 ya kura.

Yala alikuwa madarakani kama rais kati ya mwaka 2000 na mwaka 2003 na utawala wake uligubikwa na shutuma za usimamizi mbaya na pia kukamatwa kwa wapinzani matukio ambayo yalisababisha kupinduliwa kwake madarakani.

Baada ya kutangazwa matokeo na tume ya uchaguzi wengi wa waangalizi walikuwa wakisubiri kitakachotangazwa na mgombea wa tatu Henrique Rosa ambaye baadae alisema amekubali kushindwa hata hivyo alisema hatomuunga mkono mgombea yoyote kati ya wagombea hao wawili watakaopambana tarehe mbili mwezi Agosti.Rosa aliibuka watatu kwa kupata asilimia 24.19 ya kura.Kwa mujibu wa mkuu wa tume ya uchaguzi Desejado Lima Da Costa idadi ya wapiga kura waliojitokeza katika uchaguzi haikuwa kubwa kama ilivyokuwa mwaka 2008 ambapo walioshiriki ilikuwa ni asilimia 82.Safari hii ni asilimia 60 tu ya wapiga kura ndio waliojitokeza.

Hata hivyo kila kitu kilikwenda vizuri kwa mujibu wa waangalizi wa Umoja wa Ulaya.Mkuu wa kundi la waangalizi wa Umoja huo Johan Van Hecke akizungumza baada ya matokeo ya uchaguzi alisema-

'Wapiga kura wametumia haki yao ya kupiga kura na uchaguzi umefanyika katika hali ya kuridhisha licha ya kutokea dosari ndogondogo kwa mfano katika utaratibu wa kufungwa vituo vya kupigia kura''

Kwa watu wa Guinea uchaguzi huo wa jumapili ulikuwa ni hatua ya mwisho ya matumaini katika taifa hilo.

Wananchi wa Guinea hawataki tu rais mpya bali pia wanataraji kwamba atakayeingia madarakani ataleta hali ya usalama na kuumaliza umaskini katika nchi hiyo iliyozongwa na ulaji rushwa kutokana kukithiri kwa biashara haramu ya madawa ya kulevya yanayopitishwa nchini humo na kuingia barani Ulaya.

Mwandishi: De Gouvela Helena/Saumu Mwasimba

Mhariri:M. Abdul-Rahman