1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Heshima zimeendelea kutolewa kwa Grass

14 Aprili 2015

Heshima zimeendelea kutolewa kwa mwandishi wa Ujerumani na mshindi wa tuzo ya Nobel Günter Grass, aliefariki akiwa na umri wa miaka 87.

https://p.dw.com/p/1F7Pq
Neueröffnung Günter Grass-Haus Lübeck
Picha: picture-alliance/dpa/Gambarini

Habari za kifo chake zilitangazwa na shirika lake la uchapishaji la Steidl mjini Göttingen.Tangu kilipojipatia umashuhuri duniani kote, kitabu chake alichokipa jina "Die Blechtrommel" au "Tarumbeta la bati" na kuchapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1959, mwandishi huyo wa kijerumani amekuwa akiangaliwa kama mtunzi muhimu kabisa wa enzi hizi.

Kitabu hicho ndicho kilichompatia tuzo ya Nobel ya uandishi fasaha mnamo mwaka 1999.Vitabu vyake vimetafsiriwa kwa lugha kadhaa. Katika muda wote wa maisha yake mwandishi vitabu huyo, amekuwa akishiriki katika mijadala kadhaa kuhusu maisha ya jamii.

Güunter Grass akionyesha sanamu za wacheza muziki katika Studio yake mjini Behlendorf. Mada ya muziki inakutikana katika kitabu chake cha mashairi cha "Last Dance."
Güunter Grass akionyesha sanamu za wacheza muziki katika Studio yake mjini Behlendorf. Mada ya muziki inakutikana katika kitabu chake cha mashairi cha "Last Dance."Picha: picture alliance/dpa/U. Perrey

Huzuni na mshangao

Naibu wa Kansela wa Ujerumani na mwenyekiti wa chama cha Social Democratic SPD Sigmar Gabriel, amesema wamepoteza si tu moja wa waandishi mahiri wa kihistoria katika Ujerumani ya baada ya vita vikuu vya dunia, lakini pia alikuwa rafiki mkubwa wa demokrasia ya kisoshalisti.

Alikuwa muungaji mkono mkubwa wa siasa ya kansela wa zamani wa Ujerumani Willy Brandt ya kufanya suluhu pamoja na nchi za Ulaya ya Mashariki na kukifanyia kampeni za uchaguzi chama cha Social Democratic.

Günter Grass alisababisha mvutano mkali mwaka 2012 alipotunga shairi lililokuwa likiikosoa Israel. Kifo chake kimezusha huzuni na mshangao mkubwa miongoni mwa wanasiasa na waandishi vitabu wenzake.

Maisha yake yaliyojaa vilima na mabonde, nyakati za ushindi na mivutano, yalianza Oktoba 16, 1927. Günter Grass alikulia katika maisha ya kimaskini.

Wazazi wake walikuwa na duka la vyakula katika mji wa Gdansk, (wakati huo ukijulikana kama Danzig), lakini wateja wao walikuwa maskini sana kiasi kwamba walishindwa kulipa bili zao. Familia hiyo ya kikatoliki iliishi katika nyumba ndogo sana.

Günter Grass akizungumza katika ukumbi wa sanaa mjini Göttingen.
Günter Grass akizungumza katika ukumbi wa sanaa mjini Göttingen.Picha: picture-alliance/dpa/P. Steffen

Kazi zake

Günter Grass aliandika michezo ya kuigiza, mashairi na hasa fasihi ya masimulizi ya kubuni, ambayo orodha yake ndefu ilihusisha vitabu kama vile "Paka na panya" na "Miaka ya Mbwa", ambavyo pamoja na "Tarumbeta la bati" vilikuwa sehemu ya tamthilia yake yenye sehemu tatu, pamoja na vitabu vingine lukuki.

Kazi zake nyingi zilihusu zaidi mazingira ya kisiasa na machafuko ya kijamii, kama vile kuzama kwa meli ya wakimbizi katika bahari ya Baltic mwaka 1945, dhima ya wasomi katika uasi wa Ujerumani mashariki mwaka 1953, maandamano ya wanafunzi ya mwaka 1968, kampeni za uchaguzi wa shirikisho na mahusiano ya kisiasa kati ya mashariki na magharibi.

Mwandishi: Iddi Ssessanga
Mhariri: Grace Kabogo