Dunia yaahidi kuiokoa "mama dunia"
3 Juni 2017Mkataba wa Paris ni makubaliano ya mabadiliko ya tabia nchi. Hatua ya Trump ilikuwa "makosa makubwa", amesema Donald Tusk , mmoja wa maafisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya.
Mataifa mengine , ikiwa ni pamoja na India, yameonesha ishara ya kuendelea na mkataba huo . Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema kwamba wakati Marekani ilipaswa kubakia katika mkataba huo uliofikiwa mwaka 2015 , hatamhukumu Donald Trump.
Trump alitangaza kujitoa kutoka mkataba huo siku ya Alhamis , akizungumzia kuhusu matamshi yake wakati wa kampeni ya urais nchini Marekani ya "Marekani kwanza". Alisema kushiriki katika mkataba huo kutakandamiza uchumi wa Marekani, kupoteza fursa za ajira, kudhoofisha uhuru wa nchi hiyo na kuiweka nchi hiyo katika hali ya kudumu ya kutoweza kufanya chochote.
Maafisa katika utawala wake, ikiwa ni pamoja na makamu wa rais Mike Pence na mkuu wa idara ya ulinzi wa mazingira Scott Pruitt, wamesema siku ya Ijumaa kwamba makubaliano ya Paris yanaweka mzigo wa ziada kwa Marekani. "Ni kuhamisha utajiri kutoka katika uchumi imara kabisa duniani kwenda katika nchi nyingine duniani", Pence alisema katika televisheni. Kulikuwa na mchanganyiko wa mshangao duniani kote.
Ufaransa na majimbo ya Marekani
Ufaransa imesema itafanya kazi pamoja na majimbo nchini Marekani pamoja na miji kuendelea kupambana dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi. Magavana wa mji wa New York , Califonia na Washington wametangaza kuunda kile kitakachofahamika kama "Muungano wa mazingira" ambao utatumia malengo ya mkataba wa Paris.
Tasnia yenye nguvu ya viwanda vya magari nchini Ujerumani imesema Ulaya itahitaji kutathmini upya viwango vyake vya mazingira kuweza kuendelea kuwa katika ushindani baada ya uamuzi wa Marekani , ambao umeuita kuwa ni "wa kusikitisha".
Shirika la utabiri wa hali ya hewa duniani linakadiria kwamba kujitoa kwa marekani kutoka katika mkataba huo wa kupunguza utoaji wa gesi zinazoharibu mazingira kunaweza kuongeza ujoto kwa nyuzi joto 0.33 Celsius ifikapo mwishoni mwa karne hii katika hali ambayo itakuwa mbaya zaidi.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel , binti wa mchungaji ambaye kwa kawaida huweka imani yake mbali kidogo na umma, amesema mkataba huo ulihitajika "kuhifadhi kuumbwa kwetu".
"Kwa kila mtu ambaye hali ya baadaye ya sayari yetu ni muhimu, Nasema tuendelee katika njia hii ili tufanikishe kwa ajili ya mama yetu dunia", alisema huku alishangiriwa na wabunge.
Mjini Paris rais Emmanuel Macron aligeuza kauli mbiu ya rais Trump ya "Ifanye Marekani kuwa imara tena", na kusema kwa lugha ya Kiingereza kwamba muda umefika "kuifanya sayari yetu kuwa imara tena".
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Bruce Amani