DRC: Mikoa ya Ituri na Kivu Kaskazini yawekwa chini ya jeshi
4 Mei 2021Tangazo hilo lilitolewa Jumatatu jioni na Rais Felix Tshisekedi katika hotuba fupi iliyotangazwa kupitia redio na televisheni ya kitaifa. Mamlaka ya utawala na ya kimahakama sasa yatakuwa mikononi mwa jeshi na polisi.
Kuanzia Alhamisi, magavana wa mikoa hiyo miwili watawaachia nafasi askari, manaibu wa magavana watawachia polisi, halafu mawaziri wa mikoa watawachia wanajeshi watakaoteuliwa na magavana hao wa kijeshi.
Hali ya wasiwasi mashariki mwa DRC kufuatia mashambulizi
Hakuna kinga ya kibunge wakati wa utawala huu maalum, kwani mabunge ya mikoa hiyo yamesimamishwa. Mahakama ya kiraia zitabadilishwa na korti ya kijeshi. Rais Félix Tshisekedi amewaomba raia kuunga jeshi mkono.
"Kwa hivyo naalika kila mkongomani popote alipo, kwa uhamasishaji wa jumla ili kusaidiana na vikosi vyetu vinavyoulinda usalama wa eneo letu. Ni lazma raia wote kusimama pamoja na kuunga mkono wanajeshi wetu," amesema Tshisekedi.
Magavana kuripoti kwa Waziri wa Ulinzi
Wakati wa hali hiyo Maalum, magavana wataripoti kwa Waziri wa Ulinzi wa Kitaifa. Viongozi hao wapya watakuwa na mamlaka zaidi, ila wataitumia wakiheshimu sheria, kama inavyoainishwa na amri iliyosomwa na Kasongo Mwema Yambayamba, msemaji wa Rais Tshisekedi.
Vita visivyokwisha vya makundi ya wanamgambo nchini Congo
"Wana uwezo wa kufanya misako mchana na usiku katika majumba; kuwatenga watu waliopatikana na hatia na wale wasio na makao katika maeneo yaliyo chini ya ulinzi. Kutafuta na kuamuru ukabidhianaji wa silaha. Kukataza machapisho pia maandamano wanayoyumbisha usalama wa umma," amesema Kasongo Mwema.
Hali hiyo ni ya mwezi mmoja lakini itaendelea kutathminiwa baada ya kila wiki mbili. Hata hivyo, wabunge na mawaziri wa mikoa hiyo wataendelea kushughulikiwa kijamii, licha ya kuwa wamesimamishwa kazi.