DRC: Makundi ya kijamii yaandamana Beni dhidi ya machafuko
27 Novemba 2018Wazee wa busara wa mji wa Beni katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo pamoja na viongozi wa madhehebu mbalimbali wa wilaya ya Beni kwa jumla wameandamana leo, kuunga mkono operesheni za pamoja za jeshi la Umoja wa Mataifa na jeshi la Kongo FARDC dhidi ya waasi wa ADF. Maandamano hayo yanafanyika wakati waasi wa ADF wakiwa wamewauwa raia wawili usiku wa kuamkia leo katika mji mdogo wa Oicha.
Mwanasheria Nathan Lebabo, msemaji wa waandamanaji, akisoma mbele ya Meya wa mji wa Beni, barua waliyoituma kwa viongozi wa serikali ya Congo pamoja na wa Umoja wa Mataifa.
Maandamano haya, yakiwa yanalenga kuwahimiza wanajeshi wa Kongo pamoja na wale wa Umoja huo kupitia kikosi chake maalumu cha kuingilia kati FIB, kuwatokomeza waasi wa Uganda ADF wanaotajwa kuhusika katika mauaji ya raia katika eneo hili kwa kuwakata kwa mapanga.Waandamanaji walitumia fursa hiyo kulaani ukimya wa jumuia ya kimataifa,kuhusu mauwaji ya kila mara katika eneo hili.
Akiwahutubia waandamanaji, baada ya kumkabidhi barua hiyo , Meya wa mji wa Beni Bwanakawa Nyonyi, aliahidi kuituma kwa viongozi wa serikali mjini Kinshasa, na kuwaarifu wakazi wa Beni wachachokusudia kukifanya,ili amani ya kudumu iweze kurudi katika mji na wilaya ya Beni .
Naye mwenyekiti wa mashirika ya kiraia katika mji huo Kizito Bin Hangi, akiwa mmoja wa walioandamana, aliiambia DW, kuwa anafurahi kuandamana na wazee wa mji,katika harakati za kusaka amani, na kuyaunga mkono kwa majeshi ya Congo na Monusco.
Wakati huo huo Sheikh Aliamin Othman alizipinga kauli kwamba waislamu wa Bei wameshindwa kuchukua hatua ya kuwashawishi waasi wa ADF ambao wengi wao ni waislamu kuacha mauaji ya raia.
Baada ya kumkabidhi Meya barua yao, waandamanaji walielekea kwenyi ofisi kuu ya Monusco katika mji wa Beni, ambako walimkabidhi pia barua hiyo kiongozi wa kikosi cha Umoja wa mataifa Monusco .
Baadaye wataelekea katika kata ya Buili,ambako mi itafanyika ibada kwaajili ya amani itakayoongozwa na viongozi wa madhehebu mbalimbali .
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman