1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dr.Condoleeza Rice Addis Ababa

Ramadhan Ali5 Desemba 2007

Waziri wa nje wa Marekani dr.C.Rice ana jumla ya mazungumzo leo na viongozi wa kiafrikahuko Addis Ababa.

https://p.dw.com/p/CXKy
Condoleezza RicePicha: AP

Waziri wa nje wa Marekani Dr.Condoleeza Rice, amewasili mapema asubuhi ya leo mjini Addis Ababa,Ethiopia kwa mazungumzo na viongozi wa kiafrika yenye shabaha ya kutatua migogoro ya muda mrefu ya Maziwa Makuu,Somalia na hata Sudan.

Akiwa katika ziara yake ya pili tu Afrika kusini mwa jangwa la sahara,Dr.Rice aliewasili Addis Ababa mapema asubuhi ya leo,waziri wa nje wa Marekani amesema anataka kusukuma mbele juhudi za kuitatua mizozo hii kupitia msururu wa mazungumzo na mikutano na viongozi wa kiafrika wakati wa ziara yake ya masaa 24 mjini Addis Ababa.

Dr.Rice alisema na ninamnukulu,

“Nimeingiwa na wasi wasi mno kwa misukosuko mingi iliopo barani Afrika.” Aliwaambia hayo maripota aliosafiri nao kuelekea Addis Ababa,ambayo pia ni makao makuu ya umoja wa Afrika.

Dr.rice anapanga leo kukutana na viongozi wa Uganda,Burundi na Rwanda pamoja na mawaziri kutoka jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo.Anajadiliana nao ugomvi katika Maziwa Makuu .

Rais Joseph Kabila wa JKK hakuweza kwenda Addis Ababa kwa kikao cha leo –kwa muujibu alivyoarifu afisa aliefuatana na Dr.Rice.

Shabaha ya Dr.Rice ni kutunga mkakati pamoja na viongozi wan chi hizo kukabili kile ambacho Washington imekiita “vikosi dhaifu” –vile vya FDLR la Rwanda linalojumuisha viongozi mashuhuri waliohusika na mauaji ya halaiki ya 1994 na lile jeshi la waasi nchini Uganda la Lord Resistance Army (LRA).Na pia Jeshi la waasi linaloongozwa na jamadari wa kitutsi Laurent Nkunda huko mashariki mwa Kongo.

Katika kikao chake na wakuu wa Sudan mjini Addis,Dr.Rice amearifu atajaribu kuzuwia yale makubaliano kati ya serikali kuu ya Khartoum iliopo kaskazini na kusini mwa Sudan.Kuporomoka kwake kunatishia kuripuka upya vita vya kienyeji.

Waziri wa nje wa Marekani,halkadhalika, alipangwa kuona na rais Abdullahi Yusuf Ahmed wa Somalia kujadiliana nae juu ya juhudi zilizofanywa hivi punde kuleta amani nchini Somali ambayo imezongwa na vita vya kienyeji tangu 1991.Rais wa Somalia lakini, anaugua hospitalini nchini Kenya.

Marekani ina azma pia ya kukabiliana na maafa ya kibinadamu,kuwatenga upande wale wenye siasa kali na kuhimiza kuanza kazi kwa vikosi vya Umoja wa afrika vya kuhifadhi amani nchini Somalia.

Ethiopia nayo, inavutana na hasimu yake mkubwa Eritrea juu ya mpaka.Majirani hawa 2 wamepigana vita kufafanua mpaka wao hapo 1998-2000-vita vilivyochukua maisha ya watu 70.000.

Dr.Rice ana ajenda kubwa na ndefu leo Addis Ababa.