DRC yashutumu jumuia ya kimataifa suala la amani
21 Julai 2022Matamshi hayo yamejiri siku chache tu baada ya tume ya umoja wa Mataifa ya kulinda amani nchini humo (MONUSCO) kutangaza kuwa haina uwezo wa kukabiliana na waasi wa M23 ambao Kinshasa inawataja kuwa magaidi wanaoungwa mkono na Rwanda.
Kauli hiyo ya serikali ya Kongo imejiri jana Jumatano, wakati mapigano yakiendelea katika eneo la Rutshuru mkoani Kivu Kaskazini, baina ya wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na waasi wa M23 ambao Kinshasa inawataja kuwa kundi la kigaidi linaloungwa mkono na Rwanda.
Soma pia:MONUSCO:Haipo tayari kukabiliana na M23
Serikali ya Kongo imesema ipo tayari kutafuta amani, lakini haipaswi kuendelea kuona raia wake wakifa na wengine kukimbia kila siku.
Kinshasa inatambua kazi iliyofanywa na Monusco kuhusu usalama nchini humo, lakini bado inasisiti kwamba inawajibu wa kusaidiana na mamalaka za nchi hiyo katika kulinda amani katika taifa hilo ambalo halia ya usala imekuwa ikidorora katika baadhi ya maeneo.
Waziri Patrick Muyaya, msemaji wa serikali ya Kongo alisema wakilinganisha uwezo wa kijeshi ilionao MONUSCO ya sasa na ile ya miaka 10 iliopita wakati kundi la waasi la M23 liliposhindwa katika uwanja wa mapambano.
"Tunaamini kwamba leo jumuiya ya kimataifa inaweza kufanya zaidi ya kauli za kidiplomasia." alisema na kuongeza kwamba jumuiya ya kimataifa inawajibika kwa pamoja kwa hali ambayo DRC inapitia kwa sasa
Upinzani: Serikali inawajibika kwa usalama wa raia
Kwa upande wake, upinzani umeshindwa kuelewa kwa nini serikali inapeleka lawama zake kwa jumuiya ya kimataifa kuhusu tatizo ambalo ni lazima kutatuliwa na mamlaka ya Kongo.
Jean-Baptiste Kasekwa ambaye ni mbunge wa kitaifa kutoka muungano wa upinzani wa Lamuka, alishauri Monusco kujiondoa ili kuruhusu serikali kutekeleza majukumu yake ya kuwalinda Wakongomani na kutekeleza uadilifu wa eneo la kitaifa.
Soma pia:Baadhi ya makundi DRC yapinga kikosi cha jeshi la Afrika Mashariki
Alisema anasikitishwa na maneno yaliotolewa na msemaji wa serikali, ya kuvua jukumu lake la kulinda amani na usalama wa raia na badala yake kuwadhirihirishia wakongomani kwamba jukumu la kuleta amani ni la jumuia za kimataifa.
"Jukumu la kwanza la kulinda nchi na usalama wa wanainchi ni la serikali, kusukuma jukumu hili kwa watu wa nje ni kukwepa jukumu kwa uwazi."
Alisema mwanansiasa huyo na kuongeza kuwa, wananchi wanachohitaji ni kurudi katika makazi yao na kuweza kujishughulöisha na masuala ya kujenga nchi, katika hali ya usalama na amani kama mataifa mengine.
Hayo yote yamejiri wakati sasa tayari zaidi ya mwezi mmoja tangu waasi wa M23 waudhibiti mji wa Bunagana ambao ni kituo muhimu katika eneo hilo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.