Dortmund yateleza uwanjani Wembley
14 Septemba 2017Ilichukua dakika nne tu kwa Tottenham Hotspur kudhihirisha mapungufu katika safu ya ulinzi ya Borussia Dortmund ya Ujerumani wakati Son Heung-Min alipoingia katiak eneo la hatari bila kukabiliwa na mabeki wa Dortmund na kipa Roman Burki akishindwa kulilinda lango lake vizuri.
Son, aliyewahi kuichezea Hamburg na Bayer Leverkusen, alitwanga mkwaju juu ya wavu kuipa Tottenham hali ya kujiamini katika mechi iliyochezwa uwanja wa Wembley jijini London, hatua ya kwanza ya kuvunja laana ya Tottenham kucheza katika uwanja huo.
Dakika saba baadaye Shinji Kagawa alimgongea Andriy Yarmolenko ambaye alivurumisha kombora kona ya kushoto ya lango la Tottenham na kipa Hugo Lloris hakuweza kuokoa. Dakika ya 15 Harry Kane aliifungia Tottenham bao la pili na kuongeza la pili dakika ya 60. Kane aliisaidia timu yake ya Tottenham kuvunja laana ya kucheza katika uwanja wa Wembley kwa kuishinda Dortmund mabao 3-1 katika mchuano huo wa kundi H.
Kwa kuwa uwanja wao wa White Hart Lane unafanyiwa matengenezo, Tottenham wanachazea mechi zao za nyumbani katika uwanja wa timu ya taifa ya England, Wembley msimu huu na hizo zimekuwa habari mbaya kwa timu hiyo ya kocha Mauricio Pochettino. Baada ya kupoteza mechi nane kati ya 12 walizocheza Wembley, mchango wa Kane ulihakikisha Tottenham wanafurahia usiku utakaokumbukwa katika historia ya klabu hiyo.
"Ilikuwa muhimu sana kushinda, tunafurahia sana. Tulijiimarisha katika kipindi cha pili na tulitumia mbinu," alisema kocha Pochettino. "Ni zaidi ya pointi tatu. Timu imekomaa zaidi sasa. Harry Kane alicheza vizuri sana," akaongeza kusema.
Kocha wa Borussia Dortmund, Peter Bosz, amesema, "Ni wazi hatukujipanga vyema nyuma katika safu ya ulinzi katika wakati muhimu tulipotakiwa kuwa macho. Hatukuifunga mianya nyuma ya mabeki wanne wa nyuma na hilo lilikuwa na umuhimu mkubwa."
Dortmund waliwasili jijini London wakiwa hawajafungwa msimu huu, lakini kikosi chao kikibiliwa na majeraha, huku Marco Reus, Raphael Guerreiro, Andre Schurrle na Marcel Schmelzer wakiwa miongoni mwa wachezaji wanaouguza majeraha.
Katika mechi nyingine ya kundi H, mabingwa watetezi Real Madrid walianza vyema kampeni yao kwa kuichapa APOEL Nicosia 3-0 nyumbani Barnebau mjini Madrid. Cristiano Ronaldo alifunga bao la kwanza dakika ya 12 na kuongeza la pili kwa njia ya penalti dakika ya 51 ya mchezo. Sergio Ramos aliikatisha matumaini Nicosia kwa kufunga bao la tatu dakika ya 61.
Leipzig yatoka sare na Monaco
Timu nyingine ya Ujerumani, RB Leipzig ilitoka sare ya bao moja kwa moja na Monaco ya Ufaransa nyumbani Red Bull Arena mjini Leipzig, katika mechi yake ya kwanza kabisa kwenye mashindano ya Champions League. Emil Forsberg aliufumania wavu wa Monaco dakika ya 33 kabla Youri Tielemans kukomboa dakika moja baadaye.
Bao la Forsberg litaingia katika vitabu vya historia kama bao la kwanza la RB Leipzig katika ligi ya mabingwa, ingawa halitarajiwi kuwa la mwisho. "Ni kitu maalumu sana kufunga bao la kwanza la Leipzig katika Champions League," alisema Forsberg baada ya mtanange huo wa kundi G. "Najivunia sana," akaongeza kusema.
Timo Werner, mshambuliaji wa Leipzig, mara mbili alikaribia kufunga katika kipindi cha kwanza, akawa kitisho kipindi cha pili lakini hakufaulu kuona lango. "Bila shaka tulikuwa na hisia za kipekee leo. Tulitaka sana kushinda, lakini kwa bahati mbaya hatukufanikiwa," akasema Werner mwenye umri wa miaka 21.
Katika matokeo mengine ya kundi G Porto ya Ureno ilifungwa mabao 3-1 na Besiktas ya Uturuki.
Manchester City iliinyoa bila maji Feyenood mabao 4-0 katika mechi ya kundi F iliyochezwa Rotterdam, Uholanzi. Shaktar Donetsk ya Ukraine iliishinda Napoli ya Italia mabao 2-1, katika mpambano mwingine wa kundi F.
Kwingineko Liverpool ilitoka sare ya mabao 2-2 na Sevilla nyumbani Anfield. Roberto Firmino wa Liverpool alikosa penalti kipindi cha kwanza na hivyo kosa lake kuigharimu Liverpool katika mchuano huo wa kundi E. Mashabiki walikuwa wakishangilia Anfield wakati Liverpool ilipokaribishwa katika mashindano ya Champions League, na ikiongoza kwa mabao mawili kwa moja, lakini nderemo zikasita wakati Joaquin Correa wa Sevilla alipofunga bao la kusawazisha.
Mechi nyingine ya kundi E ilikuwa kati ya Maribor ya Slovenia na Spartak Moscow ya Urusi ambapo zilizoka sare ya bao 1-1.
Mwandishi: Josephat Charo/afpe/ape
Mhariri: Iddi Ssessanga