DRC yatangaza kulegeza masharti ya kukabiliana na corona
22 Julai 2020Kuanzia Jumatano, baa, migahawa, usafirishaji na shughuli nyingine zinaruhusiwa kufanya kazi. Shule zitafungua Agosti 3, huku nyumba za ibada zikiruhusiwa kufungua milango Agusti 15.
Akilihutubia taifa usiku wa kuamkia Jumatano(22.07.2020), rais Félix Tshisekedi aliwaambia wananchi, kile walichokuwa wakisubiri kwa muda mrefu, yaani kuanzishwa tena kwa shughuli mbalimbali za kimaisha.
"Kuanzia Agosti tatu, shule pamoja na vyuo vikuu vitafungua milango yake, na hiyo kipaumbele ni kwa madarasa ya mwisho. Na ifikapo Agusti 15, makanisa yatafungua milango yake." alisema Rais Tshisekedi .
Akizungumza na DW, baada ya kusikiliza hotuba ya rais, Jeremie Kinyangwa, mwanachama wa chama cha waalimu wa kiserikali katika eneo la Beni amesema, kuwa watarudi shuleni baada ya serikali kuwalipa mishahara yao waalimu ambao bado hawajasajiliwa na serikali.
Amesema kwamba kuna mikutano ya waalimu inayoandaliwa, ili kuchukuwa uamuzi wa pamoja kwani waalimu ambao bado hawajasajiliwa, walipitia kipindi kigumu wakati shule na shughuli mbalimbali vilipofunwa ili kuepusha maambukizi ya Covid-19.
Na wakati makanisa yakijiandaa kufungua milango yao ifikapo Agusti 15, baadhi ya wachungaji wanadhani kwamba kuchelewesha kufunguliwa kwa shughuli makanisani, kunadhihirisha kwamba viongozi wa serikali hawajampatia Mungu nafasi ya kwanza katika maamuzi yao.
Ifahamike kuwa safari za wakaazi kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine, zitaanza pia Agusti 15 sambamba na kufunguliwa kwa bandari, viwanja vya ndege pamoja na kufunguliwa kwa mipaka ya nchi.
Hali ya dharura ya kiafya, ilichukuliwa na rais Félix Tshisekedi mwezi Machi, ili kupunguza maambukizi ya Covid-19. Hali hiyo iliathiri maisha ya baadhi ya wakaazi, wanaofanya kazi za vibarua ilikuhudumia familia zao.
John Kanyunyu, DW-Beni