Dunia yapiga hatua kubwa kupambana na vifo vya watoto
23 Oktoba 2013.Katika ripoti iliyotolewa leo hii Shirika la kuawaokoa watoto Save the Children limeonya kwamba hakuna nafasi ya kuregeza kamba.
Ripoti ya shirika hilo iliopewa kichwa cha habari "Maisha Hatarini" imeangalia jinsi nchi 75 zinavyoshughulikia malengo ya kupambana na vifo vya watoto yaliowekwa na Umoja wa Mataifa hapo mwaka 2000 katika kutimiza Malengo ya Maendeleo ya Milenia Malengo hayo ni pamoja na kupunguza kwa theluthi mbili vifo vya watoto ifikapo mwaka 2015.
Ripoti hiyo inasema idadi ya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano wanaokufa kutokana na sababu zinazozuilika kama vile utapia mlo au ukosefu wa madawa kila mwaka, takriban imepunguwa kwa nusu kutoka milioni 12 hapo mwaka 1990 hadi kufikia milioni 6.6 hapo mwaka 2012.
Nchi zilizotia fora
Mbali na Niger miongoni mwa mataifa 10 ambayo yamepiga hatua kubwa katika kupambana na vifo vya watoto ni Liberia,Rwanda, Indonesia, Madagascar, India, China,Misri,Tanzania na Msumbiji.Kwa mujibu wa repoti hiyo ya shirika lisilo la kiserikali upande ambapo bado tatizo hilo ni kubwa, nchi ambazo hazikupiga hatua kubwa ni pamoja na Haiti, Papua New Guinea na Equatorial Guinea.
Hata hivyo kiwango cha vifo vya watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano ambavyo sio vya lazima bado ni kikubwa nchini Niger. Lakini kimepunguzwa sana kwa theluthi mbili kutoka 1,000 hadi 326 hapo mwaka 1990 na kutoka 1,000 hadi 114 hapo mwaka 2012.
Sehemu kubwa ya mafanikio yake imetokana na yale makundi yenye kipato.Hata hivyo Nigeri ikiwa ni mojawapo ya nchi maskini kabisa duniani inatekeleza mipango ya lishe na kutowa huduma bure za matibabu kwa wanawake wajawazito na watoto.
Dunia iko nje ya lengo
Lakini kwa jumla dunia iko nje ya lengo lililowekwa ambapo kiwango kikubwa cha vifo vya watoto kinazidi kujitokeza miongoni mwa nchi maskini duniani.
Kwa mfano Afrika magharibi na Afrika Kati imekuwa na asilimia 17 ya vifo vya watoto hapo mwaka 1990 na kuongezeka hadi asilimia 30 hapo mwaka 2013,vingi ya vifo hivyo vikitokea katika nchi zilizokumbwa na mizozo.
Patrick Watt mkurugenzi wa kampeni wa Shirika la Save the Children amesema maisha ya watoto milioni nne pia yangeliweza kuokolewa katika kipindi cha muongo mmoja uliopita ingelikuwa matumizi yangelikuwa sawa katika kupambana na vifo vya watoto miongoni mwa makundi yenye kipato.
Watt amekaririwa akisema wanapiga hatua za kihistoria katika vita dhidi ya vifo vya watoto lakini mafanikio hayo yasio kifani pia mara nyingi hufunika watoto wa kimaskini wanaoachwa nyuma ambapo katika kesi nyengine hali zao zinakuwa mbaya kupindukia.
Shirika hilo limezihimiza serikali kutekeleza mipango ya afya ya taifa ambayo inamfikia kila mtoto,wakiwemo watoto wachanga ambao ndio kwanza wamezaliwa kwa lengo la kuifanya mipango hiyo iwe inapatikana kikamilifu ifikapo mwaka 2030 na kupunguza utapia mlo ili kwamba kila mtoto awe anapata lishe wanayohitaji ili kuendelea kuishi na kunawiri.
Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/dpa
Mhariri: Moahammed Abdul-Rahman