DRC: Wanamgambo wa Maimai waua watu 5 Kivu Kusini
29 Mei 2020Shambulio hilo llimedaiwa kufanywa na wanamgambo wa Mai-Mai dhidi ya kambi ya wakimbizi iliyoko Mikenge katika wilaya ya Mwenga, ndani ya mkoa wa Kivu Kusini.
Kulingana na jeshi la Jamhuri ya kideokrasia ya Congo FARDC, shambulizi hilo liliendeshwa na kundi la wapiganaji Mai-Mai linaloitwa Biloze-Bishambuke dhidi ya kambi hiyo, ambayo pia iko chini ya ulinzi wa Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa MONUSCO na jeshi la Congo.
Mkuu wa ofisi ya MONUSCO hapa Kivu Kusini, Karna Soro, amethibitisha shambulizi hilo na kusema askari wa Munusco walisaidia jeshi la Congo katika mapambano dhidi ya wapiganaji hao. Karna Soro amewalaumu baadhi ya viongozi wa kisiasa kwa kuyalinda makundi yenye silaha ndani ya misitu ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na kuchochea ghasia.
Hali tete ya usalama Kivu Kusini
"Tumegundua kwamba kuna viongozi fulani wanao endelea kuhifadhi vijana hao katika misitu na kuwahimiza katika maovu hayo, lakini hata hivyo watu hao tumeanza kuwajua. Tunajifunza mbinu dhidi zaidi yao, na pia tunajifunza namna gani watu hao watajibu kwa maovu yao mbele ya vyombo vya sheria vya Congo” Amesema Soro.
Hadi sasa, hali ya usalama inabaki kuwa tete katika maeneo mengi ya mitaa ya Fizi, Uvira na Mwenga. Msemaji wa operesheni ya kijeshi Sokola yapili kusini mwa mkoa wa kivu kusini kapiteni Dieudonné Kasereka ametoa onyo kwa makundi ya wanamgambo kuweka silaha chini na kuungana na harakati za amani nchini Congo.
Makundi kadhaa ya wapiganaji wa Mai-Mai yanapatikana ndani ya mkoa wa Kivu kusini, mengi yakiwa ya kikabila. Operesheni za kijeshi zimefanyika kila mara dhidi ya makundi hayo lakini hadi sasa, hayaja tokomezwa.