1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Duru mpya mazungumzo ya Syria yaanza

Caro Robi
25 Januari 2018

Duru mpya ya mazungumzo yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa kuutafutia ufumbuzi mzozo wa Syria imeanza mjini Vienna, siku chache kabla ya mshirika wa karibu wa utawala wa Syria- Urusi kuanzisha mazungumzo mengine.

https://p.dw.com/p/2rWU1
Genf Staffan de Mistura, UN-Sondergesandter für Syrien
Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Di Nolfi

Duru mpya ya mazungumzo yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa kuutafutia ufumbuzi mzozo wa Syria imeanza mjini Vienna leo, siku chache kabla ya mshirika wa karibu wa utawala wa Syria- Urusi kuanzisha mazungumzo mengine kujaribu kuumaliza mzozo huo uliodumu kwa miaka saba sasa. 

Matumaini ni madogo ya kupatikana ufumbuzi wa vita vya Syria katika duru hii mpya ya mazungumzo yanayowaleta pamoja wajumbe wa serikali na wa upinzani lakini mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Steffan di Mistura ameelezea kuwa na matumaini akisema ni wakati muhimu sana.

Duru zilizopita za mazungumzo hayo ya kutafuta amani Syria yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa hayafanikiwa pakubwa huku majeshi ya Syria yakiungwa mkono na ya Urusi na Iran yakiendelea kupata mafanikio katika mapambano dhidi ya wanaopinga serikali ya Rais Bashar Al assad.

Jeshi hilo la Syria limefanikiwa kuyaokoa maeneo mengi ya nchi hiyo kutoka mikononi mwa waasi. Hivi karibuni, majeshi hayo yameongeza kampeni dhidi ya waasi katika maeneo ya Idlib na Ghouta Mashariki.

Syrien | anhaltende Kämpfe in der Region Ost-Ghouta
Mashambulizi ya kijeshi katika eneo la Ghouta Picha: Getty Images/AFP/A. Eassa

Uturuki nayo kwa upande mwingine imepeleka majeshi kaskazini mwa Syria kupambana dhidi ya wapiganaji wa Kikurdi ambao wana eneoo lako linalojitawala na wanaiona Uturuki kama kitisho kwa usalama wao.

Baada ya kuonekana kuvishinda vita dhidi ya wanaompinga, Rais Bashar Al Assad haonekani kuwa tayari kufanya mazungumzo ya dhati na waasi, wala kuondoka madarakani kama mojawapo ya matakwa ya waasi kuwa kuondoka kwa kiongozi huyo madarakani kutapelekea kufikiwa suluhisho la amani.

Uturuki na Urusi zimeandaa duru nane za mazungumzo.

Urusi, Uturuki na Iran zimeandaa duru nane za mazungumzo katika mji wa Astana, nchini Kazakhstan mwaka jana kwa lengo la kufikia makubaliano dhabiti ya kuundwa maeneo salama Syria na kupunguza usahama.

Mkutano ujao uliopangwa na nchi hizo tatu zinatarajiwa kufanyika mjini Sochi, nchini Urusi wiki ijayo. De Mistura anafahamu na kuutambua mkutano huo wa Sochi unaokwenda sambamba na huo wa Vienna lakini haijabainika wazi anapanga kushughulikia vipi suala hilo.

Nchi kadhaa za magharibi na za Kiarabu zinaamini mazungumzo yanayosimamiwa na Urusi yataweka msingi wa kupatikana jwa suluhisho ambalo litaungwa mkono na utawala wa Syria na washirika wake.

Kasachstan Astana syrische Rebellengruppen
Upande wa waasi ulipohudhuria mazungumzo ya amani yaliyofanyika mjini Astana, Disemba, 2017Picha: Getty Images/AFP/S. Filippov

Mjumbe mkuu wa Upinzani katika mazungumzo ya kutafuta amani Nasr Hariri amesema wataamua katika kipindi cha siku mbili zijazo iwapo utahudhuria mkutano huo wa Sochi utakaofanyika tarehe 30 mwezi huu au la akiongeza kuwa mazungumzo hayo yatakuwa kipimo kwa pande zote mbili iwapo zinajitolea kufikiwa kwa suluhisho la kisiasa au la kijeshi.

Urusi imewaalika wawakilishi wa asasi za kiraia wa Syria pamoja na Wakurdi katika mkutano huo. Wakurdi hata hivyo wamesema hawatahudhuria mkutano huo. Maafisa wa Marekani, Ufaransa, Uingereza pamoja na Saudi Arabia walikutana Paris siku ya Jumanne kujadili mchango wa Urusi katika mzozo wa Syria kupitia mazungumzo. 

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean Yves Le Drian amesema mkutano wa Vienna ndiyo matumaini ya mwisho ya kufikiwa suluhisho la kisiasa kwa mzozo wa Syria.

Duru zilizopita za mazungumzo ya Umoja wa Mataifa kuhusu Syria yaliyofanyika mjini Geneva, yalituama katika kujadili suala la kufanyika chaguzi mpya, kuwepo na mageuzi ya uongozi, katiba mpya na kupambana na ugaidi.

De Mistura hajafanikiwa kwa kiasi kikubwa kuzileta pande zinazozana Syria kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na ni katika duru iliyopita mwezi Desemba ambapo upinzani uliungana kutuma kundi la pamoja la wajumbe. Upande wa serikali umesimama kidete kupinga mazungumzo yoyote kuhusu hatma ya Assad katika siku za usoni.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/Afp
Mhariri:Iddi Ssessanga