Dunia yaadhimisha wiki ya maji
17 Agosti 2009Huku ulimwengu ukianza kuadhimisha wiki ya maji hii leo, hatua ya kuongezeka biashara ya maji imesababisha kuwepo haja ya kuanzisha mkataba wa kimataifa utakaothibitishwa kisheria kuhusu maji, utakaohakikisha hakuna mtu atakaenyimwa maji duniani kutokana na kushindwa kuyalipia.
Tunatakiwa kuyafanya maji yawe kama sehemu ya haki za binaadamu, anasema Maude Barlow, mshauri wa ngazi ya juu wa Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika masuala ya maji. Bibi Barlow anasema Tume ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa ya Geneva ni sehemu nyeti ya kupendekeza uwepo wa mkataba wa aina hiyo. Lakini, anasema suala hilo lingependeza zaidi kama lingeidhinishwa na nchi 192 wanachama wa Umoja wa Mataifa.
Umoja wa Mataifa umesema kiasi watu milioni 880 wengi wao katika nchi zinazoendelea duniani wanakosa huduma ya maji safi na salama. Ifikapo mwaka 2030 kiasi watu bilioni nne wanaweza wakawa wanaishi katika maeneo yenye uhaba mkubwa wa maji, hasa Kusini mwa Asia na China. Utafiti uliofanywa na Shirika la Mpango wa Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), umeonyesha kuwa soko la usambazaji maji duniani, usafi na upatikanaji wa maji ni zaidi ya dola bilioni 250 na huenda ikaongezeka kwa karibu dola bilioni 660 ifikapo mwaka 2020.
Patricia Jones, mtaalamu wa maji na meneja wa mpango wa Haki ya Mazingira, ameliambia shirika la habari la IPS kuwa Marekani ilijadiliana kupinga uteuzi wa mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa juu ya haki ya binaadamu kupata maji wakati wa uchaguzi kwenye Tume ya Haki za Binaadamu mwezi Machi, mwaka 2008. Bado, mtaalamu huru aliteuliwa kwa muda wa miaka mitatu, kuyasaidia mataifa wanachama kutambua uwezo na nafasi ya haki ya binaadamu kupata maji na kuishi katika mazingira safi. Bibi Jones alinukuu hotuba ya Rais Barack Obama aliyoitoa mara alipoapishwa rasmi kuingoza nchi hiyo Januari, mwaka huu aliposema nanukuu “Kwa watu wa mataifa masikini, tunaahidi kufanya kazi nyuma yenu kuhakikisha mashamba yenu yanastawi na maji safi yanatoka,'' mwisho wa kunukuu.
Aidha, Bibi Jones anasema hivi karibuni Wizara ya Mambo ya Nchi za nje ya Marekani ilishiriki kutoa ushauri kuhusu haki ya binaadamu kupata maji na mazingira safi. Bibi Jones anaongeza kuwa wawekezaji wanatakiwa wahakikishe wanamaliza tatizo la maji kwa kuyafanya maji kuwa haki ya binaadamu.
Kwa upande wake, Bibi Barlow anasema manispaa nyingi duniani zinageuza taratibu za ubinafsishaji wa huduma zao za maji. Bibi Barlow anasema jumuiya ya kimataifa inatakiwa kuziangalia nchi zenye nguvu zinazotafuta usambazaji wa maji nje ya mipaka yao, kama zilivyofanya katika mafuta. Anaitolea mfano China ambayo tayari imeanza kujenga bomba la kuvuta maji kutoka katika milima ya Himalayas iliyopo katika jimbo la Tibet.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (IPS)
Mhariri: Sekione Kitojo.