Dunia yaukaribisha mwaka mpya 2019
1 Januari 2019Mwaka 2018 ni mwaka uliojaa changamoto kwa taasisi nyingi duniani, ikiwa ni pamoja na nyanja ya siasa, biashara , ushirika na dini. Mvua kubwa haikuwazuwia makundi ya watu kuujaza uwanja maarufu wa Times Square kwa ajili ya sherehe hizo za kila mwaka mjini New York, zikiambatana na muziki wa nyota kadhaa wa muziki.
Christina Aguilera aliwaburudisha maelfu ya watu, akijitokeza na vazi lake jeupe, huku wapenda muziki wakisherehekea katika mvua. Watu walilipa hadi dola 10 kupata vazi la pancho ambalo ni la plastiki ili kuweza kujikinga na mvua hiyo.
Mjini Rio de Janeiro nchini Brazil zaidi ya watu milioni 2 walisherehekea kuingia kwa mwaka mpya katika ufukwe wa Copacabana. Fashifashi zilizorushwa kwa muda wa dakika 14 ziliingiza Brazil katika mwaka 2019 masaa machache tu kabla ya mwanasiasa wa siasa kali za mrengo wa kulia Jair Bolsonaro kuapishwa kuwa rais wa nchi hiyo. Wabrazil wengi walikuwa barabarani kwenda katika mji mkuu wa Brasilia usiku wa jana kuangalia kuapishwa kwa kapteni huyo wa zamani wa jeshi la Brazil atakapoapishwa mchana wa Jumanne.
Mjini London Waingereza na familia zao waliukaribisha mwaka mpya kwa kengele cha saa kubwa ya Big Ben, licha ya kuwa saa hiyo maarufu duniani imezimwa kwa zaidi ya mwaka sasa kutokana na mradi wa kuikarabati. Bunge lilitangaza wiki iliyopita kwamba kengele kubwa ya saa hiyo itatoa sauti kuadhimisha kuingia kwa mwaka mpya kwa msaada wa mfumo maalum wa kielektroniki kutoa nishati kwa nyundo yake, ambayo ina uzito wa kilo 200.
Maandamano ya sherehe
Mjini Paris wakaazi wa mji huo walikusanyika katika eneo la uwanja wa Champ-Elysee kusherehekea mkesha wa mwaka mpya chini ya ulinzi mkali. Waandamanaji wanaoipinga serikali kutoka katika vuguvugu linalojulikana kama vizibao vya manjano wametoa miito katika mitandao ya kijamii , kufanya "sherehe za maandamano" katika mtaa huo mashuhuri.
Polisi nchini Ufaransa iliweka uzio katika eneo hilo, huku wakifanya upekuzi wa mifuko, kupiga marufuku pombe na kuzuwia magari kuingia katika eneo hilo. Wizara ya mambo ya ndani imesema siku ya Jumapili kuwa hatua kali za usalama zinahitajika kwasababu ya "kitisho cha juu cha ugaidi" na wasi wasi juu ya "maandamano ambayo hayakutangazwa."
Rais Emmanuel Macron alitoa hotuba yake ya kawaida kwa mwaka mpya na kueleza kwa ufupi malengo ya mwaka 2019, baadhi ya waandamanaji wakikasirishwa na kodi kubwa pamoja na upendeleo wake kwa biashara , waandamanaji wanapanga kuendelea na maandamano katika wiki zijazo.
Mjini Berlin mamia kwa maelfu ya watu walisherehekea kuanza mwaka 2019 katika eneo maarufu mjini berlin la lango la Brandenburg.
Utumwa mamboleo wakemewa
Sherehe za kila mwaka za mwaka mpya zilifanyika huku kukiwa na ulinzi mkali , ambapo kiasi ya maafisa wa polisi 1,300 waliwekwa katika kila eneo la mji huo mkuu wa Ujerumani na watu walipigwa marufuku kubeba fashifashi, chupa ama mifuko mikubwa na kuingia navyo katika eneo hilo la sherehe.
Ilipofika usiku wa manane , polisi ya mjini Berlin iliripoti matukio machache ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Kiongozi wa kanisa Katoliki ameueleza mwaka uliopita kuwa mwaka wa matatizo katika wakati wake akiwa madarakani kwa kuendesha misa na sala mbele ya sanamu kubwa la mchanga la mtu wa asili katika eneo hilo la makao makuu ya kanisa. Katika misa hiyo aliyoendesha , Francis alilalamikia juu ya vile watu wengi waliishi katika mwaka 2018 katika ukingo wa utu, kutokuwa na nyumba ama kulazimika kuingia katika aina ya utumwa wa kimamboleo.
Akiongozana na mkuu wake wa kutoa sadaka , Francis alikwenda nje ya uwanja wa Mtakatifu Petro , ambako alisalimiana na mahujaji na kusali kabla mbele ya sanamu hilo la mtu wa asili , lililochongwa kutokana na mchana wa tani 720.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Zainab Aziz