1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yaomboleza kifo cha Helmut Kohl

17 Juni 2017

Viongozi wa dunia wa sasa na wa zamani wametoa salaam za rambirambi kufuatia kifo cha kansela wa zamani wa Ujerumani Helmut Kohl, muasisi wa kuungana upya kwa Ujerumani. Kohl alifariki Ijumaa akiwa na umri wa miaka 87.

https://p.dw.com/p/2erFi
Altbundeskanzler Helmut Kohl
Picha: picture-alliance/dpa/U. Baumgarten

Bendera zimeshushwa nusu mlingoti katika majengo ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels kufuatia habari za kifo cha Helmtu Kohl, kansela wa Ujerumani kuanzia mwaka 1982 hadi 1998, aliekuja kufahamika kama baba wa Ujerumani ilioungana.

Kohl alikuwa mmoja wa wanzilishi wa sarafu ya pamoja na Ulaya, alisimamia kuungana upya kwa Ujerumani Mashariki na Magharibi mwaka 1990, na alihudumu kama kansela wa Ujerumani ya Magharibi na kisha Ujerumani ilioungana.

Tukio la bahati kwa Wajerumani

Kansela Angela Merkel ambaye alinasihiwa pakubwa na Kohl, amemuelezea marehemu kama alama ya bahati kwa Wajerumani, akisema binafsi anashukur kwamba Kohl alikuwepo. Amesema katika juhudi zao zote, Helmut alikuwa mwamba tulivu na imara, na kwamba maisha yataendelea kuwa na hamasa kwa vizazi vya viongozi wa sasa na watakaokuja kuthubutu na kufanikiwa zaidi.

Helmut Kohl Bad in der Menge
Helmut Kohl katika kampeni za uchaguzi mjini Heiligenstadt jimboni Thueringen, Septemba 5, 1990.Picha: Picture-alliance/dpa/H. Hollemann

Viongozi wa Marekani wameomboleza kifo cha Kohl, wakisifu mchango wake katika kuiunganisha tena Ujerumani, ambapo rais wa zamani George H.W Bush amemueleza kuwa mmoja wa viongozi wakubwa zaidi wa Ulaya ya baada ya vita. "Helmut alichukia vita -- lakini alichukia zaidi utawala wa kiimla," alisema Bush katika taarifa yake kuhusu kansela huyo wa zamani wa Ujerumani.

Ameongeza kuwa kushirikiana na rafiki yake huyo mkubwa kusaidia kuhitimisha kwa amani vita baridi na kuungana upya kwa Ujerumani ndani ya jumuiya ya kujihami NATO, kutaendelea kuwa mmoja ya furaha zake kubwa katika maisha. Rais wa zamani Bill Clinton amemesema amehuzunishwa sana na kifo cha Kohl, ambaye uongozi wake wenye maono uliiandaa Ujerumani na Ulaya nzima kwa ajili ya karne ya 21.

"Aliombwa kujibu baadhi ya maswali mazito zaidi ya wakati wake, na katika kuyajibu kwa usahihi aliwezesha kuungana kwa Ujerumani imara yenye mafanikio na kuundwa kwa Umoja wa Ulaya," alisema Clinton, na kuongeza kuwa hatosahau siku alipotembea naye kupitia lango la Brandenburg mwaka 1994 kuhudhuria mkutano mkubwa upande wa mashariki, na kuona matumaini ya kweli machoni mwa mamia ya maelfu ya vijana.

Altbundeskanzler Helmut Kohl und US Präsident Bill Clinton
Kansela wa zamani Helmut Kohl akiwa na rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton mjini Potsdam, Ujerumani.Picha: Getty Images/AFP/S. Jaffe

Rafiki wa dhati wa Marekani

Rais Donald Trump amemsifu Kohl kama rafiki na mshirika wa Marekani. Amesema Kohl hakuwa tu baba wa muungano wa Ujerumani, lakini pia alikuwa mtetezi wa wa Ulaya na uhusiano wa kanda hiyo na Marekani. Amesema dunia imenufaika na maono yake na juhudi, na kuongeza kuwa urithi wake utaendelea kwa vizazi na vizazi.

Mwanae Walter Kohl aliwambia waandishi wa habari nje ya nyumba ya baba yake katika wilaya ya Oggersheim mjini Luwigshafen, kwamba Ulaya inahitaji watu kama baba yake wakati huu kuliko wakati wowote ule. "Unaweza kusema hivi: Watu wenye imani kama yake wangekuwa wazuri zaidi kwa Ulaya sasa hivi, ukitazama hali ya sasa mwezi Juni 2017," alisema Walter Kohl.

Walter ambaye hakuwa na uhusiano mzuri na baba yake hadi anakufa, amesema anajuta kwamba hawakusuluhishwa hadi matu yalipomkuta baba yake.

Mhimili wa historia ya Ulaya

Katibu Mkuu wa jumuiya kujihami NATO Jens Stoltenberg amemtaja Kohl kuwa mnasihi na rafiki yake, na chimbuko halisi la Ulaya. Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker amesema kohl alikuwa kiini cha historia ya Ulaya. Amesema alihakikisha muungano wa furaha wa nchi yake na kusaidia ujenzi wa Ulaya nzima na iliyo huru. 

Helmut Kohl ist tot Sohn Walter Kohl
Mwanaye Helmut Kohl, Walter Kohl ambaye baba yake amekufa hali ya kuwa hawaelewani.Picha: picture alliance/dpa/U. Anspach

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May amesema Kohl, kama kansela wa kwanza wa Ujerumani ilioungana tangu mwaka 1945, alikuwa kinara wa historia ya Ulaya, na kusema wamempoteza baba wa Ujerumani ya sasa.

Wengine waliotoa salaam ra rambirambi ni pamoja na rais wa baraza la Ulaya Donald Tusk, waziri mkuu wa Italia Paolo Gentiloni, Msemaji mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephen Dujarric, rais wa Ukrain Petro Poroshenko, waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani Henry Kissinger.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae, afpe,

Mhariri: Josephat Charo