1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yalaani mauaji kwa kukatwa kichwa mwandishi Kenji Goto

1 Februari 2015

Jumuiya ya kimataifa imelaani mauaji kwa kukatwa kichwa ya mwandishi wa habari wa Japani Kenji Goto yaliofanywa na kundi la Dola la Kiislamu IS ambapo Japani imeapa kuwafikisha wahusika mbele ya mkono wa sheria.

https://p.dw.com/p/1EU5S
Mwandishi wa habari wa Japani Kenji Goto.
Mwandishi wa habari wa Japani Kenji Goto.Picha: Reuters/www.reportr.co via Reuters TV

Waziri Mkuu wa Japani Shinzo Abe amewaambia waandishi wa habari ofisini kwake huku machozi yakimlenga lenga kwamba ameghadhibika mno juu ya vitendo hivyo vya kigaidi vya uovu mkubwa na kukirihisha.

Amesema katu hawatawasamehe magaidi hao na ameahidi kuendelea kushirikiana na jumuiya ya kimataifa kuwafanya wajutie uhalifu wao.

Abe amesema serikali ilikuwa ikifanya kila juhudi kulishughulikia suala hilo na kwamba anasikitika sana kwamba hayo ndio yamekuja kuwa matokeo.

Japani kutosalimu amri kwa ugaidi

Waziri Mkuu huyo amesema serikali yake itaongeza msaada wake wa kibinaadamu kwa Mashariki ya Kati na kuahidi kwamba Japani kamwe haitosalimu amri kwa ugaidi na azma thabiti ya kutimiza wajibu wake katika mapambano ya jumuiya ya kimataifa dhidi ya ugaidi.

Waziri Mkuu wa Japani Shinzo Abe akizungumza na waandishi wa habari Tokyo.(01.02.2015)
Waziri Mkuu wa Japani Shinzo Abe akizungumza na waandishi wa habari Tokyo.(01.02.2015)Picha: Getty Images

Rais Barack Obama wa Marekani ameongoza shutuma za kimataifa kwa mauaji hayo aliyoyaita kuwa ya uovu mkubwa sana. Amesema kwa kupitia repoti zake Ogoto alitaka kwa ujasiri kuwasilisha hali inayowakabili watu wa Syria kwa ulimwengu wa nje.

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema "mauaji hayo ya kishenzi ...yanaonyesha ukatili unaowakabili watu wengi nchini Iraq na Syria."

Serikali ya Ufaransa na Uingereza nchi ambazo pia zimepoteza raia wake kutokana na mauaji yanayofanywa na kundi hilo la IS na kurekodiwa kwenye kamera pia zimelani mauaji ya mwandishi huyo wa Japani.

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron akisema huo ni ukumbusho zaidi kwamba kundi hilo la Dola la Kiislamu ni mfano halisi wa uovu usiothamini maisha ya binaadamu.

Kundi la IS lajigamba kuhusika

Kundi la Dola la Kiislamu limedai katika ukanda wa video uliotolewa kwenye mtandao hapo Jumamosi kwamba limemuuwa mwandishi huyo wa habari Kenji Goto ikiwa ni raia wa pili wa Japani kuuwawa kwa kukatwa kichwa katika kipindi cha wiki moja.

Goto ambaye ni mwandishi wa habari za vita anayeheshimika alionekana kwenye mkanda huo wa video akiwa kwenye mavazi ya rangi ya machungwa sawa na yale yanayovaliwa na wafungwa wanaoshikiliwa kwenye gereza la Marekani katika Ghuba ya Guantanamo akiwa amepiga magoti pembeni mwa mwanaume alijifunika kunzia kichwani hadi miguuni huko uso wake ukiwa umefichwa.

Mwanamke wa Kijapani akishikilia bango la kutaka kuachiliwa kwa Kenji Goto mjini Tokyo kabla ya kuuwawa kwake.
Mwanamke wa Kijapani akishikilia bango la kutaka kuachiliwa kwa Kenji Goto mjini Tokyo kabla ya kuuwawa kwake.Picha: Reuters/T. Hanai

Mwanaume huyo anayezungumza kwa lafidhi ya Kingereza inaonekana kuwa ni mwanamgambo yule yule wa kundi la IS aliyeonekana katika video za mauaji zilizopita.

Alikuwa akimwambia Waziri Mkuu wa Japani Shinzo Abe moja kwa moja kwamba mauaji hayo ni matokeo ya maamuzi mabaya ya serikali ya Japani akikusudia msaada wa kifedha ambao serikali ya Japani iliutowa kuwasaidia wakimbizi wanaokimbia kutoka maeneo yanayodhibitiwa na kundi hilo la IS nchini Iraq na Syria na kwamba huo ni mwanzo wa jinamizi kwa Japani.

Waziri wa ulinzi wa Japani amesema ukanda huo wenye kuonyesha mwili ukiwa na kichwa cha mtu kilichokatwa juu yake yumkini ni wa kweli.

Unyama na ushenzi wa IS

Kundi la wanamgambo la IS limekuwa likitumia sheria za kinyama kwa jina la Uislamu katika maeneo ambayo inayadhibiti nchini Syria na Iraq.Limekuwa likiwaua wananchi wenyeji halikadhalika wageni wakiwemo waandishi wawili wa habari wa Marekani, mfanyakazi wa shughuli za misaada wa Marekani na wafanyakazi wawili wa shughuli za misaada wa Uingereza.

Mwanamgambo wa kundi la IS katika mojawapo ya picha wanapotishia kuwakata vichwa mateka wao.
Mwanamgambo wa kundi la IS katika mojawapo ya picha wanapotishia kuwakata vichwa mateka wao.Picha: Social media website via Reuters TV

Video hiyo mpya imekuja baada ya Japani ambayo ilikuwa ikiitegemea sana mshirika wake katika kanda hiyo Jordan kusaidia katika kadhia hiyo imesema mazungumzo ya kufanikisha kuachiliwa kwa Goto kwa mabadilishano na mfungwa yamekwama.

Kundi hilo la Dola la Kiislamu IS lilikuwa limeapa kumuuwa Goto na rubani mmoja wa Jordan Maaz al-Kassasbeh ifikapo alfajiri ya Alhamisi venginevyo serikali ya Jordan inamkabidhi kwao mpiganaji wa jihadi wa kike wa Iraq aliehukumiwa kifo kwa kushiriki katika miripuko ya mabomu katika mji mkuu wa Amman hapo mwaka 2005 yaliowa watu 60.

Raia wa pili wa Japani kuuwawa na IS

Wiki iliopita kundi la IS limedai kuhusika na kukatwa kichwa kwa raia mwengine wa Japani Haruna Yukawa ambaye amejiajiri mwenyewe baada ya kumalizika kwa muda wa mwisho waliouweka wa masaa 72 ambapo ilitaka serikali ya Japani iwalipe fedha za kumgombowa dola milioni 200 sawa na kiwango ilichoahidi kutowa serikali hiyo kwa msaada usio wa kijeshi Mashariki ya Kati.

Mama wa Goto Junko Ishido amekaririwa akiwaambia waandishi wa habari "Nashindwa kupata maneno ya kuelezea jinsi ninavyohisi juu ya kifo cha kusikitisha sana cha mwanangu."Kaka yake Junichi Goto amesema alikuwa na matumaini lakini sasa matumaini hayo yametoweka.

Junko Ishido Mama wa mwandishi Kenji Goto akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Tokyo. (01.02.2015)
Junko Ishido Mama wa mwandishi Kenji Goto akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Tokyo. (01.02.2015)Picha: Reuters

Mke wa Goto Rinko wiki iliopita alivunja ukimya wake kusihi kurejeshwa kwa mume wake huyo.Wanandoa hao walikuwa wamebarikiwa mtoto wao wa pili wiki chache kabla ya Goto kuondoka kuelekea Syria mwaka jana katika jaribio la kumtafuta rafiki yake Yukawa ambapo baadae akaja kutekwa nyara yeye mwenyewe.

Jordan yaapa kunusuru maisha ya rubani

Kufuatia kuuwawa kwa Goto Jordan imeapa itafanya kila iwezalo kumuokowa rubani wake Maaz al-Kassasbeh anayeshikiliwa na kundi hilo la Dola la Kiislamu ambaye walimteka baada ya ndege yake kuanguka nchini Syria hao mwezi wa Disemba.

Kundi la IS limekuwa likidai kuachiliwa kwa mpripuaji wa kujitowa muhanga wa kike aliyehukumiwa kifo nchini Jordan Sajida al -Rishawi ili kuyanusuru maisha ya Kassasbeh madai ambayo serikali imekubali kuyatekeleza ili mradi inapatiwa uthibitisho kwamba rubani huyo yuko hai.

Rubani wa Jordan Luteni Maaz al- Kasassbeh anayeshikiliwa mateka na IS na mpripuaji wa kike wa kujitowa muhanga Sajida al - Rishawi alioko gerezani Jordan.
Rubani wa Jordan Luteni Maaz al- Kasassbeh anayeshikiliwa mateka na IS na mpripuaji wa kike wa kujitowa muhanga Sajida al - Rishawi alioko gerezani Jordan.Picha: picture-alliance/Jordan News Agency

Baba wa rubani huyo Safi Kassasbeh ameisihi serikali ya Jordan kuyaokowa maisha ya mtoto wake huyo wa kiume kwa kila hali.

Baraza la mabalozi wa nchi za Kiarabu nchini Japani wamelaani kitendo hicho cha kishenzi cha kumuuwa kwa kumkata kichwa mwandishi wa habari wa Japani kwamba kimefanyika kwa kutumia jina la Uislamu.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/

Mhariri : Hamidou Oummilkheir